Ticker

6/recent/ticker-posts

POLISI WATENDAJI DAWATI LA JINSIA SHINYANGA WATAKIWA KUZINGATIA MAADILI WANAPOHUDUMIA WAATHIRIKA MATUKIO YA UKATILI

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Joseph Kiyengi Paul akizungumza wakati akifungua mafunzo Kazini kwa Askari Polisi Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto.


Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Askari Polisi watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Shinyanga wamekumbushwa kuzingatia maadili ya kazi yao na kuchukua hatua za haraka wakati wakiwahudumia Waathirika/Madhura wa matukio ya ukatili wa kijinsia ili wale waliofanya makosa waweze kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.


Hayo yamesemwa na Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Joseph Kiyengi Paul leo Jumatatu Januari 24,2022 wakati akifungua mafunzo Kazini kwa Askari Polisi Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto yaliyoandaliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kwa ufadhili wa Shirika la Women Fund Tanzania ‘WFT’ ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto.


Kaimu Kamanda Paul , amewataka askari polisi kuzingatia maadili mema ya kazi yao ili kutokomeza matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.


“Dawati la Jinsia ni mahali ambapo wameathiriwa kwa namna moja nyingine wanakwenda kupata huduma, kwa hiyo sisi watendaji wa dawati lazima tuwe na moyo wa kuwasaidia kweli kweli hawa watu wanaotaka huduma. Kuna akina mama, kuna watoto,mama anaweza kuwa amebakwa sasa namna ya kumhudumia yule ni lazima uwe na huruma nae kwa sababu anapokuja pale anakuwa na matumaini ya kupata msaada,lazima tumpokee vizuri, tumsikilize vizuri kwa mazingira ya usiri ili aweze kuwa huru kuona kuwa yupo salama”,amesema Paul.


“Na ni lazima tuchukue hatua za haraka kwa mfano kesi za kubaka,amebakwa anatakiwa apelekwe hospitali mapema wakachunguze waone,daktari aandike taarifa yake ambayo itasaidia kwenye ushahidi. Watoto mara nyingi wanakuwa waoga lakini lazima tutengeneze mazingira ambayo yatawafanya wawe huru kueleza matatizo yao,kuna unyanyasaji mwingi unafanywa kwa watoto,tunatakiwa tuwasaidie haraka iwezekanavyo”,ameeleza Paul.


Aidha amewakumbusha askari polisi kuwahudumia wananchi bila uoga wala upendeleo wowote na kuwashughulikia kwa mujibu sheria kwa kuzingatia maadili na miongozo ya kazi.


“Madhura/wahanga wanaofika kwetu wanategemea kuwa watapata msaada kwetu kwa hiyo ni lazima tuwapokee vizuri, tuwasikilize vizuri na tuchukue hatua zote za kisheria, tujenge ushahidi wa kesi za ukatili dhidi ya wanawake na watoto ili wale waliofanya makosa waweze kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria”, ameongeza Paul.


Kwa upande wake, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Ushirikishwaji Jamii Mkoa wa Shinyanga SSP Monica Venance Sehere amewataka Watendaji wa dawati la jinsia kutunza siri za wahanga/madhura wa matukio ya ukatili wa kijinsia na kutoa ushirikiano mkubwa kwa wapelelezi wanaopewa majalada ya matukio ya ukatili wa kijinsia.


“Tunachotakiwa kufanya ni kumsaidia aliyefanyiwa ukatili na mtuhumiwa apate haki yake kwa mujibu wa sheria”,amesema Sehere.


Mkuu wa Intelijensia Mkoa wa Shinyanga ACP Revocatus Cosmas amewasisitiza askari polisi kutunza siri kutoka kwenye jamii wakiwemo madhura wa matukio ya ukatili wa kijinsia kwani madhara ya kutotunza siri ni pamoja na kuharibu upelelezi,kuleta usaliti miongoni mwa watendaji na kusababisha uhasama miongoni mwa jamii hali inayosababisha kutokea matukio mengine ya uhalifu.


