Mratibu wa mafunzo endelevu kwa wataalam (CPD) Dkt. Mashauri Lisso akiwasilisha mada wakati wa Mafunzo kwa watoa huduma hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila.
Watoa huduma wa afya hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila wakisikiliza mada zilizowasilishwa kwenye mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Baraza la Madakatari Tanganyika
*************************
Na.WAF, Dar es Salaam
MRATIBU wa Mafunzo Endelevu kwa Wataalam (CPD) kutoka Baraza la Madaktari Tanganyika Dkt.Mashauri Lisso,amewataka watoa huduma za afya kushiriki katika mafunzo(CPD activities) ambayo yanakuza uelewa, ujuzi ,mitazamo na maarifa ili kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma bora na afya zao zinaimarika.
Akizungumza Jijini Dar es Salaam katika Hosptali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila Dkt. Lisso, amesema CPD ni takwa la kisheria kwa wanataaluma wote wa afya na mafunzo hayo yanawahusu watoa huduma wote waliosajiliwa.
"Baraza linawataka watoa huduma wote kujihusisha katika mafunzo hayo ili kukuza uelewa wao, ujuzi na maarifa na kuhakikisha huduma anayopata mteja na mgonjwa inakuwa ni bora na inafanya afya zao kuimarika"amesema Dkt. Lisso
Dk. Lisso, ameongeza kuwa mafunzo hayo hujumuisha shughuli anazofanya mtoa huduma pindi akiwa katika eneo lake la kazi.
Aidha, Dk. Lisso, amesema iwapo mwanataaluma akiwa katika majukumu yake ya kazi akashiriki mafunzo ambayo Baraza haliyatambui ana haki ya kutoa taarifa kwa kudai pointi za CPD kupitia akaunti yake ya MCT ili kupata alama kutokana na alichofanya.
Naye, Naibu Mkurugenzi wa Hosptali ya Taifa Muhimbili -Mloganzila Dkt.Julieth Mgandi, amewashukuru MCT kwa kwenda Hospitalini hapo na kuzungumza na watoa huduma.
Dk. Julieth ametoa wito kwa watumishi wa afya kuwa na utayari wa kujifunza na kupenda kusoma kila siku kwani kufanya hivyo kutasaidia kuboresha huduma za afya nchini na wananchi kupata huduma bora.
Pia Dkt. Julieth amesema kupitia mafunzo hayo wamepata uelewa na umuhimu wa kuwa na mafunzo endelevu.
Kwa upande wake Daktari Bingwa kutoka Hosptali ya Taifa Muhimbili na Mjumbe wa kamati ya CPD Prof. Francis Furia amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo watoa huduma za afya na kuwasaidia kujifunza mabadiliko yanayotokea katika fani hiyo.
Aidha Prof. Furia ameongeza kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa watoa huduma za afya kwaajili ya kufanya tafiti na pindi yanapotokea mabadiliko ikiwemo suala la ugonjwa wa Uviko 19.
"Kwa kuzingatia haya mabadiliko yanayotokea katika sekta ya afya ni muhimu kuwajengea uwezo wa kuboresha utendaji kazi wao"amesema Prof. Furia.
Prof. Furia ameongeza kuwa mafunzo hayo yanaweza kutolewa kwa njia mbalimbali ikiwemo kupitia taasisi zilizosajiliwa na Baraza au mwanataaluma mwenyewe kufanya peke yake.
"Kupitia sheria ya utoaji huduma za afya Baraza limeweka ulazima wa mafunzo hayo kwa wanataaluma wote lengo sio kuwakomoa ni kuhakikisha watoa huduma wanaotoa huduma kwa wahitaji kwa weredi na kufuatana na mabadiliko ya kimatibabu yanayotokea mara kwa mara"ameeleza Prof. Furia.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya CPD Remla Shirima, ametoa rai kwa Hosptali za Wilaya na Mikoa kupeleka taarifa zao ili kusajiliwa ndani ya Baraza.
Naye Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Homoni na Kisukari kutoka Muhimbili,Dk.Faraja Chiwanga,amesema mafunzo hayo waliyoyapata yamesaidia kujibu maswali mbalimbali waliyokuwa nayo kuhusiana na CPD.
Pia Dk. Faraja Chiwanga ameongeza kuwa ni muhimu kupata mafunzo hayo ili kutoa huduma bora na salama kwa wagonjwa.
0 Comments