Ticker

6/recent/ticker-posts

SAKATA LA UMEME LILIVYOTIKISA BUNGE WABUNGE WANG'AKA

Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina akizungumza bungeni Jijini Dodoma.



BUNGE limehitimisha rasmi Mkutano wake wa 6 Kikao cha 14 mjini Dodoma huku sakata la kukatika kwa umeme pamoja na kusuasua kwa ujenzi wa Mradi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Julius Nyerere kuteka mkutano huo.

Baadhi ya wabunge Wakichangia taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu za Kamati za Bunge za Bajeti, Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) bungeni jijini Dodoma walielezea kutoridhishwa kwako na tatizo la umeme linavyowatesa wananchi na kusuasua kwa mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere.

Wabunge hao ni pamoja na Mbunge wa Jimbo Mkinga Mkoa wa Tanga, Mhe. Dunstan Luka Kitandula , Mbunge wa Jimbo Nyasa , Mkoa wa Ruvuma, Mhe. Injinia Stella Martin Manyanya, Mbunge wa Jimbo la Geita Vijijini Mkoa wa Geita, Mhe. Joseph Kasheku Msukuma, Mbunge wa Jimbo la Igalula Mkoa wa Tabora, Mhe. Venant Daud Protas, Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Singida, Mhe. Jesca David Kishoa.

Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Mhe. Luhaga Joelson Mpina amewaonya baadhi ya Mawaziri kuacha kumuhusisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika udhaifu wao wa kiutendaji huku akiwataka kuwajibika kikamilifu katika wizara zao.

Pia Mpina amemuomba Spika wa Bunge kuunda Kamati Teule ya Bunge ili pamoja na mambo mengine ichunguze kwa kina chanzo na sababu za kukatikakatika na mgao wa umeme unaondelea, kuchunguza kwa kina uwezo wa Bodi na Menejimenti ya TANESCO katika kuliongoza shirika na kupendekeza hatua za kuchukua.

Amesema pia Kamati hiyo teule ya Bunge pamoja na mambo mengine ichunguze kwa kina sababu na chanzo cha kusuasua kwa ujenzi wa mradi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Julius Nyerere na kupendekeza hatua za kuchukua ili kunusuru mradi huu mkubwa.

Mpina amesema Katakata ya umeme inayoendelea nchini hivi sasa imeleta madhara makubwa ikiwemo kupotea kwa ajira za watanzania, kushuka kwa uzalishaji viwandani, mfumko mkubwa wa bei, kutegemea bidhaa kutoka nje ya nchi, mapato ya Serikali kushuka na uchumi kuyumba, lakini pia inarudisha nyuma jitihada nzuri na kubwa anazofanya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kuvutia wawekezaji kuja nchini.

Ameongeza kuwa sababu zinazotolewa za kukatikakatika kwa umeme zinazua maswali mengi ambapo Taarifa ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini na majibu ya Waziri wa Nishati yaliyotolewa bungeni kwa nyakati tofauti yanaleta mkanganyiko mkubwa na yanakinzana na kuleta hofu kubwa kwa watanzania wanaotegemea nishati ya umeme kuendesha maisha yao.

Mpina amesema ni siku chache pia alihoji bungeni sababu za katakata na mgao wa umeme unaoendelea nchini ambapo Waziri wa Nishati alieleza kuwa inatokana na matengenezo makubwa ya mitambo ya kufua umeme na miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme.

Amesema pia kwa nyakati tofauti Waziri wa Nishati alieleza kuwa watu waliwahi kutishiwa kufukuzwa kwa kukata umeme kwa ajili ya kufanya Scheduled repairs wakaacha scheduled repairs kwa miaka mitano kwa kuogopa kufukuzwa.

“Wakati huo huo tena Serikali ilisema sababu za katakata ya umeme zinasababishwa na kupungua kwa maji katika mabwawa ya kufua umeme kulikosababishwa na ukame” alihoji Mpina

Aidha Mpina amesema pia TANESCO mara kadhaa ilikanusha kuwepo kwa mgao wa umeme wakati maeneo mbalimbali nchini yakiwa hayana nishati ya uhakika ya umeme na shughuli na biashara nyingi zinasuasua.

Alisema TANESCO ikaja tena na kutangaza mgao wa siku 10 wa kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa 6 usiku na baadae tena yakatolewa maelezo kuwa mgao hautakuwa na makali kama ulivyotangazwa kwa kuwa shirika limefanya tathmini ya uhitaji.

