Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akihimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini jijini Dodoma wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao chenye lengo la kujitambulisha na kutoa mwongozo wa utendaji kazi anaouhitaji. Kushoto kwake ni Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi.
Sehemu ya Watumishi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama alipokuwa akihimiza uwajibikaji kwa Watumishi hao jijini Dodoma wakati wa kikao kazi chake na watumishi hao chenye lengo la kujitambulisha na kutoa mwongozo wa utendaji kazi anaouhitaji.
Kaimu Mkurugenzi, Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Bi. Adella Mkude akieleza majukumu ya idara yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati wa kikao kazi cha Waziri huyo na Watumishi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini alichokifanya jijini Dodoma kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.
Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Bi. Jeanfrida Mushumbushi akieleza namna Mfumo Mpya wa Kitanzania wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara unavyofanya kazi kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati wa kikao kazi cha Waziri huyo na Watumishi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini alichokifanya jijini Dodoma kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.
***************************
Na. James K. Mwanamyoto-Dodoma
Tarehe 15 Januari, 2022
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amewataka watumishi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini kujipanga kiutendaji ili kuhakikisha wananchi na Watumishi wa Umma wanaohudumiwa na ofisi yake wanafurahia huduma zinazotolewa.
Mhe. Jenista ametoa wito huo jijini Dodoma, wakati wa kikao kazi chake na Watumishi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa idara hiyo.
Mhe. Jenista amesema kuwa, anataka ufike wakati mtumishi wa umma anayedai haki ambayo amedhurumiwa kwa muda mrefu na mwajiri wake pindi akisikia kuwa suala lake limewasilishwa Ofisi ya Rais-UTUMISHI afurahi na kuwa na matumaini kuwa litafanyiwa kazi kwa wakati.
“Nataka Mtumishi wa Umma aliyekata tamaa ya kutolipwa malimbikizo yake ya mishahara au kupewa stahiki zake nyingine akisikia suala lake limewasilishwa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini afurahi na kuamini kuwa suala lake litafanyiwa kazi kwa haki na wakati,” Mhe. Jenista amefafanua.
Waziri Jenista ameongeza kuwa, Idara hiyo ikifanya kazi kwa uadilifu na weledi itakuwa imetoa mchango mkubwa katika kujenga morali ya utendaji kazi wa Watumishi wa Umma nchini, ikiwa ni pamoja na kujenga imani ya wananchi kwa serikali yao.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi na Watumishi wa Umma kuutumia vema mfumo wa SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI (www.swu.go.tz) kuwasilisha changamoto na malalamiko ya masuala ya kiutumishi na utawala bora ili yaweze kufanyiwa kazi na hatimae wananchi wanufaike na huduma zinazotolewa na taasisi za serikali.
“Mimi Waziri mwenye dhamana ya kumsaidia Mhe. Rais kusimamia masuala ya kiutumishi na utawala bora napenda nipokee changamoto zinazowakabili Watumishi wa Umma kupitia mfumo huu hivyo, watumishi muutumie ipasavyo,” Mhe. Jenista amesisitiza.
Mhe. Jenista anaendelea na vikao kazi na Watumishi wa Ofisi yake tangu aapishwe hivi karibuni na Mhe. Rais kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
0 Comments