Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akizungumza na Wathamini kwenye mkutano Mkuu wa pili wa Wathamini uliofanyika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre Jijini Dodoma leo tarehe 7 Desemba 2021
Sehemu ya washiriki wa Mkutano Mkuu wa Pili wa Wathamini uliofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma tarehe 7 Desemba 2021.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe William Lukuvi akimkabidhi cheti cha shukurani Mthamini Mkuu wa Ofisi ya Mthamini wa Serikali Adam Nyaruhuma wakati wa mkutano Mkuu wa pili wa Wathamini uliofanyika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre Jijini Dodoma leo tarehe 7 Desemba 2021 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wathamini wakati wa mkutano Mkuu wa pili wa Wathamini uliofanyika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre Jijini Dodoma leo tarehe 7 Desemba 2021 (PICHA NA MAGRETH LYIMO WIZARA YA ARDHI)
***********************
Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi ameitaka Bodi ya Usajili Wathamini nchini kuchukua hatua kali kwa Wathamini wote wasiokuwa waadilifu bila kujali kama wapo serikalini au wanafanya kazi sekta binafsi
Aidha, ameitaka Bodi hiyo kujipanga kuwashughulikia Wathamani wanaofanya kazi ya uthamini bila kuwa na taaluma husika wala kusajiliwa au kuwa na leseni. Aliitaka Bodi hiyo kujipanga kuwashughulikia kikamilifu watu hao ili kulinda taaluma ya uthamini na lawama zisizo na msingi.
Lukuvi alitoa kauli hiyo leo tarehe 7 Desemba 2021 wakati akifungua mkutano mkuu wa pili wa mwaka wa Wathamini uliofanyika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre jijini Dodoma
Alisema, baadhi ya changamoto zilizopo kwenye fani hiyo ya uthamini zinatokana na kukosekana uadilifu kwa baadhi ya Wathamini kwa kuwa baadhi yao hushirikiana na waguswa miradi mbalimbali ya utwaaji ardhi, ili walipwe fidia kubwa wasiyostahili.
Huku akitoa mifano jinsi alivyoweza kudhibiti udanganyifu wa uthamini kwa wananchi walioathirikia na milipuko ya mabomu katika mkoa wa Dar es Salaam wakati akiwa Mkuu wa mkoa huo Lukuvi alisema udanganyifu unaofanywa na wathamini wakati mwingine umekuwa ukiingizia hasara kubwa serikali.
‘’Baadhi ya wathamini hufanya udanganyifu kwa kushirikiana na waguswa wa miradi kwa kufanya udanganyifu katika uthamini na mara nyingi wamekuwa wakishirikiana na waguswa wa miradi mbalimbali ya utwaaji ardhi kwa ajili ya kujinufaisha’’ alisema Lukuvi.
Kwa mujibu wa Lukuvi pia baadhi ya maafisa wa taasisi za fedha zinazotoa mikopo kama mabenki nao hushirikiana na wathamini wasio waaminifu katika kudanganya thamani ya mali za wateja wao kwa madhumuni ya kukopesha fedha nyingi zaidi ya thamani ya mali zilizowekwa rehani au katika kuongeza au kupunguza thamani tofauti na uhalisia ili kutoa unafuu kwa upande unaonufaisha afisa wa benki husika na mthamini.
‘’Wakati mwingine wathamini wasio na maadili hudiriki kuweka au kuorodhesha mali ambayo hata haipo uwandani au kuondoa mali iliyopo uwandani katika taarifa ili kukidhi matakwa ya mteja wake na kuongeza kuwa vitendo vya aina hiyo vinaichafua taaluma hii’’ alisema Lukuvi
Akizungumzia uthamini kwenye maeneo yanayotwalia kwa shughuli za maendeleo, Waziri Lukuvi alieleza kuwa, wathamini wanatakiwa kujiridhisha kwanza kuwa mhitaji ardhi kama anao uwezo wa kulipa fidia na kuwa taratibu za kisheria za utwaaji ardhi zimekamilika kabla ya kuanza zoezi la uthamini.
Lukuvi alisema Waraka Na 1 wa mwaka 2006 ulielekeza taratibu zozote za utwaaji ardhi ya wananchi sizianze kutekelezwa mpaka mamlaka inayohitaji ardhi hiyo idhibitishe uwezo wake wa kulipa fidia kwa wakati na kubainisha kuwa hiyo ina maana Mthamini anapaswa kijiridhisha kama mhitaji ardhi anao uwezo wa kulipa fidia na kuwa taratibu za kisheria za utwaaji ardhi zimekamilika kabla ya kuanza zoezi la uthamini.
Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wathamini Dkt. Cletus Eligius Ndjovu kwa upande wake alitoa onyo kwa wathamini kwa kuwaeleza kuwa, bodi hiyo haiko tayari kufanya kazi na Wathamini watakaofanya kazi nje ya utaratibu na kusisistiza kuwa bodi hiyo itaendelea kuchukua hatua kali kwa watahamini wote watakaoenda kinyume na maadili ya taaluma ya uthamini.
0 Comments