Ticker

6/recent/ticker-posts

KAMATI YAIPONGEZA WIZARA KWA KUSAIDIA KUWAREJESHA WANAFUNZI WALIOKUWA NCHINI UKRAINE

Na Waandishi Wetu, Dar


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) imeipongeza Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa juhudi ilizozichukua hadi kufanikisha zoezi la kuwarejesha salama wanafunzi waliokuwa nchini Ukraine.


Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Vita Kawawa (Mb) Jijini Dar es Salaam wakati Kamati hiyo ilipotembelea Chuo cha Diplomasia (CFR).


Katika Kikao hicho ambacho pia kilihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula pamoja na Naibu Katibu Mkuu Mhe. Balozi Fatma Rajab.
“Nichukue nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa Wizara kwa jinsi mlivyoshughulikia suala zima la kuhakikisha wanafunzi wa Kitanzania walioko nchini Ukraine wanarejea salama nchini,” amesema Mhe. Kawawa.


‘’Mhe. Waziri tunawapa pongezi nyingi, kwa kazi na hatua kubwa mlizochukua na jinsi mlivyoshirikiana na wazazi wenye wanafunzi waliokuwa wanasom nchini Ukraine hasa ikizingatiwa kuwa wazazi hao waliwapeleka watoto wao binafsi bila ya kuishirikisha Serikali,’’ ameongeza Mhe. Kawawa.


Amesema kamati imeridhishwa na jinsi ambavyo Wizara ilivyosimama imara na kuwasaidia Watanzania wote waliokuwepo nchini Ukraine na kuhakikisha wanarejea nyumbani salama.


Mhe. Kawawa ametoa wito kwa Watanzania wanapokuwa nje ya nchi kujiandikisha katika Balozi za Tanzania ili kuwa rahisi kuwaratibu pale inapotokea athari yoyote kule wanapokuwepo.


Mhe. Kawawa amewapongeza vongozi wa wizara, mabalozi na watumishi wa wizara ambao kwa namna moja au nyingine wamefanikisha uondoaji wa watanzania waliokuwepo nchini Ukraine.
Akizungumza katika kikao hicho Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula ameihakikishia kamati hiyo kwamba Uongozi wake utaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhakikisha inasimamiwa ili ikamilike kwa wakati na kuendana na thamani halisi ya fedha iliyotolewa na Serikali.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula akimkaribisha Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Mhe. Vita Kawawa katika Chuo cha Diplomasia (CFR) Jijini Dar es Salaam


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula wakikagua mradi wa ujenzi wa vyumba vya mihadhara ya Chuo cha Diplomasia (CFR) Jijini Dar es Salaam


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Mhe. Vita Kawawa akizungumza wakati kamati hiyo ilipotembelea Chuo Cha Diplomasia Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula.


Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Mhe. Alexander Mnyeti akizungumza wakati kamati hiyo ilipotembelea Chuo Cha Diplomasia Jijini Dar es Salaam


Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) Mhe. Stella Ikupa akizungumza wakati kamati hiyo ilipotembelea Chuo Cha Diplomasia Jijini Dar es Salaam


Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) katika picha ya pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula, Naibu Katibu Mkuu Balozi Fatma Rajab pamoja na viongozi wa Chuo Cha Diplomasia Jijini Dar es Salaam

Post a Comment

0 Comments