*************************
Na Hamida Kamchalla, TANGA
Wananchi wote wanaomiliki vyombo vya moto Mkoa wa Tanga wametakiwa kujisajili katika mfumo wa ukusanyaji mapato kidigitali ili kuepuka usumbufu wa kujipunguzia aduabu kwa kukosa taarifa za tozo zao.
Wito huo umetolewa na Meneja wa TARURA Mkoani hapa George Tarimo wakati akiongea na Nipashe ambapo alisema mfumo huo umeanza rasmi Aprili 1 mwaka huu na unaendelea kufanya kazi hivyo wananchi ni vizuri wakatoa ushirikiano ili kufanikisha zoezi hilo kuwa endelevu.
"Hapo awali tulikuwa tuanze kukusanya mapato ya maegesho kidigitali mwezi machi, 1 lakini lilitokea tatizo kidogo tukasimamisha zoezi hilo, lakini tangu Aprili, 1 tumeanza rasmi na kazi inaendelea" alisema Tarimo.
"Kwahiyo ninachowaomba wananchi wa Tanga wanaomiliki vyombo vya moto wajisajili kwenye huu mfumo kupitia simu zao za mikononi ili waweze kupata taarifa kupitia ujumbe mfupi, na hii itasaidia sana kukwepa kupigwa faini ya ucheleweshaji malipo, kwasababu tangu siku ya kuchajiwa unapewa siku 14 za malipo na zikipita unatozwa faini ya sh elfu 10" aliongeza.
Aidha Tarimo amewaomba wananchi hao kuwapa ushirikiano mara tu mteja atakapokuwa na tatizo au kuwa na mashaka kuhusu bili yake, kwamba wafike katika ofisi za TARURA na kupatiwa ufumbuzi wa matatizo yao kitaalamu.
"Pia nawaomba watupe ushirikiani, kwasababu mfumo huu ni mpya, pindi unapopata tatizo au kutilia mashaa bili yako ya tozo, ni vizuri basi ukawasiliana na kufika kwenye ofisi zetu za TARURA hapa mkoani na hata wilayani kwa ajili ya kupata ufafanuzi" alifafanua.
Pia Tarimo amesema wananchi wameupokea na kuridhishwa na mfumo huo na hadi sasa hawajapata tatizo au malalamiko kutoka kwa watumiaji wa vyombo vya moto kuhusu ukusanyaji huu na kueleza kwamba mfumo huo ni sahihi na utaepusha mianya ya ubadhirifu wa fedha mbichi kwakuwa zitaingia moja kwa moja serikalini bila kupita kwenye mikono ya watu" alisema.
"Kwakweli tunashukuru wananchi wameupokea na kuridhika na mfumo huu, kwasababu sasa hivi hakuna haja ya kuwa na pesa taslimu mkononi, na vilevile unaweza kulipa kwa njia ya simukupitia mitandao yote pamoja na benki za CRDB na NMB" Alibainisha Tarumo.
"Hili ni jambo lenye kheri, tofauti na zamani ambapo pia maduhuli ya serikali yanakwenda moja kwa moja kwasababu hatupokei tena fedha mbichi, hivyo fedha inakuwa inakwenda kwenye mikono sahihi, tofauti na zamani walipokuwa wanawalipa Wakala wanaokusanya fedha taslimu, na mpaka hatuna taarifa yoyote ya malalamiko kutoka kwa wateja wetu," aliongeza.
Baadhi ya madereva na wamiliki wa vyombo vya moto jijini Tanga nao walisema mfumo huo unafaa kwakuwa wanawaamini fedha zao haziwezi kuliwa tena bila taarifa ya kueleweka kutoka kwa Wakala huku walieleza kwamba mfumo wa zamani uliwapa wakati mgumu hasa pale mtuaji hana pesa mfukoni na analazimika kulipa.
Vilevile wamebainisha kwamba mfumo huo pia utawasaidia TARURA kutokana na kukusanya mapato yote kwa uhakika na kuingiza serikalini moja kwa moja lakini pia utawasaidia wao kuwa na uhuru katika ulipaji ambapo mteja anapewa muda wa wiki mbili, jambo ambalo linafanya wapate muda mzuri wa kuitafuta na kulipa tofauti na zamani.
"Huu mfumo ni mzuri na sisi tumeukubali sana, kwasababu unatupa uhuru na muda mzuri tu wa kulipia maegesho ni tofauti sana na mfumo wa zamani, ulikuwa ni kama unatuzalilisha kwamaana ukisimama wakati wa kuondoka pale ni lazima ulipe na kuna wakati wakusanyaji wanakutolea maneno mabaya mfano, ukiangalia mfukoni huna pesa na imekulazimu kusimama kwenye maegesho" alisema Saidi Shabani, dereva wa bajaji.
0 Comments