Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKUU ATAKA WAKANDARASI WAZAWA KUTEKELEZA MIRADI KWA WELEDI NA UFANISI


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati akifungua mkutano wa kazi kati ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),TARURA na Makandarasi uliofanyika leo Februari 12,2022 jijini Dodoma.


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mita(TAMISEMI),Innocent Bashungwa,wakati wa mkutano wa kazi kati ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),TARURA na Makandarasi uliofanyika leo Februari 12,2022 jijini Dodoma.


Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi ,David Silinde,akizungumza wakati wa mkutano wa kazi kati ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),TARURA na Makandarasi uliofanyika leo Februari 12,2022 jijini Dodoma.


Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) , Mhandisi Victor Seff ,akizungumza wakati wa mkutano wa kazi kati ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),TARURA na Makandarasi uliofanyika leo Februari 12,2022 jijini Dodoma.


Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya,akizungumza wakati wa mkutano wa kazi kati ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),TARURA na Makandarasi uliofanyika leo Februari 12,2022 jijini Dodoma.


Sehemu ya washiriki wakifatilia hotuba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (hayupo pichani) wakati akifungua mkutano wa kazi kati ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),TARURA na Makandarasi uliofanyika leo Februari 12,2022 jijini Dodoma.

.........................................................

Na.Alex Sonna,DODOMA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa,amewataka wakandarasi wazawa kubadilika katika utendaji wao wa kazi ili miradi mbalimbali wanayopewa na serikali waitekeleze kwa weledi na ufanisi.

Hayo ameyasema leo Februari 12,2022 jijini Dodoma wakati akifungua mkutano wa kazi kati ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),TARURA na Makandarasi.

Majaliwa amesema kuwa makandarasi wa ndani wanatakiwa kujiimarisha ili kuwa na uwezo wa kutekeleza miradi mikubwa ambayo wanapewa na serikali.

“Kama msipobadilika hata miradi hii ya TARURA yatachukua makampuni ya nje na nyie kubaki mnalalamika lazima mjiimarishe katika ununuzi wa mitambo ya kisasa,teknolojia na mitaji.

“Makandarasi wa ndani lazima mjipange leo hii Rais anaongeza fedha lakini nyie mpo wakati mchina mmoja unakuta anasimaia watanzania 20 kwanini sisi tushindwe ndio maana tulisema katika miradi mikubwa lazima wazawa wawepo ili kujifunza bodi ya makandarasi lichukueni hili mliweke kwenye vikao vyenu”ameongeza

Aidha Majaliwa amewaagiza wahandisi wa TARURA wasimamie miradi kwa weledi, uadilifu na uaminifu huku wakizingatia mikataba husika na pia wawe wabunifu kutumia teknolojia mpya, sahihi na rafiki kulingana na upatikanaji wa malighafi za ujenzi.

Amesema Serikali imefanya jitihada mbalimbali katika kuijengea uwezo TARURA ili iweze kutekeleza makujumu yake ikiwa ni pamoja kuiongezea fedha kutoka sh. bilioni 247.5 ilipoanzishwa mwaka 2017 hadi kufikia Sh. bilioni 752.61 sawa na ongezeko la asilimia 204.3.

“Fedha hizo zinajumuisha sh. bilioni 127.50 kutoka Serikali Kuu, sh. bilioni 272.50 kutoka Mfuko wa Barabara, sh. bilioni 322.15 kutoka katika tozo ya sh. 100 kwa lita ya mafuta ya petroli na dizeli na sh. bilioni 30.44 kutoka kwenye ushuru wa maegesho wa magari.”

Amesema mwaka 2017, TARURA ilikuwa inasimamia mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 108,946.19 na sasa mtandao huo umeongezeka na kufikia kilomita 144,429.77 ambazo zimetangazwa rasmi kwenye Gazeti la Serikali Na. 463 la tarehe 25 Juni 2021.

Amewaagiza watumishi wa TARURA wasijiingize kwenye kazi zenye mgongano wa maslahi. “Waswahili husema mshika mawili moja humponyoka. Kwa mantiki hiyo, ikiwa unataka kufanya biashara na Serikali wakati wewe ni mtumishi ni vyema ukaacha kazi ili ufanye biashara yako kwa ufanisi”.

Amewaagiza viongozi wa TARURA wahakikishe wanapoandaa taarifa za miradi wawashirikishe watendaji wa Halmashauri, Wilaya na Mikoa na pia taarifa za utekelezaji zitolewe katika kwa Baraza la Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) na Kamati ya Ushauri ya Mkoa RCC);

Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff awasilishe kwa Bodi ya Usajili wa Wakandarasi orodha ya wakandarasi wababaishaji na awasilishe nakala kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –TAMISEMI ili iwasilishwe kwa Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi kwa hatua zaidi za kinidhamu.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Innocent Bashungwa amesema Serikali ina matumaini makubwa kupitia watendaji hao na kwamba changamoto zote zinazowakabili hazina budi kufanyiwa kazi kwa wakati ili waweze kutoa huduma bora kwa Watanzania.

Amesema wahakikishe kila mmoja anatekeleza majukumu yake ipasavyo ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa weledi na kwa viwango vinavyotakiwa ili barabara wazazosimamia zinapitika kwa wakati wote. “Hayo ndio maono ya Mheshimiwa Rais Samia.”

Bashungwa ameagiza asilimia 60 ya kazi za TARURA zitangazwe mapema, bila kusubiri mpaka mwaka wa fedha uanze ili pale mwaka wa fedha unapoanza iwe ni wakandarasi kuanza kazi.

Awali, Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Seff asema miongoni mwa changamoto zinazowakabili ni pamoja na baadhi ya makandarasi kuomba kazi nyingi na wakati mwingine kupata kazi nyingi kuliko uwezo wao, hivyo hulazimika kusubiri hadi kazi iishe eneo fulani ndipo wapeleke vifaa na kuanza kazi eneo jingine.

Post a Comment

0 Comments