************************
UMOJA wa wanawake wa Chama cha Mapinduzi ( UWT) Mkoa wa Njombe umepongeza Rais Samia Suluhu Hassan na Mwenyekiti wa CCM Taifa kwa kuliongoza vyema Taifa hatua ambayo pia imemfanya kupongezwa na viongozi wa mataifa mengine.
Akizungumza na waandishi wa habari Mwenyekiti wa UWT Njombe Scholastika Kevela alisema mbali na hilo, Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa mtekekezaji wa kweli wa Ilani ya Uchaguzi wa mwaka 2020/25, jambo linaloifanya Tanzania kuzidi kupiga hatua kimaendeleo na kuipaisha kiuchumi.
Alisema tangu aingie madarakani kwa mujibu katiba Machi Mwaka huu, Rais Samia pia amekuwa mstari wa mbele katika kujenga diplomasia na mataifa mbalimbali duniani jambo liliongeza hamasa kwa baadhi ya mataifa hayo na hivyo kuamua kuja kuwekeza nchini.
"Katika kipindi hiki ambacho tunakaribia kuuaga mwaka 2021 na kuukaribisha Mwaka 2022, watanzania tunavuka tukiwa vifua mbele kutokana na uongozi wake makini na wenye kujali maslahi ya Taifa, ukweli tukiwa kama viongozi wa UWT Mkoa wa Njombe tunaona anatutendea haki kwa uongozi wake" alisema Kevela
Alisema kama hiyo haitoshi, pongezi alizopokea kutoka kwa viongozi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC), juu ya uongozi wake, zinaonyesha kuwa kiongozi huyo Mwanamke wa kwanza katika nafasi ya Urais anakubalika kila pembe huku akiwataka watanzania kuendelea kumuombea na kumuunga mkono wakati huu anapotekeleza majukumu yake.
"Rais Samia amekuwa kiongozi wa kuonesha dira ya Serikali anayoiongoza kwa kuzingatia uadilifu, utawala wa sheria, haki, usawa, mshikamano na kuimarisha demokrasia na zaidi ameendelea kuijenga nchi kiuchumi na eneo la kimiundombinu akitoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi mipya na miradi iliyokuwepo, huu ndiyo uzalendo" aliongeza
Alisema kwa hatua hizo inaonyesha wazi wazi na kwa vitendo ya kuwa kauli yake ya' Kazi Iendelee' inatekelezeka kweli huku akiwataka viongozi wenzie wa chama na wale waliokabidhiwa dhamana mbalimbali Serikali na watanzania kwa ujumla kumuunga mkono kwa vitendo ili aweze kutimiza adhma yake ya kuwaletea maendeleo watanzania.
Aidha alisema wao kama UWT mkoa wa Njombe wataendelea kuhakikisha wanapiga kazi kwa nguvu na juhudi zote hususani katika utekelezaji waa ilani ya chama hicho na usimamizi wa miradi ya kiuchumi ya chama hicho kwa lengo la kumuunga mkono Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa
Alisema tuzo ya ushindi wa pili katika usimamizi wa miradi ya kiuchumi waliokabidhiwa mwanzoni mwa wiki na Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo katika mkutano wa kawaida wa UWT Jijini Dodoma, ni kielelezo cha vitendo cha mkoa wao kusimamia miradi ya chama hicho.
0 Comments