Ticker

6/recent/ticker-posts

"WAJAWAZITO NA WAZAZI WENYE VIASHIRIA VYA KUNDI LA DHARURA FUATENI USHAURI WA WATAALAM”- WAZIRI WA AFYA


Dkt. Dorothy Gwajima, Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto akiongea kwa njia ya Mkutano wa masafa (zoom), juu ya mkakati wa Wizara wa kila siku wa ufuatiliaji na uchambuzi wa taarifa za vifo vya mama na mtoto vilivyotokea ndani ya saa 24.

*************************

Na Atley Kuni, WAMJW, DSM.

Serikali imewakumbusha wakina mama wajawazito wanaotazamia kujifungua walio kwenye kundi la wenye vidokezo vya hatari kuepuka kujifungulia kwenye vituo vidogo ambavyo havina uwezo wa kutoa msaada wakati wa kujifungua hususan kuongeza damu na upasuaji wa dharura.

Maelekezo haya yanafuatia mkakati wa Wizara, kila siku wa ufuatiliaji na uchambuzi wa taarifa za vifo vilivyotokea ndani ya saa 24 ambapo, imebainika kuwa baadhi ya mambo yanayosababisha ni pamoja na baadhi ya wazazi walio kwenye kundi la wenye vidokezo hatarishi kuamua kujifungulia nyumbani au kwenye vituo visivyo na uwezo wa kuhimili changamoto za dharura ambazo hujitokeza mara nyingi zaidi kwenye kundi hili.

Akiongea na wataalam wa vituo vya huduma za afya nchini kupitia mkutano wa kila siku asubuhi kwa njia ya mtandao wa masafa (zoom) kutokea jijini Dar es Salaam kwenye Ofisi ndogo za Wizara, Dkt. Gwajima (Mb) amesema, tangu kuanza kwa mikutano hiyo tarehe 20 Disemba, 2021, wamebaini baadhi ya wazazi watarajiwa wamekuwa wagumu kufuata maelekezo ya kwenda kujifungua kwenye vituo vikubwa vyenye uwezo wa kutoa msaada wakati wa dharura kulingana na hali zao kiafya. Na kuongeza kuwa, baadhi ya wataalamu wamekuwa wakishindwa kuwaelimisha wazazi hao ili waridhie kufuata maelekezo, hivyo kutoa fursa ya changamoto kuibuka na kupoteza muda wa kuokoa maisha ya mama na mtoto.



“Mama mwenye ujauzito wa kwanza ama wale wenye mimba ya tano na kuendelea au mwenye kidokezo chochote kingine cha hatari, mwongozo wa Wizara ni kuwataka wakajifungulie kwenye vituo vikubwa vyenye utaalamu wa kutosha na uwezo wa kufanya upasuaji mkubwa au msaada mwingine wowote wa kitaalamu ili kumsadia mama na mtoto, hata hivyo wapo baadhi ya wazazi hawaitikii mwongozo huu na baadhi ya wataalamu hawatumii mbinu za kumsaidia na kuhakikisha mzazi anaeleewa na kuridhia” amesema Dkt. Gwajima.



Dkt. Gwajima ameongezea kusema, “katika juma moja la ufatiliaji juu ya kwa nini vifo vya mama na mtoto bado vinaendelea, pamoja na mambo mengine tumebaini pia kukosekana kwa ushirikiano baina ya wazazi/wajawazito na wataalam wa afya katika kutekeleza mwongozo wa kisera kuhusu huduma kwa wajawazito na wazazi wenye vidokezo vya hatari jambo linalochangia kuibuka kwa changamoto ambazo wakati mwingine kuzidhibiti inakuwa haiwezekani” amesisitiza Dkt. Gwajima.



Waziri Dkt. Gwajima, amemuagiza Katibu Mkuu Afya, kupitia Dkt. Ahmad Makuwani anayeratibu vikao hivyo kuwaandikia na kuwakumbusha wataalam wakuu wa vituo vyote nchini kuendelea kuwaelimisha na kuwahimiza wazazi watarajali wanapofika kliniki kupokea na kufuata elimu ya afya iliyomo kwenye miongozo ya Wizara ili kuwa na uzazi salama.

Sambamba na hilo, ameangiza, wakuu wa vituo vya huduma za afya nchini wahakikishe wanatoa taarifa kwa mganga mkuu wa wilaya au mkoa pale wanapoona mzazi mtarajiwa mwenye vidokezo vya hatari ambaye anastahili kupata huduma kwenye kituo kikubwa zaidi ili kwa pamoja waone namna ya kumsaidia.



Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto ambayo inajukumu la kusimamia suala la uzazi salama kwa mama na Mtoto, imeanzisha utaratibu vikao vya vya kujadili na kujitathmini namna gani wataweza kupunguza au kutokomeza kabisa vifo vya mama na mtoto vitokanavyo na sababu za uzazi kwani Wizara inaamini Uzazi Salama bila Vifo ni suala linalowezekana. Hivyo, wananchi watimize wajibu wao na wataalamu watimize wajibu wao.

Post a Comment

0 Comments