Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Mhe. Luhaga Joelson Mpina (kulia) akionesha fomu yake ya kuwania nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania muda mfupi baada ya kukabidhiwa na Katibu wa Kamati ya NEC, Organaizesheni ya Chama cha Mapinduzi Zanzibar, Ndugu Cassian Galosi Nyimbo, Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar Januari 14,2022.
Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Mhe. Luhaga Joelson Mpina akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar Januari 14,2022.
Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Mhe. Luhaga Joelson Mpina akiwasili katika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui, Zanzibar kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Januari 14,2022.
Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Mhe. Luhaga Joelson Mpina akitoa heshima mbele ya Kaburi la Rais wa Kwanza wa Zanzibar na mmoja wa waasisi wa Muungano wa Tanzania, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume muda mfupi baada ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya Spika katika Afisi Kuu ya CCM, Kisiwandui Zanzibar, Januari 14, 2022.
Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Mhe. Luhaga Joelson Mpina akiomba dua baada ya kuzuru Kaburi la Rais wa Kwanza wa Zanzibar na mmoja wa waasisi wa Muungano wa Tanzania, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume muda mfupi baada ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya Spika katika Afisi Kuu ya CCM, Kisiwandui Zanzibar, Januari 14, 2022.
Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Mhe. Luhaga Joelson Mpina akitoa heshima mbele ya Kaburi la Rais wa Kwanza wa Zanzibar na mmoja wa waasisi wa Muungano wa Tanzania, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume muda mfupi baada ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya Spika katika Afisi Kuu ya CCM, Kisiwandui Zanzibar, Januari 14, 2022.
Mbunge wa Jimbo la Kisesa, Mhe. Luhaga Joelson Mpina (kulia) akizungumza na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Abdulla Juma Sadalla muda mfupi baada ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya Spika katika Afisi Kuu ya CCM, Kisiwandui Zanzibar, Januari 14, 2022.
********************
MBUNGE wa Jimbo la Kisesa, Mhe. Luhaga Joelson Mpina amechukua fomu ya kuwania nafasi ya Spika wa Bunge katika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar huku akibainisha kuwa kwa sasa wananchi wanahitaji Spika imara, jasiri na mwenye weledi asiyeyumba wala kuyumbishwa na mtu yoyote katika kuusimia mhimili huo.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu hiyo Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar na kutembelea Kaburi la Rais wa kwanza wa Zanzibar na mmoja ya waasisi wa Muungano, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume, Mpina amesema kwa sasa wananchi wanahitaji Bunge imara litakaloisimamia Serikali kutekeleza majukumu yake kikamilifu, lenye nguvu ya kushauri, lenye nguvu ya kushawishi, lenye nguvu ya kukosoa na lenye nguvu na uwezo wa kukataa mipango mibovu ya Serikali.
“Wananchi wanahitaji Spika imara, jasiri na mwenye weledi asiyeyumba wala kuyumbishwa na mtu yoyote, sifa hizi ninazo endapo Chama changu cha Mapinduzi na waheshimiwa Wabunge wataridhia kunikabidhi usukani huu nitalifanya Bunge hili kuwa la mfano Afrika, Nchi za Jumuiya ya Madola na dunia kwa ujumla”amesema Mpina.
Mpina amesema anatambua pia wananchi wanahitaji Bunge lao liwe la namna gani hasa katika kipindi hiki cha mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii ambapo nchi yetu imeingia katika uchumi wa kati hivyo anao uzoefu na uwezo wa kuongoza Bunge kwa weledi mkubwa ukizingatia uzoefu wake wa vipindi vinne mfululizo bungeni, Mbunge wa Bunge la Afrika, Mjumbe na Mwenyekiti wa Kamati mbalimbali za kudumu za Bunge, Kamishna wa vyuo vikuu, Naibu Waziri na Waziri.
