Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Uvinza wakati aliposimama kuwasalimu akiwa njiani kutoka Kigoma kurejea Mkoani Dodoma leo tarehe 24 Aprili 2022.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akisikiliza kero mbalimbali za wananchi wa Wilaya ya Uvinza wakati aliposimama kuwasalimu akiwa njiani kutoka Kigoma kurejea Mkoani Dodoma leo tarehe 24 Aprili 2022.
*************************
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amesema serikali ya awamu ya sita itakamilisha ujenzi wa barabara ya Uvinza – Malagarasi ili kufungua zaidi fursa za kiuchumi katika mkoa wa Kigoma.
Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 24 Aprili 2022 alipozungumza na wananchi wa Wilaya ya Uvinza akiwa njiani kutoka mkoani Kigoma kurejea Dodoma. Makamu wa Rais amesema serikali inatambua umuhimu wa barabara hiyo na kupitia ziara alioifanya hivi karibuni Dubai(Umoja wa Falme za Kiarabu), mfuko wa maendeleo wa Abudhabi uliiridhia kutoa fedha za ukamilishaji wa barabara hiyo.
Aidha Makamu wa Rais amewata viongozi katika ngazi za kata, wilaya na mkoa kusikiliza kero za wananchi pamoja na kuwashirikisha katika mipango ya maendeleo. Ameuagiza uongozi wa mkoa wa Kigoma kufika wilaya ya Uvinza ili kuridhiana na wananchi juu ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya soko na stendi wilayani humo.
Halikadhalika Makamu wa Rais amesema viongozi wa Wizara ya Maji na Wizara ya Nishati watafika wilaya ya Uvinza ili kutatua changamoto za maji na umeme ambazo zimetajwa kama kero ya muda mrefu wilayani humo.
Awali wananchi wa Uvinza walimueleza Makamu wa Rais changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo upungufu wa watumishi katika sekta ya Afya na Elimu katika wilaya hiyo pamoja na mradi wa maji uliogharimu bilioni 1.7 ukishindwa kutoa maji.
0 Comments