Mpina amesema suala la matengenezo ya mitambo na miundombinu linaelezwa kiujumla jumla sana, haielezwi ni mitambo gani na miundombinu gani ambayo haikufanyiwa matengenezo kwa miaka sita iliyopita na ikaweza kuendelea kufanya kazi bila umeme kukatika katika kipindi chote hicho.

“Je kitalaamu inawezekanaje mitambo na miundombinu ya umeme isiyofanyiwa matengenezo kwa ratiba iliyowekwa (scheduled Maintenance) na umeme ukaendelea kuwaka kama kawaida?” amehoji Mpina.

Mpina amesema mapato ya TANESCO yamezidi kuongezeka kutoka Tsh. Bilioni 72 kwa mwezi mwaka 2015 hadi kufikia Tsh. Bilioni 160 kwa mwezi mwaka 2020 sawa na ongezeko la asilimia 102, pia katika kipindi cha mwaka 2019/2020 TANESCO ilipata faida ya Tsh Bilioni 45.25. TANESCO imeacha kutegemea ruzuku kutoka serikalini ya kiasi cha Tsh. Bilioni 143 huku mapato yakifikia Tsh. Trilioni 2.4 mwaka 2021.

Aidha amesema pia mitambo ya kukodi ya kufua umeme kwa kutumia mafuta ya IPTL, Aggreko na Symbion ilizimwa na hivyo kupelekea TANESCO kuokoa hasara ya kiasi cha Tsh Bilioni 719 kwa mwaka.

Pia TANESCO ilifanikiwa kuanza kununua vifaa vya umeme ndani ya nchi kama nguzo, transfoma, nyaya na mita za Luku hali ambayo ilipelekea kuokoa kiasi cha Tsh Bilioni 162.23 kwa mwaka huku madeni sugu ya TANESCO yakipungua kutoka Tsh Bilioni 272 hadi Tsh. Bilioni 49.

Hivyo amesema kwa ongezeko hilo kubwa la mapato ya TANESCO na kwa kuokoa fedha nyingi zilizokuwa zinalipwa kwenye mikataba mibovu suala la ukosefu wa fedha za matengenezo linatoka wapi.

Mpina amehoji kuwa Waziri wa Nishati ameeleza kuwa ukarabati na matengenezo ulikuwa haufanyiki kikamilifu kutokana na fedha kidogo zilizokuwa zikitengwa na TANESCO katika bajeti (Repair and Maintenance), je ukarabati na matengenezo yanayoendelea hivi sasa yanatumia fedha gani kwa kuwa bado tuko ndani bajeti ya mwaka 2021/2022.

Hata hivyo, katika kipindi cha miaka 5 kazi kubwa ilifanyika ya kujenga miradi mipya mikubwa ya kuzalisha umeme, vituo vikubwa vya kupoza umeme (Sub-Stations) na kukarabati mitambo ya kufua umeme na miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme ambapo ilipelekea kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme kutoka Mw 1,309 mwaka 2015 hadi Mw 1,605.86 mwaka 2020. Ongezeko hili limewezesha nchi yetu kuwa na umeme wa ziada Mw 187.

Pia usambazaji wa umeme vijijini uliongezeka kutoka vijiji 2,018 mwaka 2015 hadi kufikia vijiji 10,312 mwaka 2020 na idadi ya watumiaji umeme ikaongezeka kutoka asilimia 35 mpaka asilimia 85.

Hata hivyo Mpina amesema ukarabati na matengenezo ya mitambo na miundombinu ya umeme haifanyiki yote kwa pamoja lakini pia tuna umeme wa ziada Mw 187 ambao unaruhusu kufanya ukarabati na matengenezo kwa awamu bila kukata umeme.

“TANESCO ilikuwa ikifanya kazi zake vizuri licha ya changamoto ilizonazo na hatukuwahi kuwa na katikakatika ya umeme ya aina hii na sasa yameibuka madai mapya kwamba hadi TANESCO ipate Trilioni 2 za ukarabati na matengenezo ndio mgao wa umeme utaisha nchini” amesema Mpina.

Hivyo amesema kwa kuwa sababu zinazotolewa na Waziri wa Nishati kuhusu kukatikakatika na mgao wa umeme unaondelea hivi sasa hazieleweki na zinaleta mkanganyiko na hofu kubwa kwa wananchi wanaotegemea umeme kuendesha maisha yao.

