*********************
Na. John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa ameliagiza Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) kuratibu Siku ya Kiswahili Duniani kwa kushiriana na Wizara ya Mambo ya Nje na wadau mbalimbali ikiwa ni mkakati wa makusudi wa kuibidhaisha lugha hiyo duniani.
Kauli hiyo ameitoa leo Februari 9, 2022 jijini Dar es Salaam kwenye Ofisi za BAKITA alipotembelea, kukagua shughuli za BAKITA kwa mara ya kwanza baada ya kuteuliwa kuwa Waziri mwenye dhamana Utamaduni, Sanaa na michezo ambapo pia ameambatana na Katibu Mkuu wa Wizara yake Dkt. Hassan Abbasi.
Amesema kwa vile siku hii imetambuliwa duniani na imeshatangaza kuwa lugha ya kazi kwenye Umoja wa Afrika ni lazima kuipa umuhimu wa kipekee na kuiandaa kwa kuitangaza kwa nguvu zote ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kimkakati ambapo ametaka kila ubalozi wa Tanzania duniani kuadhimisha siku hii kikamilifu.
Akifafanua amesema maandalizi hayo yanatakiwa kuhusisha wadau wote ambao kwa namna moja au nyingine wanamchango katika kukuza na kubidhaisha lugha ya Kiswahili na amesisitiza kuanza mapema ili kutoa nafasi ya watu wengi kupata ujumbe ambao unatakiwa kutolewa kwa njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na vyommbo vya habari.
“Ninataka mtoke mwende mkabidhaishe kiswahili, pia andaeni kanzidata inayoainisha wataalam tulionao, kiwango chao cha elimu ili tuone wakihitajika tunawapata wapi” amesisitiza Mchengerwa.
Amepongeza juhudi zilizofanywa na Muasisi wa taifa la Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere za kuingiza lugha ya Kiswahili kutumika kama lugha ya taifa kupitia Chama cha Siasa cha TANU mwaka 1954 na Rais wa awamu ya Tano hayati John Pombe Magufuli kwa kukipigania Kiswahili ili kiwe lugha ya kimataifa na sasa Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa msitari wa mbele kukibidhaisha Kiswahili duniani.
Pia amesema BAKITA linahitaji kuboresha miundombinu ya mitandano kwa ajili ya kazi mbalimbali za kukuza, kueneza na kuhifadhi Kiswahili.
Akiwa ofisini hapo alipata fursa ya kutembelea darasa lenye mitambo ya kisasa zaidi barani Afrika kwa ajili ya kufundishia ukalimani.
Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji wa Baraza hilo Consolata Mushi amemhakikishia Mhe. Waziri kuendelea kubidhaisha Kiswahili ambapo amesema katika siku za hivi karibuni wamekisajili kituo cha kufundisha Kiswahili nchini Ethiopia.
0 Comments