Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MULAMULA AIPONGEZA FINLAND KWA KURIDHIA MKAKATI MPYA WA USHIRIKIANO NA TANZANIA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula ameipongeza Serikali ya Finland kwa kuridhia Mkakati Mpya wa ushirikiano kati yake na Tanzania kuanzia mwaka 2021 hadi 2025 ikiwa ni pamoja na mchango wa nchi hiyo kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.

Pongezi hizo zimetolewa na Mhe. Waziri Mulamula alipozungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 104 ya uhuru wa Taifa la Finland yaliyofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 06 Desemba 2021 na kuhudhuriwa na wageni waalikwa mbalimbali wakiwemo Mabalozi na Wakauu wa Mashirika ya Kimataifa waliopo nchini.

Balozi Mulamula amesema kuwa, kuridhiwa kwa mkakati huo mpya wa ushirikiano kati ya Tanzania na Finland kunadhihiridha jinsi ambavyo nchi hiyo imedhamiria kuendelea kushrikiana na Tanzania ili kuiwezesha kukamilisha agenda na miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa hapa nchini kwa ushirikiano na nchi hiyo.

“Tanzania inatoa shukrani kwa Serikali ya Finland kwa kuridhia Mkakati Mpya wa Ushirikiano na Tanzania kuanzia mwaka 2021 hadi 2025. Kuridhiwa kwa Mkakati huu kunadhihirisha namna ambavyo Serikali ya Finland ipo tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania ili kuwezesha utekelezaji wa agenda za maendeleo zilizopo” amesema Waziri Mulamula.

Balozi Mulamula amesema kwamba, katika kipindi cha miaka 56 ya ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Finland, nchi hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya nchi hii kwa kuchangia miradi ya maendeleo kwenye sekta mbalimbali zikiwemo elimu, utunzaji wa mazingira na misitu, nishati, TEHAMA na program za kuwawezesha wanawake kiuchumi.

Ameongeza kusema kuwa, miongoni mwa masuala muhimu ya kupigiwa mfano kwenye ushirikiano huu ni pamoja na nchi hiyo kuwezesha kuanzishwa kwa Mpango wa Kuboresha ukusanyaji Kodi ambao kwa kiasi kikubwa umechangia kuongezeka kwa ukusanyaji mapato ya ndani hapa nchini. Pia, Finland kupitia Mchakato wa Helsinki kuhusu masuala ya utandawazi na demokrasia, uliwezesha kuanzishwa kwa Taasisi ya Uongozi (Uongozi Institute) ambayo hutoa mafunzo kwa viongozi waaandamizi serikalini na wadau mbalimbali katika kuwajengea uwezo wa utendaji kazi zao za kila siku.

Katika kuwawezesha wanawake kiuchumi, Balozi Mulamula amesema, Serikali ya Finland kupitia ubalozi wake hapa nchini umeanzisha program mbalimbali za kuwawezesha wanawake kujikwamua kiuchumi ikiwemo ile ya “Wanawake Wanaweza”.

Kwa upande wake, Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Riitta Swan amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na Serikali kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo na kuipongeza Tanzania Bara inapoelekea kusherehekea miaka 60 ya uhuru.

Tanzania na Finland zilianzisha rasmi ushirikiano wa kidiplomasia mwaka 1965.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula akizungumza kama mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya miaka 104 ya uhuru wa Taifa la Finland yaliyofanyika tarehe 06 Desemba 2021 jijini Dar es Salaam. Maadhimisho hayo ambayo yaliandaliwa na Balozi wa Finland hapa nchini, Mhe. Riita Swan, yalihudhuriwa pia na Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa waliopo nchini.

Sehemu ya Mabalozi na wageni waalikwa wakimsikiliza Mhe. Balozi Mulamula (hayupo pichani) akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 104 ya uhuru wa Taifa la Finland. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Swahiba Mndeme.


Balozi wa Finland nchini, Mhe. Riitta Swan akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 104 ya uhuru wa Finland.


Sehemu ya Mabalozi na wageni waalikwa wakimsikiliza Mhe. Baloz Swan (hayupo) pichani.


Mhe. Balozi Mulamula na Mhe. Balozi Swan pamoja na wageni waalikwa wakiwa wametulia wakati nyimbo za Taifa la Finland na Tanzania zikiimbwa kuadhimisha miaka 104 ya uhuru wa Taifa la Finland.






Maafisa kutoka Ubalozi wa Finland wakiimba wimbo kwa Lugha ya Kifini kuwaburudisha wageni waalikwa wakati wa maadhimisho ya miaka 104 ya Taifa la Finland

Mhe. Waziri Mulamula akiwa ameongozana na mume wake, Dkt. George Mulamula wakipokelewa na Balozi wa Finland nchini, Mhe. Riitta Swan pamoja na mume wake walipowasili Ubalozi wa Finland kwa ajili ya kushiriki maadhimisho ya miaka 104 ya Finland.


Post a Comment

0 Comments