“Lakini pia elimu yangu si ya kutiliwa mashaka kushika na kumudu majukumu ya Spika ambapo kwa sasa nina Shahada ya Uhasibu na Fedha kutoka Chuo Kikuu Mzumbe, Nina Shahada ya Uzamili ya Sayansi ya Fedha (Msc-Finance) kutoka Chuo Kikuu cha Strathclyde nchini Uingereza na sasa ninafanya Shahada ya Uzamivu yaani PhD katika masuala ya usimamizi wa fedha za Umma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam” amesema Mpina.
Mpina amesema kwa sasa Bunge linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mfumo dhaifu wa upitishaji wa maazimio bungeni ambapo utaratibu wa sasa unaotumiwa na Spika au kiongozi wa Bunge kupitisha uamuzi kwa kuuliza wanaokubali waseme ndiyo na wanaokataa waseme siyo.
“Upigaji kura wa namna hii umekuwa machinjio ya demokrasia ya wabunge kuamua kwa haki mambo mazito kwa mustakabali wa taifa letu” amesema Mpina.
Pia Mpina amebainisha kuwa changamoto nyingine zinazolikabili Bunge kwa sasa ni kitendo cha Taarifa za ukaguzi za CAG, PPRA na PCCB kutokufanyiwa kazi kikamilifu kwa masilahi mapana ya watanzania.
“Taarifa ya CAG kujadiliwa kwa muda mfupi na kuamuliwa, uchukuaji dhaifu wa hatua dhidi ya wezi na wabadhirifu wa fedha za umma na hakuna mrejesho bungeni juu ya marekebisho na hatua zilizochukuliwa hali inayopelekea makosa na wizi kujirudia kila mwaka wa fedha”amesema Mpina
Pia Mpina amesema taarifa ya ukaguzi ya PPRA na PCCB licha ya umuhimu wake lakini haziwasilishwi bungeni kujadiliwa kwani ukaguzi wa manunuzi unaofanywa na PPRA ambao hubeba zaidi ya 70% ya bajeti ya Serikali.
“Wizi unaoibuliwa kila mwaka na PCCB katika maeneo mbalimbali ni taarifa muhimu sana kwa maendeleo ya nchi hivyo ni lazima iwe inaingia bungeni ili kuongeza nguvu ya usimamizi wa rasilimali za umma. Nikiwa Spika sitakubali kikundi cha watu wachache waendelee kutafuna mali za umma” amesema Mpina
Mbali na hilo Mpina amebainisha kuwa kuwepo kwa baadhi ya Sheria mbovu na mikataba mibovu licha ya jitihada kubwa zilizofanyika lakini bado kuna sheria mbovu na mikataba mibovu inayoendelea kuligharimu taifa na pia kuna hatari ya kuingia mikataba mipya mibovu.
“Nikiwa Spika nitaliongoza Bunge kufanyia marekebisho sheria zote mbovu na zilizopita na wakati, kufutwa kwa mikataba mibovu na kuisimamia Serikali ili kutoingia mikataba mibovu tena” amesema Mpina.
Changamoto nyingine aliyoibani Mpina ni kutokuwepo ofisi ya Bajeti na Kitengo cha Utafiti ndani ya Bunge hali inayopelekea kupitisha bajeti ya Serikali kila mwaka bila ya kuwa na taarifa za kutosha kuhusu vipaumbele, ukomo wa bajeti, ugawaji wa rasilimali fedha, kuanzisha kodi mpya, kusamehe kodi, kupunguza au kuongeza viwango vya kodi.
“leo hapa Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar nachukua fomu ya kugombea nafasi ya Spika ndani ya Chama cha Mapinduzi eneo ambalo Mmoja ya waasisi wa Taifa letu la Tanzania na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume aliuawa na kuzikwa ikiwa ni ishara ya kuenzi na kudumisha umoja na mshikamano wa Muungano wa nchi yetu” amesema Mpina.
Kuhusu uwajibikaji wa Serikali kwa Bunge, Mpina amesema baadhi ya Sheria zilizopitishwa na Bunge hazisimamiwi utekelezaji wake kikamilifu na Serikali akitolea mfano Sheria ya Uwekezaji na Local Content.
