Ticker

6/recent/ticker-posts

'VIONGOZI WA VYAMA VYA USHIRIKA TAFUTENI MASOKO'-DK.NDIEGE


Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akiongea wakati wa Mafunzo ya Masoko na Biashara kwa Viongozi wa Vyama vya Ushirika yaliyoandaliwa na Tume, Jijini Dodoma


Mrajis Msaidizi Robert Nsuza akieleza baadhi ya masuala muhimu ya kuzingatia katika utafutaji wa fursa za masoko wakati wa Mafunzo ya Masoko na Biashara kwa Viongozi wa Vyama vya Ushirika yaliyoandaliwa na Tume, Jijini Dodoma


Mwakilishi wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Victoria Michael akichangia mada wakati wa Mafunzo ya Masoko na Biashara kwa Viongozi wa Vyama vya Ushirika yaliyoandaliwa na Tume, Jijini Dodoma


Bw. Bakari Hussein Kassia Kaimu Meneja Mkuu wa Mradi wa Pamoja wa Vyama vya Vikuu vya Tumbaku (T.C.J.E) akiongea kwa niaba ya Viongozi wa Ushirika waliokuwa wakipata mafunzo ya Masoko na Biashara kwa Viongozi wa Vyama vya Ushirika yaliyoandaliwa na Tume, Jijini Dodoma


Baadhi ya washiriki wakifatilia hotuba ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege (hayupo pichani) wakati wa Mafunzo ya Masoko na Biashara kwa Viongozi wa Vyama vya Ushirika yaliyoandaliwa na Tume, Jijini Dodoma

....................................................................

Na.Alex Sonna,Dodoma

Viongozi wa Vyama vya Ushirika wametakiwa kutafuta masoko ya mazao mbalimbali yanayozalishwa kwenye maeneo yao kwa lengo la kuwawezesha wakulima kupata uhakika wa masoko yenye tija kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Dkt. Benson Ndiege akizungumza wakati wa mafunzo ya Masoko na Biashara kwa viongozi na Watendaji wa Vyama vya Ushirika yaliyoandaliwa na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Novemba 3 Desemba 2021, Jijini Dodoma amewataka Viongozi hao kutafuta fursa za masoko ndani na nje ya nchi.

Dkt. Ndiege amesema Viongozi wa Vyama vya Ushirika wana wajibu wa kuwasaidia wakulima katika kutafuta fursa za masoko ya mazao yao ambapo amesema kuwa kufanya hivyo kutasaidia Wakulima kuendelea kupata bei zenye ushindani. Ameongeza kuwa hivi sasa ni wakati kwa viongozi kushirikiana na wadau kuongeza thamani ya mazao kupitia uchakataji na uwekezaji wa viwanda ili kupanua wigo wa masoko.

“Ni wakati sasa kwa viongozi kuhakikisha mnatumia fursa mbalimbali za kujitangaza, kushirikiana na wadau wengine wa ndani na nje ya nchi ili Wakulima wetu wapate masoko ya bidhaa zao na tusiishie kuuza bidhaa ghafi bali tujielekeze kwenye bidhaa zilizoongezwa thamani,” alisema Mrajis

Akiongea katika mafunzo hayo Mrajis amesema mafunzo hayo ya biashara na masoko yanalenga kuwaongezea uwezo viongozi na Maafisa masoko wa Vyama vya Ushirika kupanua wigo wa utafutaji wa masoko ili Wakulima waendelee kunufaika na Ushirika. Hivyo, amesema Tume itaendelea kuhakikisha mafunzo hayo yanakuwa endelevu.

Akichangia mada katika mafunzo hayo mwakilishi wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) Victoria Michael amesema Vyama vya Ushirika vina fursa kubwa ya kuongeza pato la Vyama kwa kufufua viwanda vingi zaidi vitakavyosaidia kuongeza mnyororo wa thamani ya mazao akitolea mfano mazao ya Korosho na Kahawa yanayosafirishwa nje ya nchi. Akiongeza kuwa uongezaji wa thamani Pamoja na ufungashaji mzuri wa bidhaa za mazao unaongeza na kuitangaza nchi Kimataifa.

Kwa upande wake Bw. Bakari Kassia Kaimu Meneja Mkuu wa Mradi wa Pamoja wa Vyama vya Vikuu vya Tumbaku (T.C.J.E) kwa niaba ya washiriki amesema mafunzo hayo yatawawezesha kupanua fursa za masoko kupitia mada ziliangazia mifumo ya masoko ya Ushirika, masoko ya Kimkakati, Kilimo cha Mkataba, mikataba ya mauzo, aina ya minada ya uuzaji wa mazao, namna bora ya kufikia masoko ya nje ya nchi kwa kushirikisha Serikali na Balozi zilizopo katika mataifa mbalimbali.

Mafunzo hayo yalihudhuriwa na Wenyeviti, Mameneja na Maafisa masoko 145 kutoka mikoa mbalimbali, ambao ni watendaji muhimu katika uuzaji wa mazao ya wakulima katika Vyama vya Ushirika.



Post a Comment

0 Comments