Ticker

6/recent/ticker-posts

WANANCHI 57,638 WAPATA CHANJO YA UVIKO-19 RUKWA: DKT. KASULULU


Chifu Kiongozi wa Wafipa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mstaafu Joachim Wangabo akipata dozi ya pili ya chanjo ya Sinopharm jana mjini Sumbawanga wakati wa kikao cha Umoja wa Machifu wa Rukwa . Kulia ni Muuguzi Mkunga Noelia Ndotela kutoka kituo cha Afya Mazwi.

Mwenyekiti wa Umoja wa Machifu mkoa wa Rukwa Chifu Charles Chiringo Katata akizungumza jana kuwasihi machifu wenzake kuwa mstari wa mbele kuchanja chanjo dhidi ya UVIKO -19 wakati wa kikao cha viongozi hao.

Chifu Msaidizi Himaya ya Uchile Laela wilaya ya Sumbawanga Mzee Adam Matheo Ulaya akipata dozi ya kwanza ya chanjo ya Uviko-19 aina ya Sinopharm wakati wa kikao cha machifu wa mkoa wa Rukwa jana mjini Sumbawanga.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu akitoa elimu ya umuhimu wa chanjo ya UVIKO-19 kwenye kikao cha Umoja wa Machifu wa Rukwa kilichofanyika mjini Sumbawanga ambapo pia chanjo ilitolewa.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti (katikati) akifungua kikao cha Umoja wa Machifu wa Rukwa jana mjini Sumbawanga. Wa kwanza kushoto ni Chifu Kiongozi wa Wafipa na Mkuu wa Mkoa Mstaafu Joachim Wangabo na kulia ni Mwenyekiti wa Machifu Rukwa Chifu Charles Chilingo Katata.
Sehemu ya Machifu wa kabila la Wafipa toka wilaya za Rukwa wakiwa kwenye kikao cha umoja wao jana mjini Sumbawanga ambapo walipatiwa elimu ya umuhimu wa chanjo ya Uviko-19 na kuchanja.

(Habari na Picha na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa).

*********************


Na OMM Rukwa

Wananchi wa mkoa wa Rukwa wamepongezwa kwa kujitokeza kupata chanjo ya kinga dhidi ya ugonjwa wa Korona ambapo hadi kufikia mwezi Januari mwaka huu watu 57,638 wamefanikiwa kupata chanjo hiyo katika vituo vya afya.

Akizungumza kwenye kikao cha Umoja wa Machifu wa mkoa wa Rukwa jana (19.01.2022) mjini Sumbawanga, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu alisema tangu zoezi hilo la kutoa dozi za chanjo lilipoanza mwezi Julai 2021 kumekuwa na mwitikio mzuri toka kwa wananchi.

Mganga Mkuu huyo alieleza mafanikio ya chanjo kwa wananchi yaliyopatikana ni pamoja na kupungua kwa watu waliolazwa kwa maambukizi ya korona pia kutokuwepo taarifa za watu waliopata madhara baada ya kupata dozi ya chanjo ya UVIKO-19.

“Kwa kupitia chanjo ya kinga dhidi ya UVIKO-19 hatusikii tena kusongamana kwa wagonjwa wodini hata vifo vimepungua kwenye mkoa wetu. Rukwa tulipokea dozi 68,683 za chanjo ya UVIKO-19 ambapo watu 57,638 sawa na asilimia 84 tayari wamechanjwa” alieleza Dkt. Kasululu.

Kwa upande wake Chifu Kiongozi wa Machifu Mkoa wa Rukwa na Mkuu wa Mkoa Mstaafu Joachim Wangabo aliwasihi Machifu kwenda kuelimisha na kuhamasisha jamii hususan Wazee kujitokeza kupata chanjo.

Chifu Wangabo alisema yeye binafsi tayari amechanja na kuwa leo pia atarudia kupata dozi ya pili ya chanjo ili kukamilisha kwa mujibu wa utaratibu wa wataalam na kuongeza kuwa serikali imelenga kuwafanya wananchi wake wawe salama na wenye kinga dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19.

Akizungumza kwenye kikao hicho Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Joseph Mkirikiti aliwataka viongozi hao wa Machifu kufundisha maadili mema kwa jamii ili amani na maendeleo kwa mkoa yaendelee kupatikana kwani viongozi hao wanaheshimika vizuri kwenye jamii.

Post a Comment

0 Comments