Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo akipanda mti aina ya mkoko katika hafla ya uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti aina ya mikoko katika delta ya Mto Rufiji. Uzinduzi huo umefanyika mwishoni mwa wiki katika Kijiji cha Mbuchi, tarafa ya Mbwela, Wilaya ya Kibiti.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) akikagua maendeleo ya ujenzi wa daraja katika kijiji cha Mbuchi, wilayani Kibiti Dkt. Jafo ametoa rai kwa jamii ya eneo hilo kupanda mikoko kwa wingi ili kuzuia mmomonyoko wa udongo na kupunguza kasi ya maji wakati wa mkutano wa hadhara kijijini hapo.
Wakazi wa Kijiji cha Mbuchi, tarafa ya Mbwela, Wilaya ya Kibiti wakimsikilizaWaziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo katika mkutano wa hadhara kijijini hapo na Dkt. Jafo amesisitiza agenda ya mazingira
**********************
Wakazi wa Kijiji cha Mbuchi, Tarafa ya Mbwela, Wilaya ya Kibiti wametakiwa kupanda miti aina ya mikoko katika Delta ya Mto Rufiji ili kulinda miundombinu inayojengwa na Serikali kwa gharama kubwa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa daraja unaoendelea katika Kijiji cha Mbuchi.
Wito huu umetolewa mwishoni mwa wiki na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt. Selemani Jafo baada ya kuzindua kampeni ya upandaji miti aina ya mikoko katika kijiji cha Mbuchi.
Dkt. Jafo amewata wakazi wa Mbuchi kuongeza kasi ya upandaji miti aina ya mikoko kwa lengo la kupunguza kasi ya maji na mmomonyoko wa ardhi pembezoni mwa daraja linalojengwa katika Kijiji cha Mbuchi sambamba na kuhifadhi mazingira
Amesema Serikali inatenga fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha miundombinu na kutolea mfano wa barabara na madaraja, hivyo wananchi wana wajibu wa kuhakikisha wanakuwa walinzi namba moja wa rasilimali hizo na kuwabaini wahujumu ili waweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria.
"Uimara wa daraja hili linalojengwa hapa Mbuchi utategemea sana uhifadhi wa mazingira yetu, tupande mikoko kwa wingi" Alisisitiza Dkt. Jafo
Pia amesema Serikali imezindua kampeni ya upandaji miti katika ngazi ya kaya na wanafunzi mashuleni. "Tumezindua kampeni ya upandaji miti ambapo kila kaya inatakiwa kupanda na kutunza miti walau mitatu (3) na mti mmoja (1) kwa kila mwanafunzi" Alifafanua Dkt. Jafo
Nae Mkuu wa Wilaya ya Kibiti Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema kuwa zaidi ya nusu ya mikoko yote inayopatikana Tanzania iko katila Delta ya Rufiji hivyo kupitia kamati za ulinzi katika ngazi zote watahahikisha kasi ya upandaji wa mikoko na ulinzi unaimarika.
0 Comments