Ticker

6/recent/ticker-posts

RC SINGIDA AWAKUMBUKA YATIMA SIKUKUU YA KRISMAS NA MWAKA MPYA

Kaimu Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani (kulia) kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Singida akikabidhi msaada wa vyakula na vitu vingine mbalimbali vilivyotolewa na mkuu wa mkoa huo Dkt.Binilith Mahenge kwa ajili ya zawadi ya Sikukuu ya Krismas na Mwaka mpya kwa watoto Yatima na waishio katika Mazingira magumu wa Kituo cha Amani Centre for Street Children kilichopo mkoani hapa.
Mratibu wa kituo hicho Editruda Kifumo akitoa shukurani kwa mkuu wa mkoa kwa msaada huo.
Watoto wa kituo hicho wakitelemsha vitu mbalimbali vilivyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge.
Watoto hao wakiwa wamebeba msaada huo. Mbuzi aliyetolewa na mkuu wa mkoa kwa ajili ya kitoweo katika sherehe za sikukuu za mwishoni mwa mwaka.
Mtoto Emmanuel Frank akitoa shukurani kwa mkuu wa mkoa kwa msaada huo.
Mtoto Kaishi Gabriel akitoa shukurani kwa msaada huo.
Mtoto Baraka Isaka akishukuru baada ya kupokea msaada huo.
Muonekano wa Kituo cha Amani Centre for Street Children.


**********************

Na Dotto Mwaibale, Singida


MKUU wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge amekabidhi zawadi mbalimbali kwa kituo cha kulelea watoto Yatima na waishio katika mazingira magumu cha Amani Centre for Street Children kilichopo Kata ya Mandewa Manispaa ya Singida.

Zawadi zilizokabidhiwa kwa Yatima na waishio katika Mazingira ni pamoja na mbuzi mmoja, mchele, mafuta ya kupikia,sukari, sabuni, unga na vitu vingine vidogo vidogo.

Kaimu Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa wakati akikabidhi msaada huo alisema mkuu wa mkoa ametoa zawadi hizo ili watoto hao wapate chakula na kufurahia sikukuu za mwishoni mwa mwaka kwa kuwa anaguswa na kutambua uwepo wa watoto Yatima na waishio katika Mazingira magumu waliopo mkoani hapa.

Ndahani alisema kuwa mkuu wa mkoa amesisitiza kuwa lengo la Serikali kuweka Sheria, Kanuni na miongozo mbalimbali inayosimamia vituo hivyo,uanzishwaji na uendeshwaji wake ni kuhakikisha kuwa watoto wanaolelewa katika vituo hivyo wanalelewa kwa kuzingatia utaratibu.

Aidha Ndahani alisema ni muhimu kituo hicho kuwajenga watoto katika misingi ya maadili ya kiroho kusudi watoto hao wakue katika misingi ya kumjua Mwenyezi Mungu na kwamba endapo suala hilo litatiliwa mkazo Taifa litakuwa na hazina ya Raia wenye hofu ya Mungu jambo litakalopunguza na kuondoa kabisa changamoto ya mmomonyoko wa maadili katika Taifa.

Akishukuru kwa niaba ya watoto wenzake mtoto Emmanuel Frank alimshukuu Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Binilith Mahenge kwa msaada huo na akaomba msaada wa namna hiyo usiwe wa mwisho bali uwe endelevu kwani wanapopata wageni wanao watembelea wanafarijika na kujiona kama watoto wengine waliopo na familia zao.

“Tunawashukuru sana kuja kutuona na kutupatia msaada, lakini msiishie kuja kuleta misaada tu, hata kama hamna kitu msisite kuja kutusalimia na kuongea na sisi, tunaomba Mungu amzidishie mkuu wa mkoa pale alipotoa na siku nyingine tena mtukumbuke” alisema Frank.

Frank alisema watamkumbuka mkuu wa mkoa katika maombi yao ya kila siku kusudi Mwenyezi Mungu amjalie afya njema na maisha marefu na kumpa mafanikio katika safari yake ya uongozi na akawaomba wadau wengine kujitokeza kuwasaidi kama alivyofanya Dkt. Mahenge.

Akizungumza baada ya kupokea msaada huo mratibu wa kituo hicho Editruda Kifumo amemshukuru mkuu wa mkoa kwa msaadaa alioutoa kituoni hapo na kuahidi kumuombea kwa Mungu ili kusudi azidishiwe pale alipopunguza kusaidia watoto hao na kuwa msaada huo umewaongezea ari ya kuwalea watoto hao kwa nguvu na kasi mpya.

Post a Comment

0 Comments