Kamanda Jumanne Muliro akizungumza juu ya uchunguzi wa kifo cha Padre Francis Kangwa wa Wilaya ya Ubungo Dar es salaam.
***************************
Na Magrethy Katengu ----Dar es saalam
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za kiuchunguzi linaendelea kuchunguza kwa kina kifo cha Padri Francis Kangwa (49) Raia wa Zambia aliyekuwa Paroko wa Parokia ya Mbezi Mshikamano iliyopo Wilaya ya ubungo Jijini Dar es salaam.
Akitoa taarifa hiyo leo Jijini Dar es Salaam Kamanda wa Kanda hiyo ACP Muliro Jumanne Muliro amesema Padri huyo alikutwa amefariki ndani ya tenki kubwa la maji lililoko nyuma ya nyumba ya makazi ya Mapadri iliyopo mtaa wa Sokoine katika jengo la Ottoman Jijini Dar es Salaam.
Aidha amesema Padri huyo alifika katika kanisa la “St. Joseph” lililopo mtaa wa Sokoine tarehe 12.4.2022 kwa ajili ya ibada maalum, na mara baada ya ibada alielekea kwenye makazi ya mapadri kujipumzisha lakini hakuonekana mpaka tarehe 15.04.2022 alipokutwa amefariki eneo hilo.
“Uchunguzi wa awali kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za kiuchunguzi unaonesha dalili kwamba Padri huyo anaweza kuwa amejiua hata hivyo Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linaendelea na uchunguzi wa kina kubaini sababu halisi iliyopelekea kifo cha Padri huyo”. Amesema ACP Muliro.
0 Comments