******************
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Anthony Mavunde amewataka wasindikaji wa mkonge kuhakikisha wanaboresha mitambo yao ili isiathiri ubora wa nyuzi zinazozalishwa kupitia mkonge ili kumuhakikishia mkulima soko la uhakika.
Mhe. Mavunde ameyasema hayo leo tarehe 15 Machi, 2022 alipotembelea mashamba ya AMCOS za Magoma na Magunga zilizopo Wilayani Korogwe,Mkoani Tanga na kupata nafasi ya kuzungumza na wakulima ili kusikiliza changamoto zinazowakabili.
“Ni maelekezo ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoyatoa kupitia kwa Waziri Mkuu, Mhe Kassim Majaliwa Majaliwa ya kulifanya zao la mkonge kuwa la kimkakati ili kuhakikisha mkulima wa mkonge anazalisha kwa tija na kunufaika na zao lake, hivyo Wizara itaendelea kufuatilia kwa ukaribu zao hili na kuliendeleza.
Tutaipitia taarifa ya gharama za usindikaji wa mkonge kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ili tupate gharama stahiki ya usindikaji,na wakati huo huo wasindikaji lazima waboreshe mitambo yao ili mkonge mwingi wa wakulima usipotee na kutoakuathiri ubora wa zao lenyewe baada ya usindikaji.
Serikali imetenga fedha katika mwaka ujao wa fedha kuhakikisha inanunua mashine za kusindika mkonge(*KORONA*) kupitia Bodi ya Mkonge ili kuongeza wigo wa usindikaji na kupunguza mkonge unaokaukia shambani kwa kushindwa kuvunwa kwa wakati kutokana na upungufu wa mitambo”Alisema Mavunde
Naye mkulima wa mkonge aliyejitambulisha kwa jina la *Omary Juma*, alimweleza Mhe. Mavunde kuwa baadhi ya changamoto wanazokumbana nazo ni pamoja ukosefu wa maji kwenye korona hali inayopelekea kupata daraja la chini la mkonge uliochakatwa, kutokuwepo na mkataba baina ya SISALANA (Msindikaji) na AMCOS, uchakavu wa mitambo ya mwekezaji na uhaba wa korona hali inayopelekea mkonge kuvunwa mara moja badala ya mara mbili kwa mwaka.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya SISALANA, Bi.Elizabeth Kalambo alieleza kuwa Kampuni inafahamu changamoto zilizopo na tayari imeanza kuchukua hatua kadhaa ikiwemo kununua pampu za maji, na kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa visima vipya; maelezo ambayo yalionekana kutomridhisha Naibu Waziri Mavunde.
Mhe. Mavunde aliagiza kuwa anahitaji kuona pampu mpya ya maji imefungwa katika Korona ya Magoma ifikapo Alhamisi ya tarehe 17 Machi, 2022.
Vilevile, alimwomba Mhe. Basila Mwanukuzi, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe kukutana na viongozi wa AMCOS zote tano za Korogwe pamoja na Kampuni ya Sisalana kwa lengo la kujadili na hatimaye kutatua changamoto zilizopo baina yao ili wakulima wanufaike pasipo kuumizwa.
0 Comments