Na kwa kuwa, kila inapohojiwa kuhusu tatizo kubwa la umeme nchini Waziri wa Nishati amekuwa akisema asiandamwe na asishambuliwe binafsi katika suala hili.

“Hivyo basi Mheshimiwa Naibu Spika kwa heshima na unyenyevu mkubwa nakuomba ukubali Bunge lako Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liunde Kamati Teule ya Bunge ili pamoja na mambo mengine Kamati ichunguze kwa kina chanzo na sababu za kukatikakatika na mgao wa umeme unaondelea, kuchunguza kwa kina uwezo wa Bodi na Menejimenti ya TANESCO katika kuliongoza shirika na kupendekeza hatua za kuchukua” aliomba Mpina.

Aidha kuhusu kuchelewa kwa ujenzi wa Mradi wa Bwawa la kufua Umeme la Julius Nyerere Megawati 2,115, Mpina amesema Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imeeleza mradi huu utekelezaji wake unasuasua na uko nyuma kwa asilimia 44.13 kulingana na mpango kazi uliokubalika kimkataba.

Huku sababu za kuchelewa zikielezwa kuwa ni mkandarasi kushindwa kufuata mpango kazi wa mradi na mkandarasi kushindwa kutekeleza masharti ya mkataba.

Mpina amesema tangu mradi huo ulipoanza kujengwa tarehe 15, Juni 2019 ilipofikia Mwezi Mei 2021 Serikali na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini zilieleza kwamba ujenzi wa mradi huu ulikuwa umefikia asilimia 52 na hapakuwa na changamoto yoyote na wananchi waliahidiwa kuwa kufikia Novemba 15, 2021 maji yataanza kuingizwa kwenye bwawa bila kukosa ikiwa ni hatua muhimu ya ukamilishaji wa mradi huo.

Lakini maelezo ya Waziri wa Nishati kuwa siku ya kwanza anaripoti ofisini Septemba 2021 mradi ulikuwa umechelewa kwa siku 477 inaleta maswali mengi .

Mpina amesema kufikia Disemba 2021 Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imeripoti kuwa mradi huu umefikia asilimia 53.25 tu ambapo kimkataba ulipaswa kuwa umefikia asilimia 97.38 ukiwa nyuma ya utekelezaji kwa asilimia 44.13.

“Hii ina maana kwamba kuna ongezeko la asilimia 1.25 tu katika kipindi chote cha Miezi 7 iliyopita yaani kutoka Mei hadi Disemba 2021 hii ni ishara kwamba ujenzi wa mradi huu unasuasua na hauwezi kukamilika tarehe 14 Juni 2022 kama ilivyopangwa kwa mujibu wa mkataba” amesema Mpina.

Mpina amesema mradi huo umekuwa ukikaguliwa mara kwa mara na umekuwa ukitembelewa na viongozi mbalimbali zikiwemo Kamati za Bunge, Viongozi Wakuu wa Kitaifa na haijawahi kuelezwa kama kuna changamoto yoyote ya utekelezaji wa mradi huo na kwamba fedha zote zilizohitajika zilitolewa na Serikali kwa wakati.

Amesema ilipofika Oktoba 2021 ilielezwa kuwa mkandarasi hataweza kuingiza maji kwenye bwawa Novemba 15, 2021 kwa kuwa mkandarasi alikaidi kufuata design iliyowekwa na wataalamu ya kujenga mahandaki matatu ya kuchepusha maji ya Mto Rufiji na badala yake akajenga handaki moja hali iliyopelekea kuchelewa kukamilisha kazi hiyo, wakati huo huo sababu zilizowasilishwa na mkandarasi za kusingizia Uviko- 19 zilikataliwa na Serikali.

Mpina akaongeza kuwa baadaye Serikali ilitoa sababu nyingine zilizopelekea kuchelewa kuingiza maji kwenye bwawa kufikia Novemba 15, 2021 kuwa ni mkandarasi kuchelewa kuleta mitambo ya kubebea milango (Hoist Crane System) kutokana na viwanda kufungwa na safari za meli kuathiriwa na janga la Uviko-19.

