Ticker

6/recent/ticker-posts

KATIBU MKUU NZUNDA AITAKA TVLA KUFANYA KAZI KIBIASHARA ZAIDI

Katibu Mkuu Mifugo Bw.Tixon Nzunda Mwenye kaunda Suti kushoto, akikagua baadhi ya Chanjo zinazozalishwa Katika Taasisi ya chanjo Tanzania (TVI) Kibaha.Kulia ni Mkurugenzi wa Huduma za afya ya Mifugo (DVS) Prof.Hezron Nonga
Katibu Mkuu Mifugo Bw.Tixon Nzunda kulia akisikiliza kwa umakini maelezo kutoka kwa Mtendaji Mkuu TVLA Dkt.Stella Bitanyi kushoto juu ya ubora wa chanjo zinazozalishwa na Taasisi yake.



******************************

Na Kumbuka Ndatta


Katibu Mkuu Mifugo Bw.Tixon Nzunda ameelekeza kwamba wakala wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) ifanye kazi Kibiashara ili iweze kujiendesha yenyewe bila kutegemea ruzuku kutoka Serikalini.


Hayo ameyasema leo tarehe 26/01/2022 alipofanya ziara yake ya kwanza tangu alipoteuliwa tarehe 08 Januari 2022, na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo)


"Fanyeni kazi kibiashara na kwa uadilifu mkubwa ,mashamba hayo yanayovamiwa na Wananchi hakikisheni mnayatumia kibiashara, tengeni fedha kwenye bajeti yenu ili yaweze kupimwa ili kuondokana na adhaa ya kuvamiwa na wanachi". Alisema Nzunda.


Katika ziara hiyo, Katibu Mkuu Mifugo Bw.Tixon Nzunda, ameelekeza, Mifumo ya utendaji kazi ya Kielekroniki iimarishwe katika vituo vyote vya Wakala.


Pia, katika kutatua changamoto ya Uhaba wa Watumishi wa wakala hiyo, katibu Mkuu Mifugo amemweelekeza Mtendaji mkuu wa Wakala hiyo kufuatilia maombi ya kuajiri watumishi wapya Ofisi ya Rais Utumishi wa Umma ili kukidhi mahitaji ya taasisi hiyo.


Vile vile Nzunda ameelekeza kuwa Mali za wakala zilindwe, zitunzwe ili ziweze kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa. Pia, ameelekeza Wakala kufanya kazi kwa karibu na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini (GCU) cha Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kutangaza kazi nzuri zinazofanywa na wakala hiyo.


Aidha, Katibu Mkuu Mifugo ameielekeza Wakala hiyo kuandaa mkutano mmoja kila mwaka ili kukutana na wadau wanaotumia chanjo hizo ili kupata mrejesho kutoka wadau hao. Pamoja na Mambo mengine,Katibu Mkuu Mifugo ameelekeza wakala wajikite katika kutafuta masoko ya chanjo hizo nje na ndani ya nchi.


Awali Dkt.Stella Bitanyi, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) alitoa taarifa ya utendaji kazi wa (TVLA) kwa Katibu Mkuu Mifugo Bw.Tixon Nzunda, kuwa, kazi kubwa wanayofanya ni pamoja na uchunguzi na Utambuzi wa Magonjwa ya Wanyama na Wadudu wanaosambaza magojwa na uhakiki wa usalama na Ubora wa Vyakula vya Mifugo.


Pia, wakala inatimiza Majukumu yake kwa kupima,kutathimini na kuhakiki Vitendanishi, mimea tiba pamoja na kemikali zinazotumika katika maabara za Wanyama.Vile vile taasisi hiyo inafanya tafiti za Magonjwa ya wanyama na Wadudu wanaosambaza Magonjwa hayo na kutoa Ushauri/teknolojia ya kudhibiti Magonjwa husika na Wadudu waenezao magonjwa hayo.


Pia, Dkt. Bitanyi amemwambia Bw. Nzunda kuwa TVLA inatengeneza na kuzalisha aina saba (7) chanjo dhidi ya magonjwa ya Mifugo ikiwa ni pamoja vitendanisha.


Aidha, Chanjo za Mifugo zinazozalishwa na TVLA ni pamoja naTemevac,(chanjo dhidi ya Mdondo), Kimeta, Chambavu,Tecoblax (Mchanganyiko wa Kimeta na Chambavu), Kutupa Mimba (Brucellosis), Homa ya Mapafu ya ng'ombe (CBPP) na Homa ya Mapafu ya Mbuzi (CCPP).


Dkt. Bitanyi amesema kuwa ili kusogeza huduma karibu kwa wafugaji, vituo hivyo vya uchunguzi wa Magonjwa ya Mifugo vipo pia katika mikoa ya Arusha, Dodoma, Iringa, Mtwara, Mwanza, Sumbawanga, Tabora na Kliniki ya Mifugo na Maabara meatu-Simiyu.


Vile Vile Mtendaji Mkuu wa TVLA, amesema kuwa taasisi yake inakumbana na changamoto kadhaa, baadhi ni pamoja na Uvamizi wa wananchi katika mashamba yanayomilikiwa na wakala hiyo, inayotoka na kupanuka kwa Miji na kutopatikana kwa hati miliki kwa baadhi ya Maeneo. Pia Mwamko mdogo wa matumizi ya Chanjo na Huduma za Maabara.


Aidha, Changamoto nyingine ametaja kuwa mtaji mdogo usioweza kuruhusu Uwekezaji Mkubwa katika Kiwanda cha Uzalishaji chanjo hasa katika kununua Mitambo na Mashine za kisasa kwa ajili kuzalisha chanjo.


Katibu Mkuu mifugo, pia alipata fursa ya kutembelea kiwanda cha kuzalisha Chanjo kibaha (TVI) na kujionea jinsi chanjo za mifugo zinavyotengenezwa.


Pia, Nzunda aliipongeza taasisi ya TVLA kwa kazi nzuri wanayofanya na kuwataka wanasayansi hao kuongeza umahili na Weledi katika kazi zao na kuzingatia Uadilifu.

Post a Comment

0 Comments