************************
Wafugaji wa nyuki katika halmashauri ya Wilaya ya Itigi Mkoani Singida wamepatiwa mafunzo ya ufugaji wa nyuki Ili kuongeza uzalishaji na tija katika kuongeza thamani mazao ya nyuki kupitia mradi wa EIF TIER II.
Awali akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi Idara ya Utawala na Maendeleo ya Rasilimali watu, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Bw. Edward Nkembo Amesema kuwa anawashukuru wafugaji wote waliofika Kwa ajili ya kupatiwa mafunzo ya mnyonyoro wa thamani wa asali Mkoani Singida.
Bw. Nkembo Amesema kuwa mafunzo haya ambayo yataendeshwa na Shirika la kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Singida kupitia mradi wa Enhanced Intergrated Framework (EIF) ambao ni mradi wa kuwajengea uwezo wajasiriamali wadogo na wa kati walioko katika mnyororo wa thamani katika mazao ya Asali Mkoa wa Singida, Mawese Kigoma, Mbogamboga na matunda kwa Mkoa wa Mara na Simiyu pamoja na Mwani na Dagaa Kwa Tanzania Visiwani.
"Serikali kupitia mradi huu wa Enhanced Intergrated Framework (EIF) umedhamiria kujenga Viwanda Viwili vidogo katika kata za Mwamagembe na Itigi pamoja na kuwawezesha wajasiriamali kupata mizinga ya kisasa ya kuvunia asali kupitia vikundi vyenu". Amesema Bw. Nkembo.
Bw. Nkembo ameongeza kwa kusema kuwa Viwanda hivyo vitasaidia kusindika asali kwa ubora na Viwango vya kimataifa na kuyafikia zaidi masoko ya ndani na nje ya nchi.
Awali akielezea utekelezaji wa mradi wa kuwajengea uwezo wajasiriamali wadogo na wa kati Kaimu mratibu na Msimamizi wa mradi wa EIF TIER II kutoka Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Bi. Natasha Ngowi amesema mafunzo hayo yamelenga kuwaelimisha wajasiliamali hao kuhusu uchakataji na usindikaji wa zao la asali na uongezaji thamani wa bidhaa nyinginezo zitokanazo na nyuki.
Bi. Natasha amesema kuwa lengo jingine la mradi huu ni kuimarisha ushindani wa Biashara ndogo na za kati Ili kuyafikia masoko ya ndani na ya kimataifa, kupunguza umaskini na kutoa ajira kwa Wanawake na Vijana.
Bi. Natasha ameongeza kwa kusema kuwa mradi huu unafadhiliwa na chombo kinachoitwa Enhanced Integrated Framework (EIF) ambacho kipo katika shirika la Biashara la Dunia (WTO) Kwa kushirikiana na UNDP na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ufadhili wa mradi huu na Muda wa utekelezaji wake ni miaka mitatu na utatekelezwa Kwa upande wa Tanzania bara na Zanzibar. Meneja wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Singida Bi. Agness Yesaya ameeleza kuwa kazi kubwa inayofanywa na SIDO Mkoa wa Singida ni kuwajengea uwezo wajasiriamali kwa kuwapa teknolojia, mafunzo, kuhakikisha wanaongeza thamani ya mazao yao na kuwahakikishia upatikanaji wa vifungashio vinavyoendana na soko.
Naye Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi Bw. Jonathan Dulle amesema kuwa, Halmashauri imepokea Kwa mikono miwili Ujenzi wa Viwanda Viwili ambavyo vitajengwa katika eneo la Wamagembe na Itigi ambao utagharimu fedha za kitanzania Shilingi milioni 150 unakwenda kutibu changamoto ikiwemo usindikaji wa asali.
Bw. Dulle ameongeza Kwa kusema kuwa Ujenzi wa Viwanda hivyo utapelekea kuongezeka mapato kwa halmashauri ya Wilaya ya Itigi na Serikali kwa ujumla kutokana na tozo itakayopatikana katika bidhaa ya Asali na Nta, itaongeza ajira na kipato kwa wananchi.
0 Comments