Ticker

6/recent/ticker-posts

SURA MPYA MAJENGO YA SHULE KUKABILI UHABA WA MAENEO



**************

NA JUMA ISSIHAKA

RAIS Samia Suluhu Hassan, ameelekeza kubadilishwa kwa majengo ya shule akitaka yajengwe kwa mtindo wa Ghorofa ili kukabili changamoto ya uhaba wa maeneo.

Amesema kufanya hivyo kutafanikisha matumizi ya maeneo madogo katika utekelezaji wa miradi hiyo na hivyo kuondoa malalamiko ya kushindwa kujenga shule kutokana na eneo kutotosha

Rais Samia aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana, wakati wa ufunguzi wa Barabara mpya ya Bagamoyo kipande cha njia nne cha Morocco - Mwenge chenye urefu wa kilometa 4.3.

Alisema kutokana na sehemu nyingi kukumbwa na changamoto ya maeneo madogo na hivyo kushindwa kujenga shule, ni wakati sahihi wa kubadili aina ya ujenzi.

"Nilikwenda Mkuranga nikakuta changamoto hii, nimekuja Kinondoni kuna hili, nadhani ni wakati muafaka sasa tubadilishe majengo ya shule zetu, badala ya mabanda kuongozana sasa twende juu," alisema.

Alieleza kufanya hivyo kutaondoa changamoto hiyo, kwani ujenzi wa ghorofa hauna ukomo zaidi ya uwezo wa kifedha.

Alisema kwa maeneo madogo yaliyopo ni vyema wakaona namna ya kujenga maghorofa kwa kuwa juu hakuna mipaka zaidi ya uwezo wa kitaalamu na fedha.

"Lakini vinginevyo kuna mipaka tuliyowekewa na wenzetu wa mipango miji, kwahiyo ndugu yangu Tarimba (Mbunge wa Kinondoni) kwa eneo dogo ulilonalo tujipange kwenda juu badala ya kukaa kugombana na kuchelewesha maendeleo," alisema.

Aidha, Rais Samia alikemea vitendo vya baadhi ya wananchi waaotupa taka kuziba mitaro na hivyo kusababisha mafuriko, huku wengine wakizibua vyoo wakati wa mvua.

"Wanafanya hivi bila kujali watoto wetu ni watundu wakati mwingine hawasikii, wanaingia katika mitaro hiyo na kubeba maradhi," alisema.

Alisema wengine huchimba michanga katika maeneo ya miradi na hivyo kupunguza umadhubuti wake.

Rais Samia alisema wapo baadhi ya watu wanaoegesha gari pembeni na kuachia mafuta, jambo ambalo linaharibu barabara na hivyo kuigharimu serikali kukarabati kabla ya muda uliopangwa.

"Kuna tabia nyingi za ajabu ajabu zimekuwa zikifanyika, niwaombe sana ndugu zangu a Dar es Salaam, twende tukatunze moundombinu tunayokenga, naombeni sana tubadilike," alisema.

Kuhusu mradi wa barabara hiyo alisema wazo la utekelezaji wake lilianza wakati a Hayati Dk.John Magufuli, hivyo ni vyema wananchi kuhakikisha wanabeba juhudi zake ili aliyoyatamani yaonekane.

Alieleza serikali inafanya jitihada nyingi katika kujenga miundombinu nchi nzima ili kuleta urahisi wa usafiri na usafirishaji wa watu na mizigo na kuinua uchumi.

Alisema upanuzi na maboresho hayo ya barabara si tu yatapunguza kero ya msongamano bali yatapunguza ajali za barabarani wakati wa kutoka na kuingia katika Jiji la kibiashara la Dar es Salaam.

Post a Comment

0 Comments