***********************
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo atashiriki kwenye uzinduzi wa makala maalumu iitwayo ‘Royal Tour’ jijini New York nchini Marekani.
Makala hayo maalumu ambayo mchakato wake umefanyika kwa takribani mwaka mzima umemshirikisha moja kwa moja Rais Samia akiwa katika vivutio mbalimbali vya utalii nchini Tanzania kwa lengo la kuongeza watalii na kuvutia wawekezaji.
Uzinduzi huo wa aina yake unaohudhuriwa na takribani watu 400 umepangwa kufanyika kwenye Jumba Mashuhuri la Makumbusho liitwalo Guggenheim kuanzia saa moja na nusu za usiku za Marekani, sawa na saa nane na nusu usiku kwa Afrika Mashariki.
Miongoni mwa washiriki ni pamoja na wakuu wa taasisi za biashara za kimataifa, waongoza utalii wa kimataifa, viongozi wa kisiasa, mashirika ya kimataifa, waandishi wa habari na Watanzania waishio Marekani.
Pia wafadhili na wadau mbalimbali zikiwemo taasisi za uhifadhi kama TANAPA, NCAA, TTB, TAWA, TFS na makundi ya wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Tanzania wakiwakilishwa na CTI, TBA, TPSF, TATO na CEOrt wanahudhuria.
Shughuli hiyo itaoneshwa mubashara kupitia televisheni za Marekani kwenye mfumo wa utangazaji wa umma (PBS) kupitia kituo cha televisheni cha WTTS yenye watazamaji takribani milioni 3.5 na baadaye makala hayo itaoneshwa kwenye zaidi ya chaneli 300 zinazowafikia takribani asilimia 86 ya Wamarekani.
Makala hayo yatazinduliwa pia jijini Los Angeles, Aprili 21, mwaka huu na baada ya matukio hayo mawili, filamu hiyo pia itarushwa kwenye mtandao wa kidijitali wa Amazon na Apple TV.
Kwa Tanzania, filamu hiyo itazinduliwa kwanza jijini Dar es Salaam tarehe 28 Aprili na baadaye visiwani Zanzibar tarehe 7 Mei.
0 Comments