*******************
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limetumia Maonesho ya Sita ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania yanayofanyika Zanzibar kutoa elimu na kutatua changamoto zinazowakabili wazalishaji, wenye viwanda, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.
Maonesho hayo yaliyoanza Desemba 3, mwaka huu yalifunguliwa juzi na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Othman Masoud, ambapo yameandaliwa na Wizara ya Viwanda Zanzibar kwa kushirikiana na TANTRADE.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho hayo jana, Afisa Mdhibiti Ubora wa TBS, Alphred Mosha, alisema baadhi ya washiriki wa maonesho hayo waliotembelea banda la shirika hilo wamekuwa na changamoto toufati, ambapo wengine hawajui jinsi ya kupata kiwango cha bidhaa zao.
Alisema kama ilivyo kauli mbiu ya maonesho hayo inayosema Tumia Bidhaa za Tanzania, Ijenge Tanzania, wao kama TBS wanawaelimisha washiriki wa maonesho hayo kwamba wanapotumia bidhaa ya Tanzania ambayo imekaguliwa wanakuwa na uhakika zaidi na usalama wa ile bidhaa kuliko anayetumia bidhaa ambayo haijakaguliwa.
Alisema baadhi ya washiriki wa maonesho hayo wanafika kwenye banda la TBS wakiwa changamoto tofauti, wengine wakiwa hawajui jinsi ya kupata viwango vya bidhaa zao, hivyo wanaelimishwa na wakiwa tayari wana uwezo wa kuwapatia viwango vya bidhaa zao.
"Wengine wanakuwa wanazalisha bidhaa, lakini hawajui taratibu za kupata alama ya ubora au utaratibu wa bidhaa zao kukaguliwa na TBS, hivyo tunakuwa tunawaelimisha ni kitu gani kifanyike ili bidhaa zao ziweze kupata alama ya ubora," anasema Mosha.
Alisema miongoni mwa majukumu ya TBS ni kutoa elimu kwa wazalishaji pamoja na wafanyakazi wa sekta na taasisi za viwanda kuhusiana na uzalishaji wa bidhaa bora, uzalishaji salama na udhibiti wa ubora.
"Kwa hiyo katika kutimiza lengo hilo kwenye maonesho haya tunawaelimisha wananchi, wafanyabiashara na wenye viwanda kuhusiana na alama ya ubora. Wanatakiwa kujua kwamba bidhaa zote ambazo zimethibitishwa ubora wake ambazo zinazalishwa nchini na zimethibitishwa ubora wake huwa zinatumia alama ya ubora," alisema Mosha na kuongeza;
Hii alama ya ubora inakuwa na manufaa kwa pande zote mbili, upande wa mzalishaji, mfanyabiashara na kwa mtumiaji."
Alisema kwa upande wa wafanyabiashara au wenye viwanda na wazalishaji, alama ya ubora inawapa nguvu na kujiamini kwamba bidhaa zao zinakidhi viwango vya bidhaa husika katika nchi yetu.
"Lakini pia inampa uhakika wa soko kwamba bidhaa yake imeishakaguliwa , hivyo soko lake linakuwa na wigo mpana zaidi ikilinganishwa na bidhaa ambayo haijakaguliwa," alisema Mosha na kusisitiza;
"Bidhaa ambayo imekaguliwa inakuwa na uwezo kupata masoko hata nje ya nchi, kwani huwa zinapima na kuthibitishwa na mahabara za TBS ambazo zina vyeti vya umahiri vinavyotambuliwa kimataifa.
Kwa hiyo bidhaa zikienda soko la Kenya, Uganda au hata nje ya Afrika zinakuwa zinakuwa zinapenya kwenye soko hayo kirahisi zaidi kuliko bidhaa ambazo hazijakaguliwa."
Kuhusu upande wa watumiaji, alisema alama ya ubora inamfanya awe na uhakika kwamba bidhaa hiyo imekaguliwa na haina madhara kwa matumizi ya bidhaa husika, hivyo inamhakikishia kwamba bidhaa hiyo inakidhi viwango vya kitaifa.
"Kwa hiyo anakuwa na uhakika kwamba hii bidhaa nikiitumia siwezi kupata madhara yoyote," alisema Mosha.
0 Comments