Aidha ameongeza kuwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini ililieleza Bunge sababu 9 zilizotolewa na Serikali juu ya kusuasua kwa mradi huo ambazo zote zimesababishwa na mkandarasi kushindwa kufuata mpango kazi na kutekeleza masharti ya mkataba lakini jambo la kusikitisha hadi sasa hakuna hatua yoyote kwa mujibu wa mkataba iliyochukuliwa na Serikali dhidi ya mkandarasi huyo.

Mpina amesema kwa kuwa Serikali imekuwa ikitoa majibu kinzani kila inapopata nafasi ya kueleza sababu za kuchelewa kwa ujenzi wa mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere.

Na kwa kuwa hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa kwa mkandarasi kwa mujibu wa mkataba hadi sasa licha ya mradi kuripotiwa kuchelewa kwa asilimia 44.13

“Hivyo basi naliomba Bunge lako Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liunde Kamati Teule ili pamoja na mambo mengine kuchunguza kwa kina sababu na chanzo cha kusuasua ujenzi wa mradi wa Bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Julius Nyerere na kupendekeza hatua za kuchukua ili kunusuru mradi huu mkubwa”amesema Mpina.

Mbali na suala la umeme, pia Mpina ameitaka Serikali kuijengea uwezo wa kifedha na rasilimali watu Ofisi ya Msajili wa Hazina ili iweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu ya kuyasimamia Mashirika ya Umma yapatayo 237 ambapo kwa sasa uwezo wake wa kusimamia ni asilimia 13 tu.

Mpina amesema ukurasa wa 31 wa Taarifa ya Kamati ya Bajeti jedwali namba 1 linaloonyesha mwenendo wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali ambapo mapato yasiyo ya kodi hadi kufikia Disemba 2021 yalikuwa ni asilimia 36 tu.

“Hapa Serikali haijaleta mchanganuo wa kila wizara na taasisi na kiasi kilichokusanywa ili kuliwezesha Bunge kujua ni wizara gani na taasisi gani iliyoshindwa kukusanya kikamilifu mapato ya Serikali. Makusanyo ya miezi 6 kuwa asilimia 36 ina maana kuwa hakuna uwezekano wa kufikia asilimia 100 kama ilivyopangwa, mwaka wa fedha uliopita tulielezwa sababu ya kushindwa kukusanya mapato ya Serikali ilitokana na athari za janga la Uviko-19, leo tuelezwe sababu ya kuporomoka kwa mapato yasiyo ya kodi ni nini huku kukiwa hakuna Corona”amehoji Mpina.

Katika hatua nyingine Mpina ameeleza kusikitishwa kwake namna ajira za watanzania zinavyopokwa na wageni katika nchi yetu, ajira za watanzania hazina ulinzi hali iliyopelekea nguvu kazi ya watanzania wapatao milioni 60 kutoshiriki kikamilifu katika shughuli za kuleta maendeleo ya nchi yao, huku ajira zao zikichukuliwa na wageni na wao kubaki watazamaji.

Mpina amesema iko mifano ya Serikali kununua bidhaa na huduma nje ya nchi hata zile zinazopatikana nchini mfano Wizara ya Mifugo na Uvuvi mwaka 2021/2022 imeanza kuagiza dawa za kuogesha mifugo kutoka nje ya nchi wakati kuna viwanda vya watanzania vilivyoajiri wazawa na vinazalisha dawa hizo kwa wingi na zenye ubora unaostahili.

Aidha ametolea mfano mwingine ni ujenzi wa barabara na madaraja kupewa wageni hata kwa miradi ambayo ingeweza kutekelezwa na wazawa, mfano huko Maswa mkoani Simiyu barabara ya lami ya kilomita 11 amepewa mkandarasi kutoka nje ya nchi na mshauri elekezi kutoka nje.

Eneo lingine ni kitendo cha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuingia mkataba Novemba 2021 na Kampuni ya Kimataifa ya Teknolojia ya India Tech Mahindra wa Tsh. Bilioni 69 ili kuboresha utoaji huduma kwa mtandao huku nchi yetu ikiwa imepiga hatua kubwa sana katika ujenzi wa mifumo ya TEHAMA.

“Tuna vijana wabobezi nchini wa kupigiwa mfano na wamebuni mifumo mingi ikiwemo GePG, Max Malipo nk. iweje leo washindwe kujenga mfumo utakaowafaa TANESCO haya yote yanafanyika Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge lipo na Serikali ipo” amesema Mpina.

Post a Comment

0 Comments