Na Mwandishi wetu – Arusha
Wakulima katika skimu za kilimo cha umwagiliaji Mkoani Arusha, wamepewa elimu kuhusiana na namna ya kusajili vyama vya umwagiliaji na utoaji wa ada na tozo na kupewa utaratibu wa kulipia ada hizo zitakazosaidia kuboresha na kurekebisha miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji pale itakapokumbwa na madhara yatokananyo na athari za mabadiliko ya tabianchi au uchakavu.
Bi Fatuma Mwera Afisa Kilimo kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji akizungumza na baadhi ya viongozi wa skimu za kilimo cha umwagiliaji katika Halmashauri ya Arusha katika kata ya Ilikiding’a alibainisha kuwa, usajili wa vyama vya umwagiliaji utasaidia skimu kutambulika na kupata fursa zinazojitokeza ikiwa ni pamoja na kupelekewa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji.
Aidha aliwaasa viongozi hao kuwa vinara katika swala zima la usimamizi na utunzaji wa mazingira hususan vyanzo vya maji ikiwa ni pamoja na kutokufanya shughuli za kibinadamu katika vyanzo hivyo.
Aliendelea kusema kuwa, skimu zote za kilimo cha umwagiliaji zitafanyiwa maboresho kwa awamu lakini , skimu ambazo zimesajiliwa ndizo zitakazopewa kipaombele kwanza wakati wa maboresho hayo. “ Ni vizuri kusajili wote kwa pamoja ili tupange mipango ya kazi kirahisi na kuzifikia skimu kwa awamu, Alisisitiza.”
Picha ikionesha wataalam kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika kikao cha pamoja na Afisa Kilimo Umwagiliaji na Ushirika wa Wilaya ya Arusha,hayupo pichani wakijadili kwa pamoja maswala ya tozo za Umwagiliaji.
Bi. Fatuma Mwera,Afisa Kilimo toka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji akiongea na viongozi wa skimu za umwagiliaji katika wilaya ya Arusha kuhusiana na maswala ya Tozo na Ada za umwagiliaji.
Kulia Kaimu Mkurugenzi wa Mipango toka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Reginald Diyamet na Mhandisi Naomi Mcharo, wakijadili jambo linalohusu Kilimo cha Umwagiliaji kupitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020.
0 Comments