Ticker

6/recent/ticker-posts

RC KILIMANJARO APOKEA MADARASA 56 YA COVID-19 KATIKA SHULE 36 ZA SEKONDARI WILAYANI SAME

Mkuu wa Wilaya ya Same Edward Mpogolo (katikati) akikata utepe kuashiria upokeaji wa madarasa 56 kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kilmanjaro Stephen Kagaigai katika hafla iliyofanyika wlayani Same jana. Wengine ni madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Same.
Mkuu wa Wilaya ya Same Edward Mpogolo, akizungumza wakati akipokea madawati hayo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Same Yusto Mapende akizungumza katika hafla hiyo.
Madiwani wa Halmshauri ya wilaya hiyo wakionesha furaha zao wakati wa kupokea madawati hayo.
Mwonekano wa madarasa hayo kwa ndani.
Muonekano wa madarasa kwa nje baada ya ujenzi wake kukamilika.
Muonekano wa madarasa hayo.
Muonekano wa madarasa hayo.







Na Mwandishi Wetu, Same




JUMLA ya madarasa 56 katika Shule za Sekondari 36 ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro yamekabidhiwa kwa Mkuu wa mkoa huo yakiwa tayari kwa ajili ya wanafunzi watakapofungua shule Januari mwakani.

Zaidi ya kiasi cha Sh. 1.12 Bilioni kimetumika katika kutekeleza ujenzi wa madarasa hayo ambayo yamejengwa na kukamilika kwa wakati.

Akizungumza juzi kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo Stephene Kagaigai wakati wa hafla ya kupokea madarasa hayo kwenye Shule ya Sekondari Kibacha Mkuu wa Wilaya ya Same Edward Mpogolo alisema madarasa hayo yanaenda kuwa muarobaini wa kutatua changamoto ya upungufu wa madarasa ndani ya wilaya hiyo.

Mpogolo alisema Serikali kupitia kwa Rais Samia Suluhu imesikia kilio cha wananchi wa wilaya hiyo na kutoa kiasi hicho cha fedha ambacho kimetekeleza ujenzi wa madarasa hayo ambayo yamejengwa kwa ufanisi mkubwa na kuwa kivutio kikubwa kwa wanafunzi na wananchi.

Mpogolo alisema wanafunzi ambao wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani ni 5217 huku wanafunzi waliomaliza kidato cha nne wakiwa ni 3544 ambapo ukilinganisha idadi ya waliomaliza na wanaoingia kunaongezeko la wanafunzi zaidi ya 1673 jambo ambalo madarasa yaliyokuwapo awali yasingeweza kukidhi.

"Kweli tumepokea madarasa haya kupitia fedha za COVID-19 ambapo sasa ni jukumu letu sisi viongozi na jamii kuwahimiza watoto waweze kusoma kwa bidii huku wakitambua Serikali yao inawajali ambapo tunawaomba viongozi wa maeneo husika kuhakikisha miundombinu ya madarasa hayo inalindwa ipasavyo ili iweze kuwanufaisha watoto wa sasa na vizazi vijavyo".alisema Mpogolo.

Mpogolo ameishukuru Serikali kwa kuwapatia fedha hizo ambazo zimekuja nje ya bajeti na kusukuma gurudumu la maendeleo mbele kwenye wilaya hiyo.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji mradi wa ujenzi wa madarasa hayi Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Same Rogate Nlula alisema ujenzi wa madarasa hayo 56 katika shule 36 ndani ya wilaya hiyo umekamilika kwa wakati na kila chumba cha darasa kina madawati yakutosha tayari kwa matumizi ya wanafunzi mwakani.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Same Yusto Mapende ni alisema kukamilika kwa madarasa hayo kumeibua hisia kubwa na ari kwa wazazi na walezi katika kuhakikisha watoto wao wanafika shuleni na kupata elimu wakiwa kwenye mazingira bora.

Baadhi ya wakuu wa shule za sekondari ndani ya wilaya hiyo akiwemo Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kwambegu, Godwin Kitale na Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kibacha, Onan Kadinde wamesema kukamilika kwa madarasa hayo kutakuwa kumepunguza mlundikano wa wanafunzi madarasani kwani darasa moja lilikuwa likibeba watoto 85 huku pia wakiomba Serikali kuwasaidia ujenzi wa mabweni katika shule za sekondari ndani ya wilaya hiyo.

Post a Comment

0 Comments