NA MWANDISHI WETU, MOROGORO
MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma amesema Taasisi za Mahakama na ile ya Vizazi na Vifo (RITA) zina umuhimu mkubwa katika mchakato wa malipo ya fidia kwa wategemezi wa mfanyakazi anayefariki kutokana na ajali au ugonjwa unaotokana na kazi.
Dkt. Mduma ameyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati wa semina za kuwajengea uwezo Watendaji wa Mahakama na wale wa RITA kuhusu majukumu ya Mfuko wa Fidida kwa Wafanyakazi (WCF) hususan mchakato wa malipo ya fidia.
“Mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuzitaka Taasisi zake kuongeza ufanisi na ubora wa huduma kwa wananchi.” Alisema Dkt. Mduma.
Kwa upande wa Mahakama, Dkt. Mduma alisema “mafunzo haya ni muhimu sana kutokana na nafasi ya Mahakama katika kufanikisha upatikanaji wa nyaraka mbalimbali za mirathi ambazo ndizo hutumiwa na Mfuko katika mchakato wa malipo ya fidia kwa wategemezi wa mfanyakazi anayefariki kutokana na ajali au ugonjwa unaotokana na kazi " alifafanua Dkt. Mduma.
Halikadhalika kwa upande wa RITA nayo inahusika katika kufanikisha upatikanaji wa nyaraka mbalimbali za vizazi na vifo ambazo hutumiwa na WCF katika kuanzisha mchakato wa malipo ya fidia kwa wategemezi wa mfanyakazi anayefariki kutokana na ajali au ugonjwa unaotokana na kazi.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki kutoka Mahakama, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Temeke, Mhe. Jaji Ilvin Mugeta ameipongeza WCF kwa kuwaandalia mafunzo hayo kwani Mahakama inafanya kazi zake kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali WCF ikiwemo.
“Hivyo tunafarijika tunapopata fursa ya kuongeza uelewa wa mambo mbalimbali vilevile ni matarajio yangu kuwa mafunzo haya yataleta manufaa makubwa ikiwemo kuimarisha mahusiano kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi na kuchangia kukuza uchumi wa nchi yetu". Alisisitiza Jaji Mugeta.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Usajili wa Vizazi na Vifo (RITA) Bi. Victoria Mushi, alisema mafunzo hayo yamekuwa bora kwao kwani watakapotoka hapo watawaelimisha wengine umuhimu wa kutumia majina sahihi kwenye nyaraka zao za vizazi na vifo
“ Hii itasaidia wananchi watakapokua wanachukua vyeti vyao viwe vina taarifa sahihi ili kuwarahisishia wenzetu wa WCF kutokua na mashaka wakati wanapochakata taarifa katika huduma wanazotoa," alisema Bi. Mushi.
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma.
Mhe. Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Temeke, Ilvin Mugeta
Mkurugenzi wa Uendeshaji WCF, Bw. Anselim Peter, akitoa mada.
Baadhi ya Wasajili kutoka RITA, wakiwa kwenye mafunzo.
Watoa mada kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Tathmini, Dkt. Abdulsalaam Omar, Mkurugenzi wa Uendeshaji, Bw. Anselim Peter na Mkuu wa Kitengo cha Sheria, Bw. Abraham Siyovelwa wakati wa mafunzo hayo.
0 Comments