Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Mhe. Selemani Zedi akizungumza baada ya wajumbe wa kamati hiyo kutembelea Mradi wa Machinjio ya Kisasa Ndembezi katika Manispaa ya Shinyanga.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imetembelea Mradi wa Machinjio ya Kisasa Ndembezi katika Manispaa ya Shinyanga na kuuagiza Uongozi wa Manispaa hiyo kufanya jitihada za maksudi kuimarisha eneo la Masoko kwa kuongeza idadi ya ng’ombe na mbuzi wanaotakiwa kuchinjwa ili mradi ulete tija.
Akizungumza baada ya Wajumbe wa LAAC waliombatana pia na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange kutembelea Mradi huo leo Ijumaa Machi 18,2022, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Mhe. Selemani Zedi amesema licha ya kukamilika kwa mradi huo lakini wamebaini kuwa idadi ya ng’ombe wanaotakiwa kuchinjwa haitoshi ukilinganisha na uwezo wa machinjio hiyo.
“Tumeona mradi umekamilika na umeanza kufanya kazi lakini tulichobaini ni kwamba mradi ni mkubwa, una uwezo mkubwa lakini kwa sasa hakuna ng’ombe na mbuzi wa kutosha kufikia kiwango cha uzalishaji kilichopo.
Kamati inafahamu kwamba hii miradi ya kimkakati ambayo fedha zilitoka Benki ya Dunia ambapo halmashauri nyingi ikiwemo hii ya Manispaa ya Shinyanga ilipata na kuanzisha miradi na nyinyi Shinyanga mlianzisha Mradi wa machinjio ya kisasa lengo lake lilikuwa Halmashauri itengeneze miradi ili hiyo miradi igeuke kuwa vyanzo vya mapato”,amesema Zedi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukene mkoani Tabora.
“Sasa mradi wa Machinjio umekamilika, ushauri wetu ni kwamba zifanyike jitihada za maksudi, lazima mpate watu wa masoko wazuri wanaoweza kuisukuma vizuri, wapite huko na huko ili mpate ng’ombe na mbuzi wa kutosha wa kuchinja kwa sababu mradi huu una uwezo wa kuchinja ng’ombe 500 kwa siku lakini sasa mnachinja ng’ombe 20 kwa siku na pia wanatakiwa kuchinjwa mbuzi 1000 lakini sasa mnachinja mbuzi 38 kwa siku”,amesema Zedi.
Ameongeza kuwa lengo la miradi ya kimkakati ni kuzifanya halmashauri zijitegemee ziwe na vyanzo vya mapato hivyo kuutaka uongozi wa Manispaa ya Shinyanga kuongeza ubunifu ili mradi huo uwe na manufaa zaidi.
“Tunajua Menejimenti, Mkurugenzi wa Manispaa na timu yako, Mkuu wa wilaya na Mkuu wa Mkoa huu mradi mmeukuta kwa jinsi mlivyojieleza, kamati ina imani na utendaji kazi wenu, tunajua mna uwezo wa kuibadili hii hali ya machinjio hii ili ilete tija.Tunakupongeza Mkurugenzi kwa kushirikisha Waheshimiwa Madiwani na hata kwenye hii ziara wapo tunajua haya tuliyoyaacha waheshimiwa madiwani wataendelea nayo”,amesema Zedi.
Naye Mjumbe wa Kamati ya LAAC, Mhe. Rashid Shangazi ambaye ni Mbunge wa Mlalo mkoani Tanga ameushauri uongozi wa Manispaa ya Shinyanga kubuni miradi mingine jirani na machinjio hiyo ya kisasa ili kuongeza mapato.
“Haya mapungufu ya mradi wa machinjio siyo jambo dogo,Mkurugenzi najua umerithi haya matatizo ya mradi tumia ubunifu mpya kuendeleza mradi huu na kutengeneza miradi mingine ikiwemo viwanda vidogo katika eneo hili la machinjio. Hii njia tuliyopotea tusiendelee kupotea zaidi”,amesema Shangazi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Jomaary Mrisho Satura amesema wameyapokea maelekezo ya Kamati ya Bunge (LAAC) ikiwa ni pamoja na kuimarisha eneo la masoko na kurekebisha kasoro zilizokuwepo ili kuleta mabadiliko na mradi ulete tija.
