***********
Naibu Waziri wa Kilimo Mh Anthony Mavunde amezitaka Taasisi za Fedha nchini kuweka masharti nafuu ya mikopo kwa wakulima ili waweze kukopesheka na iwasaidie kulima kwa tija na kuongeza uzalishajiwa mazao nchini.
Naibu Waziri Mavunde ameyasema hayo leo katika Vijiji vya Isinde na Songambele vilivyopo Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo,Mkoani Katavi wakati akizungumza na wakulima maeneo hayo ikiwa ni muendelezo wa ziara ya ukaguzi wa miradi iliyofadhiliwa na Shirika la Mageuzi ya Kijani Afrika-AGRA.
Mkulima Aniceth Gosberth na Muuzaji wa pembejeo za kilimo Eutropia Sangu wameiomba serikali isaidie ulegezwaji wa masharti ya mikopo kwa Taasisi za fedha ili wakopesheke kwa kuwa wanaamini wakipata mitaji zaidi wataweza kuimarisha kilimo na kuongeza tija.
“Ni kweli masharti ya mikopo inayotolewa na Taasisi nyingi za fedha si rafiki kwa mkulima mdogo kukopesheka,ninafahamu kwamba Taasisi za fedha zinaongozwa na sheria ya Benki Kuu juu ya masharti ya mikopo lakini ziangalie namna nzuri ya kuweka masharti nafuu kwa wakulima kukopesheka kirahisi pasipo kuathiri takwa la Benki Kuu.
Mh Rais Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo ya Taasisi za fedha kupunguza riba zao kwa mikopo ya kilimo na kwasasa tumeanza kushuhudia Benki nyingi zikitoza riba isiyozidi 10% kwenye mikopo ya Kilimo.Hi hatua kubwa katika kuelekea kuwa riba ya tarakimu moja kwenye mikopo ya Kilimo hapa nchini ili kuchochea ukuaji wa sekta ya kilimo”Alisema Mavunde
Ziara hii inayoongozwa na Mjumbe wa Bodi ya AGRA na Rais Mstaafu Dr.Jakaya Kikwete pamoja na Makamu wa Rais wa AGRA Bi. Aggy Konde imehitimishwa leo baada ya kukagua miradi zaidi ya 20 katika mikoa ya Iringa,Mbeya Songwe,Rukwa na Katavi ambapo zaidi ya wakulima,wauza pembejeo na wasindikaji 100,000 wamenufaika na ufadhili wa AGRA kupitia huduma mbalimbali.
0 Comments