Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof.Adolf Mkenda,akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 16,2022 kuhusu maadhimisho ya Wiki ya Ubunifu na Mashindano ya Kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu maarufu kama (MAKISATU) kwa mwaka 2022 ambapo kilele cha Mashindano hayo kufanyika Mei 15 hadi 20,2022 jijini Dodoma.
......................................................
Na Zena Mohamed, Dodoma.
WIZARA ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imesema Wizara hiyo imetenga kiasi cha shilingi bilioni moja za kitanzania kwa kwa ajili ya kuendeleza wabunifu watakao tambuliwa katika mashindano ya kitaifa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu( MAKISATU) mwaka huu.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo na Waziri wa Wizara hiyo,Prof.Adolf Mkenda wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya MAKISATU kwa mwaka 2022 ambapo amesema maadhimisho ya wiki ya ubunifu na MAKISATU zinalenga pamoja na mambo mengine kuibua,kutambua na kuendeleza jitihada zinanzofanywa na wabunifu wa kitanzania na kuhamasisha matumizi ya sayansi ,teknolojia na ubunifu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Amesema wiki ya ubunifu ni sehemu ya mikakati ya serikali ya awamu ya sita ya kuongeza hamasa ya matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu kama nyenzo za kutatua changamoto za kiuchumi na kijamii.
"Wiki ya ubunifu inaandaliwa kwa kushirikiana na program ya FUNGUO ya UNDP na itafanyika katika mikoa 17 nchini". Amesema.
Ametaja mikoa hiyo kuwa ni Dar es saalam, Dodoma, Mbeya, Arusha, Iringa, Mwanza, Zanzibar, Tanga, Kilimanjaro, Morogoro, Njombe, Kagera, Mtwara, Kigoma, Mara na Ruvuma.
Ambapo amesema wiki hiyo ya kitaifa ya ubunifu kwa mwaka 2022 itaadhimishwa kuanzia Mei 15 hadi Mei 20 mwaka huu katika jiji la Dodoma itakayoenda sambamba na kilele cha MAKISATU.
"Usajili wa ubunifu kwa ajili ya Mashindano ulifikia mwisho tarehe 10, Februari, 2022, Lakini kutoka na uhitaji, Leo nichukue fursa hii kutangaza rasmi, kuongeza muda wa usajili wa Wabunifu hadi Februari 28 mwaka huu na hadi kufikia jana tarehe 15 Februari, tumesajili wabunifu zaidi ya 480 kwa ajili ya Mashindano,"Amesema Waziri Mkenda.
Pia ameeleza kuwa mashindano ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, washiriki watatoka katika makundi saba ambayo ni Shule za Msingi Shule za Sekondari Vyuo vya Ufundi Stadi Vyuo vya Ufundi Vyuo Vikuu Taasisi za Utafiti na Maendeleo na Mfumo usio Rasmi huku akisema usajili wa washiriki wa MAKISATU mwaka huu ulianza rasmi tangu Desemba 27 mwaka 2021 na usajili huo unaratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikishirikiana na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) inayosajili wabunifu wa makundi ya Vyuo Vikuu na Taasisi za Utafiti na Maendeleo.
Huku Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) inasajili wabunifu wa makundi ya Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi Stadi na wale wa Mfumo usio rasmi Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi linalosajili wabunifu wa kundi la Vyuo vya Ufundi na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) kwa kushirikiana na Wizara inayosajili wabunifu wa makundi ya Shule za Msingi na Shule za Sekondari.
"Katika kilele hicho kutakuwa na maonesho ya teknolojia na bunifu mbalimbali, bidhaa na huduma zinazotolewa na taasisi zitakazoshiriki zikiwemo taasisi za kitafiti na maendeleo, Vyuo Vikuu, kumbi za ubunifu, taasisi za kibiashara, wakala za Serikali, Wizara na Taasisi binafsi na pia katika kilele hicho kutakuwa na utoaji tuzo kwa wabunifu 21 walioshinda MAKISATU,"amesema.
Ameeleza kuwa kupitia MAKISATU 2019, 2020 na 2021, Wizara imefanikiwa kuibua na kutambua wabunifu wachanga 1,785.
Kupitia wabunifu hao bunifu 466 zilikidhi vigezo, zimetambuliwa na kuhakikiwa na kati ya hizo bunifu mahiri 200 tayari zinaendelezwa na Serikali ili kufikia hatua ya kubiasharishwa.
“Aidha napenda kutoa taarifa kuwa kati ya bunifu zinazoendelezwa na Serikali, 26 zimeshafikia hatua ya kubiasharishwa, wakati 95 ziko katika hatua ya Sampuli kifani (prototype) na nyingine katika hatua za awali za kuandaa sampuli kifani” amesema.
0 Comments