Akisoma taarifa ya Mradi wa Ujenzi wa Machinjio ya Kisasa Ndembezi, Afisa Mifugo na Uvuvi Manispaa ya Shinyanga, Mohamed Chamzhim amesema ujenzi ulianza rasmi Mei 26,2017 na ulitarajiwa kukamilika Desemba 2018 hata hivyo ujenzi haukukamilika kwa wakati hivyo ulisogezwa mbele hadi Novemba 31,2021.
Amesema kwa sasa ujenzi wa miundo mbinu ya machinjio umekamilika kwa asilimia 100 na jumla ya fedha zilizotumika mpaka sasa ni shilingi 5,969,863,980.29.
“Tangu kuanza kwa uchinjaji hadi hadi tarehe Machi 11,2022, Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imekusanya jumla ya shilingi 93,540,000/= sawa na wastani wa shilingi 26,107,000/= kwa mwezi. Aidha gharama za uendeshaji ni shilingi 15,205,588.79 kwa mwezi ambazo zinahusisha malipo ya vibarua 31, BAKWATA, ulinzi, umeme na maji”,amesema Chamzhim.
“Mikakati ya kupunguza gharama za uendeshaji iliyopo ni pamoja na kuchimba kisima kirefu na kuweka tenki ili kuwa na maji yanayoweza kutumika katika machinjio na kuweka mfumo wa kuvuna maji ya mvua”,amesema.
ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Mhe. Selemani Zedi (katikati aliyevaa koti la bluu) akiwasili leo Ijumaa Machi 18,2022 katika Mradi wa Machinjio ya Kisasa Ndembezi Manispaa ya Shinyanga akiwa ameambatana na wajumbe wa LAAC. Kulia ni Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange, wa pili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Muonekano wa sehemu ya Mradi wa Machinjio ya Kisasa Ndembezi Manispaa ya Shinyanga
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Mhe. Selemani Zedi (wa tatu kulia aliyevaa koti la bluu) akiwa katika eneo la kupumzikia mifugo kwenye Mradi wa Machinjio ya Kisasa Ndembezi Manispaa ya Shinyanga akiwa ameambatana na wajumbe wa LAAC. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Mhe. Jomaary Satura akifuatiwa na Mjumbe wa Kamati ya LAAC Rashid Shangazi ambaye ni Mbunge wa Mlalo mkoani Tanga ,Afisa Mifugo na Uvuvi Manispaa ya Shinyanga, Mohamed Chamzhim na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko. Wa kwanza kulia ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga Mhe. Elias Ramadhan Masumbuko akifuatiwa na Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zuwena Omary.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC),Selemani Zedi (katikati aliyevaa koti la bluu) akizungumza baada ya kuwasili katika Mradi wa Machinjio ya Kisasa Ndembezi Manispaa ya Shinyanga.
Afisa Mifugo na Uvuvi Manispaa ya Shinyanga, Mohamed Chamzhim akisoma taarifa ya Mradi wa Ujenzi wa Machinjio ya Kisasa Ndembezi wakati Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ilipotembelea mradi huo.
Afisa Mifugo na Uvuvi Manispaa ya Shinyanga, Mohamed Chamzhim akionesha Mitambo ndani ya Machinjio ya Kisasa Ndembezi Manispaa ya Shinyanga kwa wajumbe Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) walipotembelea mradi huo.
Wajumbe Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) wakiangalia mitambo ndani ya Machinjio ya Kisasa Ndembezi Manispaa ya Shinyanga.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Mhe. Jasinta Mboneko akizungumza jambo wakati wajumbe Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) walipotembelea mradi wa Machinjio ya Kisasa Ndembezi Manispaa ya Shinyanga.
Afisa Mifugo na Uvuvi Manispaa ya Shinyanga, Mohamed Chamzhim akionesha chumba cha Ubaridi ndani ya Machinjio ya Kisasa Ndembezi Manispaa ya Shinyanga kwa wajumbe Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) walipotembelea mradi huo.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Mhe. Selemani Zedi akizungumza baada ya wajumbe wa kamati hiyo kutembelea Mradi wa Machinjio ya Kisasa Ndembezi katika Manispaa ya Shinyanga na kuuagiza Uongozi wa Manispaa hiyo kufanya jitihada za maksudi kuimarisha eneo la Masoko kwa kuongeza idadi ya ng’ombe na mbuzi wanaotakiwa kuchinjwa ili mradi ulete tija.
Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Mhe. Rashid Shangazi akizungumza baada ya wajumbe wa kamati hiyo kutembelea Mradi wa Machinjio ya Kisasa Ndembezi katika Manispaa ya Shinyanga.
Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
0 Comments