Ticker

6/recent/ticker-posts

ANWANI ZA MAKAZI KUIBADILISHA TANZANIA KUWA YA KIDIJITALI


Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi kwenye picha ya pamoja na Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Bi. Mariam Mtunguja wakijifunza namna ya kupata postikodi ya kata mbalimbali nchini kwa kutumia simu ya mkononi wakati wa semina ya kuwajengea uwezo viongozi wa Mkoa wa Morogoro kuhusu mfumo wa anwani za Makazi na Postikodi iliyofunguliwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mkoani hapo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa semina ya kuwajengea uwezo viongozi wa Mkoa wa Morogoro kuhusu mfumo wa anwani za Makazi na Postikodi katika ukumbi wa mikutano wa Mbaraka Mwinshee leo Januari 19, 2022.


Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Bi. Mariam Mtunguja, akitoa salamu za Mkoa kabla ya kumkaribisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi (hayupo pichani) kwa ajili ya kufungua semina ya kuwajengea uwezo wataalam wa Mkoa huo kuhusu mfumo wa anwani za makazi na postikodi iliyofanyika kwenye ukumbi wa Mbaraka Mwinshee leo Januari 19, 2022.


Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Clarence Ichwekeleza akitoa taarifa kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi kabla ya ufunguzi rasmi wa semina ya kuwajengea uwezo viongozi wa Mkoa wa Morogoro kuhusu mfumo wa anwani za makazi na postikodi uliofanywa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo (hayupo pichani) katika ukumbi wa mikutano wa Mbaraka Mwinshee wa Mkoani humo.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi (kushoto) akiongea na Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Bi. Mariam Mtunguja, baada ya kuwasili ofisini kwake mkoani humo kwa ajili ya kufungua semina ya kuwajengea uwezo viongozi wa Mkoa huo kuhusu mfumo wa anwani za makazi na postikodi iliyofanyika kwenye ukumbi wa Mbaraka Mwinshee leo Januari 19, 2022.

*************************
Anwani za Makazi kuwa Msingi wa Utambuzi wa Kila Mwananchi

Na Prisca Ulomi, WHMTH, Morogoro

Serikali imejikita kutekeleza mfumo wa Anwani za Makazi na Postikodi nchi nzima kwa lengo la kuibadilisha Tanzania kuwa ya kidijitali kwa kuwa anwani za makazi na postikodi ni msingi wa utambuzi wa kila mwananchi

Hayo yameelezwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ambaye amewakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi wakati akifungua mafunzo ya kujenga uelewa kwa viongozi, watendaji na wataalam wa Mkoa wa Morogoro kuhusu mfumo wa anwani za makazi na postikodi

Dkt. Yonazi amesema kuwa anwani za makazi na postikodi ni msingi wa utambuzi ili kila mwananchi aweze kutambuliwa pale alipo ambapo nia ya Serikali ni kuihakikisha kuwa kila mtaa, barabara, inakuwa na jina la mtaa na kila nyumba inakuwa na namba ya nyumba

Vile vile, ameitaka Sekretarieti ya Mkoa wa Morogoro kusimamia utekelezaji wa mfumo huu ili ifikapo Mwezi Mei mwaka huu jambo hili liwe limekamilika kwa kuwa utekelezaji wa mfumo huu utaiwezesha Serikali kuwa na sensa bora ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti mwaka huu

Ameongeza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu inayoratibu jambo hili, imeelekeza taasisi zote za Serikali nchi nzima zinatekeleza mfumo huu wamiliki wote wa majengo na nyumba nao waweke namba za nyumba kwenye nyumba na majengo yao na wataalam wote waliojengewa uwezo watumike vizuri kutekeleza mfumo wa anwani za makazi na postikodi na jambo hili liwe ajenda kwenye vikao

Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Bi. Mariam Mtunguja akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Martine Shigela amesema kuwa kimsingi tumechelewa kutekeleza mfumo huu wa anwani za makazi, ila kwa kuwa viongozi mtajengewa uelewa, ni matumaini yangu kuwa kwa pamoja tutashirikiana na wataalam wetu kutekeleza jambo hili kwenye maeneo yetu ndani ya muda uliopangwa na niahidi kuwa Mkoa wa Morogoro hatutawaangusha Wizara

Naye Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Clarence Ichwekeleza, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Jim Yonazi, amesema kuwa mfumo wa anwani za makazi na postikodi ni moja ya aina ya mawasiliano kama zilivyo aina nyingine za mawasiliano na mfumo huu unahusisha eneo husika ambapo utamuwezesha mwananchi kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine; utarahisisha shughuli za kiuchumi, kijamii na utawala

Wakitoa salamu za shukrani kwa niaba ya viongozi wengine, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Morogoro Mjini Fikiri Juma, amesema kuwa viongozi watoe majina ya mitaa ndani ya siku moja ili kufanikisha utekelezaji na Mstahiki Meya wa Manispaa ya Morogoro, Pascal Kihanga amesema watahamasisha wananchi kununua vibao vya nyumba ili kufaniisha uwekaji wa mfumo wa anwani za makazi kwenye Mkoa huo

Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Post a Comment

0 Comments