***************
Na John Mapepele
Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Dkt, Hassan Abbasi amesema Utamaduni ni uchumi hivyo vijana wa Tanzania wanatakiwa kuchukua maendeleo chanya ya utamaduni ili waweze kunufaika na kuinua maisha yao na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Dkt. Abbasi ameyasema hayo leo Januari 20, 2022 kwenye Vyombo vya Habari wakati alipokuwa akikagua maandalizi ya Tamasha la Utamaduni la Mkoa wa Kilimanjaro kwenye Uwanja wa Chuo cha Ushirika Moshi, tamasha ambalo litakalofanyika Januari 22,2022 mjini hapo ambalo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi
“Hivi sasa matamasha ya utamaduni katika nchi mbalimbali duniani kama lile la Reo nchini Brazil yanaingiza fedha nyingi na kuinua uchumi wa nchi zao na sisi tumeanza tunataka kutumia utamaduni kuinua uchumi wa wananchi na nchi yetu” amesisitiza Dkt. Abbasi
Amesema Tamasha la Utamaduni la Mkoa wa Kilimanjaro linaasisi matamasha mengine ambayo yatafanyika kwenye kila mkoa hapa nchi.
“Tamasha hili linakwenda kuasisi matamasha mengine lakini ndiyo njia ya kwendea kwenye tamasha kubwa kuliko yaliyowahi kufanyika nchini ambalo litajumuisha mikoa yote ambalo tumepanga lifanyike Mei mwaka huu litakalohusisha mikoa yote ya Tanzania, na litaonesha urithi wa tamaduni mbalimbali chanya. Tutarajie makubwa!”. Amefafanua Dk. Abbasi
Amewataka vijana kuchangamkia fursa za utamaduni na kuondokana na mawazo kuwa utamaduni ni ukale na badala yake kuuenzi na kujivunia huku wakitumia utamaduni kujipatia ajira na kuboresha maisha yao.
Ametoa wito kwa wananchi wote kujitokeza kushiriki kwenye tamasha la mkoa wa Kilimanjaro ambalo hilo ambapo amesema milango wa chuo cha Ushirika Moshi ambapo tamasha hilo litafanyika itakuwa wazi kuanzia saa 12 asubuhi.
0 Comments