Ticker

6/recent/ticker-posts

ZUNGU AKUTANA NA RAIS MWENZA WA BUNGE LA UMOJA WA ULAYA

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Bunge la Umoja wa Ulaya yamekubaliana kuimarisha ushirikiano miongoni mwao na miongoni mwa wabunge wao. Hayo yameafikiwa tarehe 02 Aprili 2022 kwenye makao makuu ya Bunge la Umoja wa Ulaya nchini Ufaransa, wakati wa mazungumzo baina ya Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu na Rais mwenza wa Bunge la Pamoja la Umoja wa Ulaya na Jumuiya ya Nchi za Afrika, Caribbean na Pasifiki (OACPS), Mhe. Prof. Carlos Zorrinho).

Mazungumzo hayo yaliyofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 41 wa Bunge la OACPS na EU ambapo Mhe. Zungu anaongoza ujumbe wa Tanzania, viongozi hao walikubaliana pia kupitia Mabunge yao kuhakikisha kuwa uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Umoja wa Ulaya na baina ya Bunge la Tanzania na Bunge la Umoja wa Ulaya unaimarishwa zaidi.

Aidha, Mhe. Zungu alitumia fursa hiyo kumwalika Mhe. Zorrinho pamoja na baadhi ya Wabunge wa Bunge la EU kuitembelea Tanzania na kujionea wenyewe hatua mbalimbali zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suhuhu Hassan katika kusukuma maendeleo ya Tanzania. Rais huyo mwenza wa Bunge la Pamoja la Ulaya na ACP alipokea mwaliko huo kwa furaha na kuahidi kufanya ziara hiyo nchini siku zijazo akiambatana na baadhi wa Wabunge wa Bunge la Umoja wa Ulaya. Alieleza kuwa Tanzania ni moja ya nchi za kipaumbele kwa Umoja wa Ulaya na Bunge hilo linafurahishwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Tanzania kusimamia ajenda za maendeleo na ustawi wa jamii, hususan katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuimarisha demokrasia na haki za binadamu.

Mhe. Zungu alimwomba mwenyeji wake huyo kuwahamasisha wawekezaji wa Ulaya waendelee kuja kuwekeza nchini kwenye masuala ya uchimbaji wa gesi na maeneo mengine, kwani Tanzania imebarikiwa kuwa na fursa nyingi za uwekezaji.

Viongozi hao walihitimisha mazungumzo yao kwa kusisitiza umuhimu wa kuongeza ushawishi wa mabunge yao kutoa miongozo itakayoimarisha ushirikiano baina ya Umoja wa Ulaya na nchi za Afrika, Carribean na Pacific pamoja na masuala yanayohusu kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha amani eneo la ukanda wa maziwa makuu hususan nchini Msumbiji. Professa Zorrinho alieleza kuwa EU ina imani kubwa zaidi na Tanznaia katika masuala ya usuluhishi wa migogoro na kukuza amani duniani.

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Zungu aliambatana na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na kwenye Umoja wa Ulaya, Mhe. Jestas Abuok Nyamanga na maafisa wengine waandamizi wa Ubalozi na Bunge.



Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Assan Zungu (kushoto) akisalimiana na Mhe. Professa Carlos Zorrinho, Rais mwenza wa Bunge la Pamoja la OACPS na EU (kulia) wakati wa kikao chao kilichofanyika katika ofisi za Bunge la EU zilizopo Strasbourg,Ufaransa. Tukio hilo lilifanyika tarehe 02 Aprili,2022 wakati wa Mkutano wa Bunge la Pamoja la OACPS na EU unaoendelea Strassbourg.





Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Mussa Assan Zungu (aliyesimama) akichangia katika moja ya kikao cha Bunge la Pamoja la OACPS na EU kilichofanyika katika ofisi za Bunge la EU zilizopo Strasbourg, Ufaransa. Tukio hilo lilifanyika tarehe 02 Aprili, 2022. Mhe.Zungu analiwakilisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika vikao hivyo.




Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Assan Zungu (katikati kulia) akiwa katika kikao chake na Mhe. Professa Carlos Zorrinho, Rais mwenza (co-President) wa Bunge la Pamoja la OACPS na EU (wa pili kushoto) wakati wa kikao chao kilichofanyika katika ofisi za Bunge la EU zilizopo Strasbourg,Ufaransa. Tukio hilo lilifanyika tarehe 02 Aprili, 2022 wakati wa Mkutano wa Bunge la Pamoja la OACPS na EU unaoendelea Strasbourg. Kulia mwa Mhe. Zungu ni Mhe. Jestas Nyamanga, Balozi wa Ubalozi wa Jamhuri wa Muungano nchini Ubelgiji na kwenye Umoja wa Ulaya (kulia) na maofisa wengine kutoka Bunge la Tanzania na Bunge la EU.




Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Assan Zungu, (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Mhe. Balozi Dkt George Pinto Chikoti, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya OACPS (kulia) na Mhe Balozi Jestas Abuok Nyamnaga (kushoto) nje ya ukumbi kunakofanyika Mkutano wa 60 wa Bunge la OACPS unaofanyika katika ofisi za Bunge la EU jijini Strasbourg, Ufaransa. Tukio hilo lilifanyika tarehe 29 Machi, 2022. Mhe. Zungu analiwakilisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika vikao hivyo.




Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Mussa Assan Zungu (aliyesimama kulia) akibadilishana mawazo na mmoja wa Wabunge wa Bunge la Umoja wa Ulaya wakati wa Mkutano wa 41 wa Bunge la Pamoja la OACPS na EU uliofanyika katika ofisi za Bunge la EU zilizopo Strasbourg,Ufaransa. Tukio hilo lilifanyika tarehe 02 Aprili, 2022. Mhe. Zungu analiwakilisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika vikao hivyo.

Post a Comment

0 Comments