Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu, akishiriki ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kata Ilunda kilichopo wilayani Mkalama mkoani Singida kwa kuchanganya mchanga wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo aliyoifanya leo wilayani humo. Kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma za Afya TAMISEMI, Dkt. Ntuli Kapologwe.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu, akikagua darasa la Uviko-19 la Shule ya Sekondari ya Gumanga.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge, akizungumza katika ziara hiyo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Sophia Kizigo na Mbunge wa Iramba Mashariki, Francis Isack.
Mkurugenzi wa Sera na Mipango TAMISEMI, John Cheyo, akiteta jambo na Waziri Ummy wakati wa ziara hiyo.
Mkurugenzi wa Kikundi cha Vijana cha Iguguno Youth Group kinachojishughulisha na ufyatuaji wa matofali na ufugaji wa kuku wa kienyeji Vicky Mwaisakila akitoa taarifa ya kikundi hicho kwa Waziri Ummy.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Vijana wa Kikundi cha Iguguno Youth Group na baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Singida.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijiji wa Wilaya ya Mkalama, Edward Masola akitoa taarifa ya ujenzi wa miradi ya barabara wilayani humo.
Mbunge wa Iramba Mashariki, Francis Isack akimuelekeza jambo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu.
Diwani wa Kata ya Ilunda, Mohamed Imbele, akizungumza kwenye ziara hiyo.
Ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Ilunda ukiendelea.
Wananchi wa Kata ya Ilunda wakiwa kwenye mkutano eneo kinapojengwa kituo cha afya ambapo walipata fursa ya kuzungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Ummy Mwalimu.
Mkazi wa Kata ya Ilunda, Oscar Daudi akitoa shukurani kwa Serikali kwa kutoa fedha za ujenzi wa kituo hicho cha afya.
Mkazi wa Kata ya Ilunda Josephina Maige akizungumzia adha wanayoipata kwa kukosa kituo cha afya katika kata hiyo.
Mkazi wa Kata ya Ilunda, Hawa Gimbi akizungumzia furaha yake kwa Serikali kuanza kujenga kituo hicho cha afya kwani aliwahi kunususika kufariki alipokuwa mjamzito wakati akipelekwa hospitali kujifungua.
Mkazi wa Kata hiyo Omari Mkali akizungumzia umuhimu wa kituo hicho cha afya kwa wananchi wa eneo hilo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Asia Messos (kulia) akizungumzia kuhusu ujenzi wa Zahanati ya Kisuluiga iliyopo Kata ya Gumanga ambapo Waziri Ummy ameagiza Halmashauri hiyo itoe Sh.60 milioni ili kukamilisha ujenzi wake.
*********************
Na Dotto Mwaibale, Mkalama
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Ummy Mwalimu amewataka Wananchi wa Wilaya ya Mkalama mkoani Singida kuzitunza barabara zilizojengwa na Serikali kwa gharama kubwa.
Ummy ametoa ombi hilo wakati akizungumza na wananchi hao wakati akikagua barabara ya Singa- Kinampundu-Ilunda iliyojengwa kwa kiwango cha changarawe katika ziara ya kikazi ya siku moja wilayani humo ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.
"Jambo lililokubwa nawaomba wananchi mzitunze hizi barabara kwa sababu Serikali inazichonga lakini kunawananchi wanapitisha majembe ya kukokotwa na ng'ombe kwa hiyo niombe ulinzi wa barabara uwe ni jukumu letu sote kwa sababu fedha zilizotumika kuzitengeneza ni nyingi hivyo tunatamani ziendelee kuwa na ubora na zisaidie kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi" alisema Waziri Ummy.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara hiyo Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijiji wa Wilaya ya Mkalama, Edward Masola alisema matengenezo ya barabara hiyo yatagharimu kiasi cha Sh.milioni 91,201,000.
Alisema barabara hiyo ambayo inaunganisha Kata za Ilunda na Kinampundu itakapokamilika itarahisisha usafiri kwa wananchi kufikia huduma za elimu, afya na masoko.
Katika hatua nyingine Waziri Ummy amemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida kusaini mikataba yote ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kata ya Ilunda baada ya kuwepo madai ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo kugoma kuisaini kufuatia mgororo wa kugombea sehemu ya kujengwa kituo hicho ambapo baadhi ya madiwani walitaka kijengwe Gumanga.
Awali akitoa taarifa ya kituo hicho cha afya, Mganga Mkuu wa wilaya hiyo, Ibrahim Pazia alisema fedha za ujenzi wa kituo hicho ni Sh.250,000,000 zilizotokana na tozo na kuwa kitakuwa na majengo matatu jengo la wagonjwa wa nje (OPD) jengo la maabara na kiteketeza taka.
Alisema mradi huo utakapo kamilika utahudumia wananchi 12,000 wa vijiji vya Asanja, Nkungi, Ilunda na Iambi, Kinambili, Nduguti na vijiji jirani vya Mkunguru, Kidigida na Kata ya Kinampundu.
Waziri Ummy alitumia nafasi hiyo kuwaomba waheshimiwa madiwani kuacha mivutano ambayo haina tija ambayo inakwamisha maendeleo ya wananchi kama ilivyotokea katika kata hiyo.
Katika ziara hiyo Waziri Ummy alitembelea na kukagua kikundi cha Vijana cha Iguguno Youth Group kinachojishughulisha na ufyatuaji wa matofali na ufugaji wa kuku wa kienyeji ambapo aliwaunga mkono kwa kuwachangia Sh.2,000,0000 ambapo pia Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge aliwachangia kiasi hicho cha fedha.
Aidha Waziri Ummy alitembelea na kukagua darasa moja la Uviko-19 kati ya saba la Shule ya Sekondari ya Gumanga ambayo yamejengwa kwa Sh.140,000,000.
0 Comments