Naye Mkuu wa Idara ya Uchunguzi wa Kisayansi Mkoa wa Shinyanga ASP Juma Sadiki Bahati ametaka elimu iendelee kutolewa katika jamii kwamba mwanamke anafanyiwa ukatili wa kubakwa asioge mpaka pale atakapopatiwa huduma baada ya kuripoti kituo cha polisi ili kutunza ushahidi.


“Mwanamke anapobakwa asioge hata kama atakuwa amechafuka kiasi gani wakati wa purukushani za ubakaji kwa huo ni ushahidi wake mkuu. Huo uchafu ni ushahidi wake katika kesi ya ubakaji ili kukomesha matendo maovu ya wanaume waovu. Nendeni mkatoe elimu hii kwa jamii”,amesema Bahati.


Wakili wa Serikali Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Shani Wampumbulya akielezea kuhusu Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 amesema katika usikilizwaji wa mashauri ya mtoto kunakuwa na usiri unaotakiwa ufanyike mahakamani ambapo sheria hiyo ilianzisha mahakama ya mtoto na sheria hiyo haitaki kupeleka kesi ya mtoto mahakamani upelelezi ukiwa unaendelea na ndani ya miezi shauri lake liwe limesikilizwa na kutolewa maamuzi.


“Katika kuwakamata watoto waliokinzana na sheria kwenye kuwaweka mahabusu sheria haitaki wachanganywe na watu wazima kutokana na umri wao.Hivyo kama kutakuwa na vyumba tofauti ni muhimu kumuweka mtoto chini ya uangalizi wa polisi basi awekwe chumba cha tofauti lakini kama hapatakuwa na uhatarishi wowote wa mazingira yake akiwa nje itapendeza akipewa dhamana akakae nyumbani hadi kipindi ambacho upelelezi utakuwa umekamilika kisha kufikishwa mahakamani”,amesema Wampumbulya.


Mratibu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Shinyanga, Mkaguzi wa Polisi Analyse Kaika amesema Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limepata Ruzuku kutoka Taasisi ya Women Fund Trust ‘WFT’ kwa ajili ya kutekeleza Mradi wa Kupinga Ukatili dhidi ya wanawake na watoto katika Halmashauri za wilaya ya Shinyanga.


Amesema Mafunzo Kazini kwa askari polisi watendaji wa dawati la Jinsia na Watoto yamelenga kukumbushana baadhi ya sheria, vipengele,taratibu, kanuni wanazopaswa kuzingatia watendaji wa dawati la Jinsia ili kuepuka kukengeuka au kupishana na miongozo ya nchi.


Kaika amezitaja baadhi ya mada zilizotolewa wakati wa mafunzo hayo ni maadili ya askari wa jeshi la polisi,Usiri wa taarifa kutoka kwenye jamii,majukumu ya dawati la jinsia na watoto,sheria ya mtoto ya mwaka 2009,jinsi ya kutunza ushahidi wa makosa ya jinai, sura 16 (R.E 2019) inavyomlinda mtoto na jinsi ya kutunza ushahidi wa makosa ya jinai.


Mada zingine ni Jinsi sheria ya ndoa Sura ya 29 (R.E 2019) inavyomlinda mtoto/mwanamke, sheria ya kanuni ya adhabu inavyomlinda mtoto/mwanamke,sheria ya elimu inayomlinda mtoto/mwanafunzi, sheria inasemaje kuhusu wanaokula njama ya kutenda kosa la jinai na adhabu dhidi yao, upelelezi wenye tija,jinsi ya kuhoji watoto na jinsi ya kuhudumia madhura wa ukatili wa kubaka na kulawiti.


ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Joseph Kiyengi Paul akizungumza wakati akifungua mafunzo Kazini kwa Askari Polisi Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto yaliyoandaliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga kwa ufadhili wa Taasisi ya Women Fund Trust ‘WFT’ leo Jumatatu Januari 24,2022 katika ukumbi wa Bwalo la Polisi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kupinga ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Picha na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Joseph Kiyengi Paul akitoa mada kuhusu Maadili ya Askari wa Jeshi la Polisi wakati akifungua mafunzo Kazini kwa Askari Polisi Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto. Kushoto ni Mkuu wa Intelijensia Mkoa wa Shinyanga ACP Revocatus Cosmas. Kulia ni Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Ushirikishwaji Jamii Mkoa wa Shinyanga SSP Monica Venance Sehere
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Joseph Kiyengi Paul akitoa mada kuhusu Maadili ya Askari wa Jeshi la Polisi wakati akifungua mafunzo Kazini kwa Askari Polisi Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto.

Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Ushirikishwaji Jamii Mkoa wa Shinyanga SSP Monica Venance Sehere akizungumza kwenye mafunzo Kazini kwa Askari Polisi Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto.
Wakili wa Serikali Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Shani Wampumbulya akitoa mada kuhusu Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 kwenye mafunzo Kazini kwa Askari Polisi Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto.
Mratibu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Shinyanga, Mkaguzi wa Polisi Analyse Kaika akizungumza kwenye mafunzo Kazini kwa Askari Polisi Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto.
Mratibu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Shinyanga, Mkaguzi wa Polisi Analyse Kaika akielezea lengo la mafunzo kazini kwa polisi watendaji wa dawati la Jinsia na watoto.
Mkuu wa Intelijensia Mkoa wa Shinyanga ACP Revocatus Cosmas akitoa mada kuhusu Usiri wa taarifa kutoka kwenye jamii wakati wa mafunzo Kazini kwa Askari Polisi Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto.
Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Brighton Rutajama akizungumza kwenye mafunzo Kazini kwa Askari Polisi Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto.
Mkuu wa Idara ya Uchunguzi wa Kisayansi Mkoa wa Shinyanga ASP Juma Sadiki Bahati akitoa mada jinsi ya kutunza ushahidi wa makosa ya jinai wakati wa mafunzo Kazini kwa Askari Polisi Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto.
Afisa kutoka Dawati la Jinsia na Watoto jeshi la polisi wilaya ya Shinyanga, Secilia Kizza akitoa mada jinsi ya kumhoji mtoto aliyefanyiwa ukatili wa kubakwa au kulawitiwa pia kuhoji watu waliofanyiwa ukatili wa kubakwa, kulawiti wakati wa mafunzo Kazini kwa Askari Polisi Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto.
Afisa kutoka Dawati la Jinsia na Watoto jeshi la polisi wilaya ya Shinyanga ,Afande Vivian Zabron akitoa mada jinsi ya kumhoji mtoto aliyefanyiwa ukatili wa kubakwa au kulawitiwa pia kuhoji watu waliofanyiwa ukatili wa kubakwa, kulawiti wakati wa mafunzo Kazini kwa Askari Polisi Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Joseph Kiyengi Paul (katikati) ,Mkuu wa Intelijensia Mkoa wa Shinyanga ACP Revocatus Cosmas (kushoto) na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Ushirikishwaji Jamii Mkoa wa Shinyanga SSP Monica Venance Sehere wakiwa kwenye mafunzo Kazini kwa Askari Polisi Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto.
Askari Polisi wakiwa kwenye mafunzo Kazini kwa Askari Polisi Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto.
Mafunzo Kazini kwa Askari Polisi Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto yakiendelea
Askari Polisi wakiwa kwenye mafunzo Kazini kwa Askari Polisi Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto.
Askari Polisi wakiwa kwenye mafunzo Kazini kwa Askari Polisi Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto.
Askari Polisi wakiwa kwenye mafunzo Kazini kwa Askari Polisi Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto.
Askari Polisi wakiwa kwenye mafunzo Kazini kwa Askari Polisi Watendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto.

Post a Comment

0 Comments