Ticker

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YATOA MUONGOZO KWA MADALALI NCHINI

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza katika mkutano na Madalali uliofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 15 Desemba 2021.
Sehemu ya Madalali waliohudhuria mkutano baina yao na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi tarehe 15 Desemba 2021.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza katika mkutano wa Madali uliofanyika jijini Dar es Salaam tareher 15 Desemba 2021.
Mmoja wa Madalali maarufu kama Dalali Msomi akichangia kwenye mkutano wa Madalali uliofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 15 Desemba 2021.

*****************

Na Munir Shemweta, WANMM

Serikali imetoa muongozo wa kusimamia shughuli za udalali nchini kwa lengo la kuwawezesha madalali kufanya kazi zitakazoleta tija kwa serikali na jamii kwa ujumla.

Muongozo huo una madhumuni ya kutambua madalali, shughuli zao, mahali wanapofanyia kazi, utaratibu wa kuratibu na kudhibiti shughuli za udalali pamoja na kulinda maslahi ya wateja, wamiliki, madalali na serikali.

Walengwa wa muongozo huo ni madalali wa nyumba, majengo, viwanja na mashamba, Serikali Kuu na serikali za mitaa, sekta binafsi, wananchi na wadau wote katika shughuli za udalali wa nyumba, majengo, viwanja na mashamba.

Hayo yalibainishwa leo tarehe 15 Desemba 2021 na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alipokutana na wawakilishi wa makampuni ya uuzaji na upangishaji nyumba, viwanja na mashamba pamoja na madalali mmoja mmoja.

Kwa mujibu wa Waziri Lukuvi, muongozo huo unamtaka kila dalali anayepangisha, kuuza kiwanja ama au kupangisha nyumba kusajiliwa na usajili huo utafanyika kuanzia mwezi januari hadi 2022.

Alizitaja sifa na vigezo ambazo madalali watatambulika kupitia muongozo huo kuwa, ni pamoja na kuwa raia wa Tanzania mwenye akili timamu na umri usiopungua miaka 18, anuani au namba ya simu au utambulisho kwa mfumo wa kieletroniki (barua pepe), mahali pa kufanyia kazi panapofahamika, kuwa na namba ya mlipa kodi, kitambulisho cha NIDA, pamoja na kuwa na cheti cha utambulisho kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

"kupitia muongozo huo utambuzi wa madalali utafanywa na idara mpya ya mipango miji na mazingira katika miji na katika halmashauri za wilaya’’ alisema Lukuvi.

Alieleza kuwa, baada ya taratibu kukamilika halmashauri husika itampa mwombaji utambulisho wa kufanya shughuli za udalali wa nyumba/ majengo, viwanja na mashamba na kusisitiza mtu au kampuni yeyote itatakiwa kufuata taratibu ikiwemo kujaza fomu ya maombi ya usajili, kuwasilisha barua ya utambulisho kutoka serikali za mitaa na kulipa ada ya utambulisho shilingi 20,000/-kwa kila mwaka.

Hata hivyo, Waziri Lukuvi alisema kuwa, katika muongozo huo kuna makatazo ambayo dalali hatakiwi kufanya kwenye shughuli zake na kuanisha baadhi ya makatazo hayo kuwa ni pamoja na kufanya kazi bila kutambuliwa na halmashauri, kukwepa kodi, kufanya udanganyifu, kupokea malipo tofauti na malipo yaliyotajwa na kushawishi au kushinikiza mmiliki kutoza au kulipa beo tofauti na makubaliano.

Waziri Lukuvi aliwataka madalali waliohudhuria mkutano huo kufanya kazi kwa maadili kwa kuwa wengi wao wamekuwa wakifanya kazi kwa lengo la kujipatia kipato kikubwa na kudhulumu wananchi huku wakishindwa kuchangia kodi na mapato ya serikali.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula aliwataka madalali kutafakari na kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na serikali na kusisitiza kuwa lengo la serikali ni kuona madalali wanafanya kazi zao bila kubughudhiwa lakini kwa kufuata sheria na taratibu.

‘’Niwaombe madalali mtafakari maelekezo ya serikali maana lengo ni kuona mnafanya kazi zenu bila kubughudhiwa’’ alisema Dkt Mabula

Kwa upande wao Madalali wameishukuru serikali na kuwapatia muongozi ambao sasa unaenda kutambua kazi zao wanazofanya. Hata hivyo, baadhi ya Madalali wameitaka serikali kuweka mfumo rahisi utakaowawezesha kulipa kodi kwa kuwa hivi sasa unapotaka kufanya malipo wanaelezwa baadhi ya taarifa hazipo.

‘’Mhe Waziri hii kazi ya udalali ni ngumu sana na kila mtu kwa hivi sasa ni dalali, aliyestaafu kazi, mwenye nyumba, mtoto wote ni madalali na ninaomba serikali za mitaa kutoa elimu bila ya hivyo itakuwa vurugu ‘’ alisema Salum Chepa.

Post a Comment

0 Comments