******************
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh Anthony Mavunde jana ametembelea Kata ya Chang’ombe,Jijini Dodoma kwa madhumuni ya kukagua ujenzi wa kituo cha Afya,Kituo cha Polisi,Eneo litakalojengwa stand ya mabasi ya kisasa pamoja na kusikiliza kero za wananchi.
Aidha Mh Mavunde ameishukuru serikali chini ya Mh Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika kata ya Chang’ombe yenye thamani zaidi ya Tsh 500m ambayo imejikita katika kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi.
Mbunge Mavunde Diwani wa Kata ya Chang’ombe Mh Bakari Fundikira na Kamati ya ujenzi kwa usimamizi mzuri wa miradi hiyo na kuwasisitiza kuhakikisha inakamilika kwa wakati ili wananchi waanze kupata huduma.
Akijibu kero za wananchi,Mbunge Mavunde amewahakikishia wananchi kwamba ahadi ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Chang’ombeni sokoni mpaka mnadani ipo palepale na kwamba wataendelea kuifuatilia kwa ajili ya utekelezaji wake kwa kuwa hatua muhimu za awali zimeshakamilika.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi,Diwani wa kata ya Chang’ombe Mh Bakari Fundikira amemshukuru Rais Samia kwa miradi mikubwa ndani ya kata na pia amemshukuru Mbunge Mavunde kwa ushirkiano mkubwa anaotoa kuwaletea wananchi maendeleo na hasa katika kusaidia upatikanaji wa eneo la ujenzi wa kituo cha Afya na mchango wake wa mifuko ya saruji 100 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Polisi.
0 Comments