Ticker

6/recent/ticker-posts

UOZO WA VIUMBE VIFU CHANZO KIKUU CHA KUCHAFUKA KWA MTO MARA-PROF.MANYELE

Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya kuchunguza chanzo cha kuchafuka kwa Mto Mara Prof. Samweli Manyele akieleza sababu za kuchafuka kwa Mto huo baada ya kukamilika kwa taarifa ya Kamati hiyo ya Kitaifa iliyoundwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo Machi 12, 2022. Kushoto ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga na Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Bw. Edward Nyamanga. Komando wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania Sajenti Cosmas Aloyce Nyakaho akichukua sampuli ya Maji kwenye mto Mara ikiwa ni sehemu ya kuchunguza sababu za kuchafuka kwa Mto huo hivi karibuni Bw. Daniel Ndio - Mkurugenzi wa Udhibiti na Usimamizi wa Kemikali kutoka Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali ambae ni Mjumbe wa Kamati ya Kitaifa ya kuchunguza chanzo cha kuchafuka kwa Mto Mara akifafanua jambo mbele ya waandishi wa Habari hii leo tarehe 26.03.2022 baada ya kuainisha vyanzo vya uchafuzi katika Mto Mara. Katikati ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya kuchunguza chanzo cha kuchafuka kwa Mto Mara Prof. Samweli Manyele na Bi. Mary Maganga Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais.

***************

Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya kuchuguza chanzo cha kuchafuka kwa Mto Mara Prof. Samweli Manyele amesema kufuatia uchunguzi wa kimaabara uliofanyika kwenye sampuli zilizochukuliwa katika maji ya Mto Mara hivi karibuni imebainika kuwa chanzo kikuu cha kuchafuka kwa Mto Mara ni kusambaa kwa tope la uozo wa viumbe-vifu lililotibuliwa na mvua kubwa ilionyesha kwa kipindi cha muda mfupi.

Prof. Manyele amesema hayo leo tarehe 26.03.2022 alipokuwa akiongea na waandishi wa Habari katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa jijini Dodoma wakati akitoa ufafanuzi kuhusu taarifa ya uchunguzi wa kuchafuka kwa Mto Mara.

Aidha, Prof. Manyele amesema kuwa sababu kubwa ya kuchafuka kwa Mto Mara imetokana na mrundikano wa kiwango kikubwa cha tope lililosababishwa na uozo wa viumbe (organic matter) kilichobainika chini ya ardhi oevu ya huo.

Amevitaja viumbe hivyo ni pamoja na mimea ya matete, magugu maji na uwepo wa vinyesi vya wanyama uliosababishwa na wingi wa mifugo iliyopo katika eneo hilo. Vilevile, Kamati yake imebaini kukosekana kwa hewa ya Oxygen katika maji ya Mto Mara hali iliyopelekea vifo vya Samaki nakusema kuwa hali hiyo imetokana na mmeng’enyo wa viumbe-vifu wakati wa uozeshwaji wake chini ya maji uliosababishwa na wingi wa mimea maji kwenye eneo oevu la Mto Mara.

Katika taarifa yake Prof. Manyele amesema vipimo vya awali vya ubora wa maji vilionyesha uwepo wa mafuta hali iliyolazimu kufanyika kwa utafiti wa kina na matokeo ya sampuli yalionesha kuwa utando wa mafuta unaonekana juu ya maji ya Mto Mara unatokana na mchakato wa uozaji wa viumbe-vifu vya mimea vilivyopo kwenye eneo oevu la Mto Mara.

Kufuatia kukamilika kwa taarifa ya kina ya uchunguzi wa kuchafuka kwa Mto Mara, Kamati ya Kitaifa imeshauri maji ya Mto huo yanaweza kutumika kwenye shughuli mbalimbali za binadamu kwa kuwa sampuli zilizochukuliwa na kufanyiwa vipimo hazikuonesha kuwepo kwa kemikali za sumu na kusema kuwa viumbe kama Samaki ni salama kwa matumizi ya binadamu.

“Samaki wa Mto Mara wanaweza kutumiwa kama kitoweo bila kusababisha madhara kwa afya ya binadamu” Alisisitiza Prof. Manyele.

Kuhusu maji ya Mto Mara kuwa meusi, Kamati imesema kuwa hali ya weusi wa maji itandelea kuwepo mpaka mvua zitakaponyesha kwa wingi na kusafisha mto huo.

Ripoti hii imetokana na uteuzi uliofanywa Machi 12, 2022 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo kuchunguza chanzo cha uchafuzi wa mazingira uliojitokeza ndani ya Mto Mara. Kamati hiyo ilikuwa na wajumbe 11 chini ya uenyekiti wa Prof. Samwel Manyele wa Idara ya Uhandisi wa Kemikali na Madini kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Post a Comment

0 Comments