Ticker

6/recent/ticker-posts

WANUFAIKA WA MIRADI INAYOFADHILIWA NA MAMLAKA YA ELIMU TANZANIA (TEA) WAHIMIZWA KUSHIRIKISHA WANANCHI


Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Prof. Maurice Mbago (aliyesimama) akizungumza na watendaji wa Manispaa ya Sumbawanga (hawako pichani) ikiwa ni sehemu ya ziara ya kutembelea miradi inayofadhiliwa na TEA. Wengine ni Mjumbe wa Bodi, Atupele Mwambene (kulia) na Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Bahati Geuzye

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Prof. Maurice Mbago (wa pili kulia) na Mjumbe wa Bodi ya TEA Atupele Mwambene (wa kwanza kulia) wakiwa katika moja ya madarasa matatu yaliyojengwa kwa ufadhili wa TEA, katika Shule ya Msingi Haloli iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe.
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Prof. Maurice Mbago (wanne kulia) na Mjumbe wa Bodi ya TEA, Atupele Mwambene (wa tatu kushoto) baada ya kutembelea nyumba za walimu zilizojengwa katika Shule ya Sekondari Kasanga iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo, mkoani Rukwa
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Prof. Maurice Mbago akishiriki ukaguzi wa ujenzi wa bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari Kichema iliyopo Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa.


*********

Bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imehimiza shule zinazonufaika na miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Elimu Nchini, unaoratibiwa na TEA kushirikisha wananchi wa maeneo husika katika hatua zote za utekelezaji wa miradi ili kuwa na utekelezaji wenye ufanisi.


Ushauri huo umetolewa kwa pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya TEA, Prof. Maurice Mbago na Mjumbe wa Bodi, Atupele Mwambene wakati wa ziara yao ya kutembelea miradi ya miundombinu ya elimu inayofadhiliwa na Mfuko wa Elimu katika mikoa ya Rukwa na Songwe.


Wamesema wananchi wanapopata taarifa za utekelezaji wa miradi kupitia Kamati na Bodi za Shule, wawakilishi wao pamoja na viongozi wa Serikali za mitaa na vijiji wanakuwa tayari kushiriki kwa kuchangia nguvukazi hivyo kuleta ufanisi katika utekelezaji na utunzaji wa miradi.


Miradi iliyotembelewa mkoani Rukwa ni ujenzi wa Bweni la wasichana katika Shule ya Sekondari ya Kichema iliyopo Manispaa ya Sumbawanga uliofadhiliwa kwa Shilingi Milioni 75, ujenzi wa nyumba 4 za walimu katika Shule ya Msingi Muzi unaofadhiliwa kwa Shilingi Milioni 100 na nyumba za walimu zinazotumiwa na familia sita (Six in one) katika Shule ya Sekondari Kasanga uliogharimu Shilingi Milioni 145. Miradi hiyo miwili ipo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo.


Katika mkoa wa Songwe wametembelea mradi wa ujenzi wa madarasa matatu katika Shule ya Msingi Haloli iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, uliogharimu Shilingi Milioni 60.


Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ni Taasisi ya Umma inayofanya kazi chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. TEA inaratibu Mfuko wa Elimu wa Taifa wenye jukumu la kuboresha miundombinu ya elimu ili kuhakikisha upatikanaji wa elimu bora kwa usawa nchini kote

Post a Comment

0 Comments