Afisa Usajili kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Yusuph Mwakasyafuka akitoa mafunzo leo kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Waislamu Morogoro (MUM) huduma zinazotolewa na taasisi hiyo na jinsi ya kuzipata kwa njia ya mtandao.
Mafunzo yakiendelea.
Mafunzo yakiendelea.
***************
Na Mwandishi Wetu, Morogoro
WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) leo Januari 16, 2022 imewapa mafunzo wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro (MUM) jinsi ya kuingia katika ujasiriamali kabla au mara baada ya kumaliza masomo yao.
Akizungumza katika Warsha hiyo, Afisa Usajili kutoka BRELA, Bw. Yusuph Mwakasyafuka ameeleza kuwa urasimishaji wa biashara ni hatua ya kwanza na muhimu sana katika uanzishaji na uendelezaji wa biashara hatua ambayo ikirukwa inaweza kusababisha kuyumba au kuanguka kwa biashara badaye.
“Watu wengi wanafanya makosa wakati wa uanzishwaji wa biashara, mathalani kuanzisha na kutangaza biashara ambayo haijasajiliwa ni kinyume na taratibu kwa sababu kwa kufanya hivyo unaweza kuwa unavunja sheria kwa kutumia jina la mtu mwingine bila kujua au mtu mwingine anaweza kulisajili jina hilo na kulifanya lake kisheria” amesema Bw. Mwakasafyuka.
Aidha Bw. Mwakasafyuka amewatoa hofu kuhusu gharama za usajili wa kampuni na kueleza kuwa mtu anaweza kusajili kampuni akiwa na mtaji wa kuanzia shilingi za kitanzania elfu ishirini (20,000) na kuendelea na ada za usajili zimegawanyika katika makundi mbalimbali kulingana na mtaji husika.
“Ada za usajili wa kampuni sio kubwa kama watu wengi wanavyodhani na hii ni kwa sababu zimegawanywa kulingana na kiasi cha mtaji mfano kama mtu ana mtaji wa kuanzia shilingi za kitanzania 20,000 hadi 1,000,000 atapaswa kulipa ada ya usajili ya 167,200” ameeleza Bw. Mwakasafyuka.
Kwa upande mwingine pia kuna fursa ya kurasimisha biashara kwa wajasiriamali ambao hawajafikia hatua ya kufungua kampuni, hivyo wao wanaweza kusajili jina la biashara kama hatua ya kuanzia ambapo ada ya usajili ni shilingi ya kitanzania 20,000 pekee.
Kwa upande wa Alama za Biashara na Huduma ambazo hufahamika zaidi kama (logo) hizi mtu anaweza kukamilisha usajili wake kwa shilingi za kitanzania 125,000.
Usajili wa alama hizi una faida lukuki katika soko la ushindani wa kibiashara kwa sababu unasidia kuitangaza bidhaa husika na kuifanya ifahamike kwa wateja kama ni bidhaa na kama ni huduma kusaidia wale wanaohitaji waweze kuifikia kwa urahisi pale inapohitajika.
Naye Bi. Mariam Swalehe Said, Mkuu wa Idara ya Uhasibu katika chuo hicho ameipongeza BRELA kwa juhudi zake za kutoa elimu kwa umma na uhamasishaji wa urasimishaji wa biashara kwa sababu ni muhimu sana kwa vijana ambao wameanza masomo na wanaoelekea kumaliza masomo.
“Elimu hii itawafungulia njia mpya wanafunzi wa chuo, badala ya kusoma masomo darasani pakee sasa wanapata fursa ya kufahamu pia upande wa pili wa kuna vitu gani wanapaswa kufanya, nawashukuru sana BRELA kwa elimu hii” alisema Bi. Mariam.
Katika urasimishaji wa biashara BRELA imepewa majukumu kwa mujibu wa sheria kusajili Kampuni, Majina ya Biashara, Alama za Biashara na Huduma, Utoaji wa Leseni za biashara kundi A, Leseni na Viwanda na Hataza.
Huduma zote hizi zinatolewa kwa njia ya mtandao ambapo mhitaji anatakiwa kuwa na namba ya utambulisho wa taifa (NIDA), anuani ya barua pepe, namba ya simu ya mkononi inayofanya kazi na baada ya hapo atatakiwa kutembelea www.brela.com ili kuweza kufanya sajili.
0 Comments