Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI JAFO AAGIZA TATHIMINI ZA ATHARI KWA MAZINGIRA KUZINGATIA SHERIANA TAKWIMU ZA TMA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo akizungumza wakati akifungua rasmi warsha ya wadau wa mazingira kuhusu umuhimu wa huduma za hali ya hewa, iliyofanyika katika Ukumbi wa Maktaba, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tarehe 18/02/2022.


Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Dkt.Agnes Kijazi akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa warsha ya wadau wa mazingira kuhusu umuhimu wa huduma za hali ya hewa, iliyofanyika katika Ukumbi wa Maktaba, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tarehe 18/02/2022.

**************

Dar es Salaam; Tarehe 18 Februari, 2022;

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo amewaagiza wadau wa mazingira kuzingatia takwimu za hali ya hewa katika kuandaa tathmini za athari kwa mazingira nchini ili kutekeleza matakwa ya sheria Na.2 ya mwaka 2019 ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.

Mhe. Jafo alitoa maelekezo hayo wakati akifungua rasmi warsha ya wadau wa mazingira kuhusu umuhimu wa huduma za hali ya hewa, iliyofanyika katika Ukumbi wa Maktaba, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tarehe 18/02/2022.

“Nikiwa waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) nitahakikisha kabla ya kutoa vyeti tathmini za athari kwa mazingira (EIA), jambo kubwa nitakaloliangalia ni chanzo cha takwimu zilizoambatishwa, hivyo hakuna namna ya kukwepa, tutumie takwimu sahihi za hali ya hewa kwa mustakhabali wa nchi yetu”. Alisema Mhe.Jafo.

“Kila mradi unaotaka kuwekezwa unatakiwa kufanyiwa tathimini za athari za mazingira (EIA), na mchakato wa EIA ni lazima unahitaji takwimu za hali ya hewa, na ikitokea umekosea takwimu utaleta shida”. Alieleza Mhe. Jafo.

Aidha, Mhe. Jafo alieleza kuwa sheria Na.2 ya mwaka 2019 ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inaipa Mamlaka ya Hali ya Hewa jukumu la kutoa takwimu za hali ya hewa na kuzitaka wizara,taasisi na wataalam elekezi wa mazingira (consultants) kuzingatia umuhimu wa matumizi ya takwimu za hali ya hewa na endapo takwimu hizo zitakosekana inatakiwa kupata ushauri wa kitaalamu kutoka TMA na kutokufanya hivyo ni kuvunja sheria za nchi.

Awali, Mhe Jafo alisema warsha hiyo imetokana na mchakato wa kisheria ambapo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania mwaka 2019 na kanuni zake kusainiwa mwaka 2021, hivyo kupelekea taasisi tatu ambazo ni Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Chama cha Wataalam wa Mazingira Tanzania (TEEA) kuona umuhimu wa kubadilishana mawazo ya namna ya kutekeleza sheria hiyo. Vilevile, Mhe Jafo aliwataka TMA kuandaa semina kwa maafisa mazingira waliopo katika halmashauri na mikoa yote nchini ili wafahamu vyema masuala muhimu ya hali ya hewa kama ilivyoainishwa katika sheria. Pia aliwataka (TMA) na kutoa mada kwenye vikao vya wakurugenzi wa jiji na halmashauri, ili kuwajengea uelewa wa sheria hiyo Na. 2 ya mwaka 2019.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi alieleza kuwa warsha hii ni fursa muhimu ya kuboresha huduma katika sekta ya mazingira kwa kuzingatia matumizi sahihi ya huduma za hali ya hewa zinazotolewa na TMA na matakwa ya kisheria pamoja na kuimarisha uelewa kuhusiana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi.Aidha,Dkt. Kijazi aliwajulisha washiriki wa warsha hiyo kwamba huduma za hali ya hewa zinazotolewa nchini zimeongezeka viwango vya usahihi hivyo zinafaa kutumika katika sekta zote za maendeleo.

Aidha, mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Bi Lilian Lukambuzi alisema NEMC na TMA wameingia makubaliano yenye lengo la kufanya tafiti za pamoja kuhusu masuala ya ya hali ya hewa na mazingira na kufuatilia miradi ya kimkakati ili kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu.

Naye, mwakilishi wa TEEA Bi. Rukia Ismail alifafanua kuwa warsha hiyo itawasaidia katika kuimarisha ufanisi wa kuandaa thathmini za athari kwa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wadau wa mazingira katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa takwimu za muda mrefu za hali ya hewa.

Warsha ya wadau wa mazingira kuhusu umuhimu wa huduma za hali ya hewa imeandaliwa kwa ushirikiano wa TMA, NEMC na TEEA ikiwa na lengo la kujenga uelewa kuhusu taarifa za hali ya hewa na umuhimu wa kuzingatia mipango ya utekelezaji wa mipango hiyo.

Imetolewa na;

KITENGO CHA UHUSIANO, MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA (TMA).

Post a Comment

0 Comments