Mwenyekiti wa Kata ya Bomang’ombe AMINA YUSUF SWAI akizungumza na waandishi wa habari waliotembelea wanufaika wa mradi wa TASAF kwa kaya masikini wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro leo.
ELIAZA MNYONE mnufaika wa mradi wa TASAF kutoka Kaya Masikini wilayani Hai mkoani Kilimanjaro akitoa ushuhuda wake jinsi TASAF ilivyomsaidia katika kuinua maisha ya familia yake.
Grace Mkie ambaye kilio chake kilikuwa juu ya namna anavyoweza kusomesha watoto wake Tasaf ikatimiza ndoto akitoa ushuhuda wake kwa waandishi wa habari.
ELIAZA MNYONE mnufaika wa mradi wa TASAF kutoka Kaya Masikini wilayani Hai mkoani Kilimanjaro akionesha moja ya biashara yake ya mkaa inayomuingizia kipato baada ya kusaidiwa na TASAF.
Huu ni mradi wa ELIAZA MNYONE wa ufugaji wa kuku na bata biashara ambayo pia inamuingizia kipato.
Bi Fatma Itika ni mmoja wa wanufaika wa TASAF wanaofanya ujasiriamali wa kuuza mchele mara baada ya kusaidiwa na ruzuku ya TASAF.
Bi Seferosa Mnene akifanya biashara ya mboga mboga na matunda katika soko la Kibaoni Kata ya Bomang'ombe wilayani Hai kwa kusaidiwa na TASAF.
Zaidi ya Wakazi 55 wa Kata ya Bomang’ombe wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro ambao kwao mlo mmoja ilikuwa anasa wameondokana na umaskini baada ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) kuwawezesha kuondokana na hali hiyo.
Awali Kata hiyo ilisajili wahitaji 124 lakini sasa wamebaki 69 baada ya baadhi ya wanufaika kupitia Tasaf kuweza kuendesha maisha yao huku wengine wakisomesha watoto wao elimu ya chuo Kikuu.
Mwenyekiti wa Kata ya Bomang’ombe AMINA YUSUF SWAI amesema, baadhi ya wanufaika mbali ya kumudu kujikimu kimaisha, huku wakifanya shughuli mbalimbali za kimaendeleo wameweza kulipia familia zao bima za Afya.
Baadhi ya wanufaika hao ni ELIAZA MNYONE, ambaye kutoka katika mlo mmoja sasa ameweza kuanzisha biashara yake ya mkaa, kufuga kuku wa kienyeji na bata zaidi ya 50 ambao kila wiki wanamwingizia faida ya elfu 50.
“Naishukuru sana Tasaf, maana kupitia biashara hii ya nimeweza kununua kiwanja ambacho kupitia faida ninayoipata nitaweza kujenga nyumba yangu na kuondokana na maisha ya kupanga ninayoishi sasa,” alisema Mnyone.
Nae Grace Mkie ambaye kilio chake kilikuwa juu ya namna anavyoweza kusomesha watoto wake Tasaf ikatimiza ndoto hiyo baada ya kumwezesha kusomesha watoto wake kuanzia ngazi ya elimu ya msingi, sekondari na sasa elimu ya juu.
Wakati mpango huu unakuja mwaka Julai 2014 mwanangu mkubwa alikuwa anaingia kidato cha kwanza wengine wakiwa elimu ya msingi, lakini sasa yupo Chuo cha Mipango Dodoma, huku wengine wakichukua masomo ya diploma ya Uhasibu huko Jijini Arusha.
“Sina cha kuwalipa TASAF maana wameweza kuwa mkombozi, baada ya ujane nilipitia kipindi kigumu sana, lakini kupitia fedha hizo nimeweza kumalizia nyumba yangu, nasomesha watoto na kuendelea na biashara yangu ya kuuza magadi,” alisema Mkie.
Hakuna mradi ambao hauna ukomo, hivyo wanufaika wa Tasaf ambao bado ni wategemezi wametakiwa kujiwekeza ili waweze kujitegemea kama ilivyo kwa wenzao 55 ambao sasa wanaweza kujitegemea wenyewe na kuendesha maisha yao.
0 Comments