“Mfano licha ya kuwa na Kampuni ya inayozalisha dawa za kuogesha mifugo nchini lakini Wizara inaagiza dawa za kuogesha mifugo kutoka nje ya nchi hali inayopelekea kudhoofisha juhudi za kukuza uwekezaji wa ndani, kuua ajira za watanzania na kodi za nchi, hii ni hujuma kubwa kwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anayehangaika usiku na mchana kutafuta wawekezaji” amesema Mpina.
Pia kwa upande wa ujenzi wa barabara na madaraja nchini bado mengi yanajengwa na kampuni za kigeni licha ya kuwepo kampuni za wazawa zenye uwezo wa kutekeleza miradi hiyo.
“Mfano zipo barabara zenye urefu wa kilomita 11 zinajengwa na wakandarasi kutoka nje na mshauri mwelekezi kutoka nje ya nchi huku makampuni ya wazawa yakihaha kutafuta kazi, vijana wa kitanzania kukosa ajira na fursa hiyo ikichukuliwa na wageni lakini Bunge liko kimya na Serikali iko kimya” amesema Mpina
Kuhusu waraka uliosambazwa mitandaoni hivi karibuni kuwachafua baadhi ya viongozi ukiwahusisha wastaafu kwa kuwasingizia walikuwa wanamfanyia kampeni Mhe. William Lukuvi awe Spika.
Mpina amesema kuna waraka ambao umesambazwa kwenye mitandao ukimuhusisha yeye kushiriki vikao vya siri na viongozi wengine kumuandaa Mhe. William Lukuvi kuwa Spika wa Bunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Napenda kukanusha waraka huo na kwamba mimi sihusiki na vikao hivyo kwa kuwa mimi ni mgombea wa nafasi ya Spika na ndio maana leo niko hapa kuchukua fomu ya Spika, nimejiuliza sana nini nia na madhumuni ya waraka huo, ulilenga kufanikisha nini na kwanini utolewe wakati huu” amehoji Mpina.
Mpina amesema waraka huo unafikirisha sana kwani kuanzia tarehe 2 hadi tarehe 6 mwezi Januari zilizotajwa kwamba alikuwa Dodoma kushiriki vikao hivyo hivyo ukweli ni kwamba alikuwa na ziara jimboni kwake Kisesa na tarehe 7 Januari alihudhuria vikao vya kamati ya fedha, utawala na mipango pamoja na kamati ya ukimwi katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu Mkoani Simiyu.
“Tarehe 10 Januari nilisafiri kwenda Dar es Salaam kwa ndege kupitia uwanja wa ndege wa Mwanza ushahidi wote ninao. Hivyo si kweli kwamba nilikuwa nashikiri vikao na kuratibu kampeni huko Dodoma waraka huo unatafakarisha zaidi kutoa taarifa za uongo kwa kuwahusisha wastaafu akiwemo Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda kiongozi mnyenyekevu na mwadilifu na aliyelitumikia taifa hili kwa kujitoa kwa hali ya juu iweje leo achafuliwe na kikundi cha watu wachache wenye malengo wanayoyajua wao” amehoji Mpina.
Pia amehoji mamlaka husika kutochukua hatua za kisheria kwa wote waliondaa na kusambaza waraka huo ambao ulionekana pia kumkera Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.
“Najiuliza kwa nini hadi leo TCRA hawajachukua hatua kwa upotoshaji huo mkubwa uliofanywa dhidi yangu na viongozi wengine, hili kundi la watu kwanini linakingiwa kifua na mamlaka husika? Pamoja na Mhe. Rais kulalamikia upotoshaji huo uliofanywa na watu hao lakini bado hadi leo hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa” amehoji Mpina
Kutokana na hali hiyo, Mpina ameamua kuchukua hatua kali za kisheria kwa wote waliohusika kuratibu na kusambaza uongo huo dhidi yake.
“Sitakubali kuchafuliwa kwa namna yoyote, njama na nia ovu zilizopagwa dhidi yangu, nimeamua kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wote waliohusika kuratibu na kusambaza uongo huo, hatutakubali taifa letu kuondoshwa kwenye ajenda za maendeleo na kujadili fitina na majungu ” amesema Mpina
0 Comments