************************
Shirikisho la Mchezo wa Kuogelea Duniani leo Machi 15, 2022 limeridhia kutoa ufadhili wa kuboresha miundombinu mbalimbali ya mchezo wa kuogelea hapa nchini, masomo na mafunzo ya mchezo wa kuogelea kwa vijana wa kitanzania pamoja na kujenga bwawa kubwa la kuogelea lenye viwango vya kimataifa vya Olimpiki ili kuweza kuisaidia Tanzania kupiga hatua kwenye mchezo huo katika anga za kimataifa.
Kauli hiyo ameitoa Rais wa Shirikisho la Mchezo wa Kuogelea Duniani (FINA) Bw. Husain AL Musallam baada ya kufanya mazungumzo na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa mjini Zanzibar, ambapo amesema FINA itaendelea kushirikiana na Chama cha Mchezo wa Kuogelea Tanzania (TSA) ili kuendeleza vipaji vya mchezo huo.
Katika mazungumzo hayo, Rais Husain AL Musallam, amefurahishwa na amepongeza juhudi na mikakati kabambe inayofanywa na Serikali ya awamu ya sita katika kuboresha michezo, ambapo amesema amefurahishwa na mipango iliyopo ya kuendeleza miundombinu ya mchezo huo baada ya kutembelea na kuona eneo litakalojengwa miundombinu kwa ajili ya mchezo huo unaojumuisha Mpango Mkuu (Master Plan).
Mhe. Mchengerwa amemshukuru Rais Al Musallam kwa ufadhili huo na kumweleza kuwa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imekusudia kuleta mapinduzi makubwa katika michezo na kwamba tayari imeshatenga maeneo mbalimbali kwa ajili ya uwekezaji wa miundombinu ya mchezo huo ikiwa ni pamoja na mabwawa ya kuogelea yenye viwango vya Olimpiki.
Katika mazungumzo hayo, Mhe. Waziri alifuatana na Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Michezo. Yusuph Singo ambapo baada ya mazungumzo hayo amemwelekeza kuhakikisha Idara ya Michezo inasimamia kwa ukaribu na ufanisi mchakato mzima wa kuwapata vijana watakao pelekwa masomoni kupitia ufadhili huo kwa haki na kuwapata vijana wenye sifa, uwezo na kiu ya kufanya vizuri katika mchezo wa kuogelea ili kuinua kiwango cha mchezo huo hapa nchini.
“Tanzania ina vijana wenye vipaji na vipawa vya kufanya vizuri katika mchezo huu na kuliletea taifa heshima hivyo, nakuagiza uende ukasimamie kwa haki mchakato mzima wa kuwapata vijana wenye sifa bila upendeleo”. Amesisitiza Mhe, Mchengerwa
0 Comments