Ticker

6/recent/ticker-posts

WATOTO NA VIJANA BALEHE WATIMIZA HAKI YAO YA KUTOA MAONI YA UBORESHAJI WA MITAALA


***************

Wizara ya Maendeleo ya Jamii ,Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kupitia UNICEF-TANZANIA wameandaa mkutano maaalum wa siku mbili wa watoto kwa ajili ya kutoa maoni ya uboreshwaji wa Mitaala nchini.

Mkutano huo unafanyika kuanzia tarehe 02 hadi 03/02/2022 Mjini Morogoro Katika Hotel ya Adema, ukiwa umewashirikisha wawakilishi wa wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari kutoka Mikoa 26 ya Tanzania Bara, wawakilishi kutoka vyuo vya ufundi na vyuo vya maendeleo ya Jamii, Wanafunzi kutoka vyuo Vikuu, Walimu na Wazazi.

Katika ufunguzi wa Mkutano huo Mkurugenzi wa Maendeleo ya Watoto Wizara ya Maendeleo ya jamii jinsia wanawake na makundi maalum Bwana. Sebastian Kitiku amesema, lengo la mkutano huo ni kuhakikisha watoto wanapata haki ya kutoa maoni yao ya uboreshwaji wa Mitaala nchini.

 "Kushirikisha watoto katika masuala yanayowahusu ni kulinda haki,ulinzi na ustawi wao.Mapitio ya Mtaala yanawahusu kwa sababu wao ndio watumiaji wa Mitaala hiyo,amesema."

Amesema, Baraza la watoto tayari limependekeza maeneo ya vipaumbele katika kuboresha Mitaala hiyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha Elimu inayotolewa nchini inaendana na maendeleo ya sasa.

Amesisitiza kuwa Serikali inatambua na kuheshimu nafasi ya watoto na vijana katika kuchangia maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu TET Dkt.Aneth Komba amesema, mapitio ya Mitaala ni zoezi la kawaida ambalo hufanyika kila baada ya mzunguko mmoja wa mtaala.

Amesema kwa sasa Serikali kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania inafanya mapitio ya sita ya Mitaala toka Tanzania kupata Uhuru.

Dkt.Komba ameeleza kuwa kufanya mapitio haya ya Mitaala haimaanishi kuwa Mitaala tunayotumia kwa sasa haifai, ila imepitwa na wakati kulingana na maendeleo ya sasa.

 "Mitaala iliyopo sio bure kabisa ila imepitwa na wakati kulingana na ukuaji wa maendeleo nchini, mambo yalisosomwa miaka 20 nyuma si lazima kwa mtoto wa sasahivi kuyasoma" amesema"

Aidha amewahakikishia watoto hao maoni watakayotoa yatafanyiwa kazi na baada ya kukusanywa yataenda kuchakatwa na kupata picha halisi ya Mtaala utakavyokua.Na baada ya hapo watoto watapata fursa tena ya kupitishwa kabla ya kuandaa mtaala wenyewe.

Kwa upande wa watoto hao pia walipata fursa ya kutoa maoni yao na baadhi yao wakitaka Mtaala wa Elimu Nchini kuzingatia suala la Elimu ya TEHAMA kuanza kufundishwa toka Elimu ya Msingi, Lugha ya Kiswahili itumike katika ufundishaji na ujifunzaji, Elimu ya Fedha pia izingatiwe ili kuweza kuwajengea watoto uwezo mzuri wa kutumia na kutunza fedha.

Post a Comment

0 Comments