Maafisa wa TBS wakitoa maelezo kwa wageni waliotembelea banda la TBS kuhusu taratibu za kuingiza bidhaa nchini katika maonesho ya 23 ya ujenzi Afrika yanayofanyika Diamond Jubilee jijini Dar es salaam.
************
NA Mwandishi Wetu
Waagizaji wa bidhaa nje ya nchi wameshauriwa kuhakikisha bidhaa wanazoingiza nchini zinakidhi viwango ili kuepuka kupata hasara na kuepusha Tanzania kuwa dampo la bidhaa zisizokidhi viwango.
Ushauri huo umetolewa mwishoni mwa wiki na Mkaguzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Venance Colman wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Maonesho ya Kimataifa ya 23 Ujenzi ya Afrika yaliyoanza Machi 24 hadi 26, mwaka huu kwenye ukumbi wa Diamond Jublee jijini Dar es Salaam.
Colman alisema TBS imeshiriki maonesho hayo kwa ajili ya kutoa elimu kuhusiana na masuala ya viwango ikiwa ni pamoja na uingizaji wa bidhaa zenye viwango nchini na kwamba hiyo imekuwa fursa muhimu hasa ikizingatiwa kwamba washiriki wengi wa maonesho hayo walitoka nje ya nchi.
''Washiriki wengi wa maonesho haya wametoka nje ya nchi, hivyo elimu kubwa iliyotolewa ilikuwa ni kuhusiana na taratibu za uingizaji wa bidhaa nchini, sisi kama Shirika tumetumia fursa hiyo kutoa elimu na kuwahimiza washiriki hao kuhakikisha bidhaa zinazoingizwa nchini zimepimwa na kukidhi viwango,''alisema.
Kwenye Maonesho hayo washiriki walikuwa wanauliza sana kuhusiana na uingizaji wa bidhaa nchini, hivyo walihimizwa wahakikishe wanapima ubora wa bidhaa kabla hazijaingizwa nchini.
Alitaja faida za kupima ubora wa bidhaa kabla ya kuingizwa nchini kuwa ni pamoja na kuepuka kupata hasara pindi zikifika nchini na zikabainika hazikidhi viwango pamoja na kuepusha Tanzania kuwa dampo la bidhaa zisizokidhi viwango.
Hasara hizo ni pamoja bidhaa zao kuteketezwa iwapo zitabainika hazikidhi viwango ikiwa ni pamoja na kutozwa faini. Aidha, washiriki hao walipewa elimu kuhusiana na umuhimu wa uthibitishaji ubora wa bidhaa.
Wakizungumza kwenye maonesho hayo baadhi ya washiriki walipongeza uwepo wa TBS kwenye maonesho hayo, kwani wameweza kupata elimu kuhusiana na faida za kuingiza nchini bidhaa zilizopimwa, hatua ambayo inawahakikishia usalama wa mitaji yao.
''Kwa washiriki wa maonesho haya ambao tumepata elimu hiyo tunaahidi kuwa mabalozi wa viwango hatua ambayo italinda mitaji yetu, hivyo kuongeza mchango wetu katika ukuzaji uchumi wa nchi tunazotoka,'' alisema mmoja wa washiriki aliyejitambuisha kwa jina Yasini.
0 Comments