Mkutano wa 21 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta (BLM) la Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umefunguliwa leo tarehe 06 Desemba 2021 katika Hotel Verde mjini Zanzibar.
Mkutano huo umeanza na ngazi ya Maafisa Waandamizi kwa lengo la kuandaa taarifa zitakazowasilishwa katika mkutano wa Makatibu Wakuu na Mawaziri. Pia unafanyika ukiwa umewakutanisha nchi wanachama wote isipokuwa wajumbe wawili (Rwanda na Sudan ya Kusini) ambao wanashiriki mkutano kwa njia ya mtandao.
Akifungua mkutano Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia Sekta za Uzalishaji na Jamii, Mhe. Christophe Bazivamo ameeleza umuhimu wa mkutano wa sekta ya afya hasa wakati huu ambapo dunia imetangaza kuwepo kwa wimbi la nne la janga la UVIKO-19.
Mhe. Bazivamo amesisitiza nchi wanachama wa jumuiya ya Afrika Mashariki kuendelea kushirikiana na kamati ya uratibu ya UVIKO-19 ya jumuiya hiyo ili kuweza kuhakikisha tahadhari zinaendelea kutiliwa mkazo sambamba na utolewaji wa chanjo ili kuweza kudhibiti maambukizi mapya ya ugonjwa huo na kuruhusu kuendelea kwa shughuli za kiuchumi kwa ustawi wa wananchi.
“Hakuna nchi iliyo salama dhidi ya janga la UVIKO-19 kwakuwa kama nchi nyingine ndani ya jumuiya haipo salama ni hatari kwa jumuiya yetu na dunia kwa ujumla” alisema Mhe. Bazivamo
Pia alifafanua, kupitia mkutano huo nchi wanachama zitapata fursa ya kusikia taarifa zitakazowasilishwa na kila nchi ili kwa pamoja kuweza kuchangia na kushauri namna bora ya kukabiliana na janga hilo, kuwasilisha changamoto, na maoni yatakayosaidia kusimamia afya za wananchi kwa ujumla.
Vilevile masuala mtambuka yanayozigusa nchi wanachama yatapata nafasi ya kujadiliwa na kupatiwa suluhu ya pamoja. Masuala hayo ni pamoja na; taratibu za kufuatwa mipakani wakati janga la UVIKO-19 likiendelea kudhibitiwa, taratibu za upimaji wa UVIKO-19 ndani ya jumuiya, na kuwezesha usafiri huru wa wafanyakazi, huduma, ajira na bidhaa unasimamiwa kwa maslahi mapana ya jumuiya.
Mkutano huo unafanyika katika ngazi tofauti kwa utaratibu ufuatao:- Tarehe 06 - 08 Desemba 2021 ni Mkutano wa ngazi ya Watalaamu; Tarehe 09 Desemba 2021 ni Mkutano wa ngazi ya Makatibu Wakuu; na tarehe 10 Desemba 2021 ni Mkutano wa ngazi ya Mawaziri.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano wa ngazi ya watalaamu umeongozwa na Dkt. Abdul S. Ali, Mganga Mkuu na Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, akishirikiana na Bw. Eliabi Chodota Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Wajumbe wengine walioshiriki mkutano huo wanatoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na watoto – Tanzania Bara, Wizara ya Afya, Ustawi wa Jami, Wazee, Jinsia, na watoto – Tanzania Zanzibar; Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia, pamoja na taasisi zilizo chini ya Wizara za Afya.
=============================================================
Mwenyekiti wa Mkutano ngazi ya Wataalamu kutoka Jamhuri ya Kenya, Dkt. Kuria Francis akiwakaribisha wajumbe katika Mkutano wa 21 wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofunguliwa leo tarehe 6 Desemba 2021 katika Hotel Verde Mjini Zanzibar.
Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania ambaye pia ni Mganga Mkuu na Mkurugenzi Mkuu wa Wizara ya Afya ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Abdul S. Said (kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Eliabi Chodota wakifatilia mkutano.
Ujumbe wa Tanzania ukifuatilia mkutano.
Sehemu nyingine ya ujumbe wa Tanzania
Ujumbe kutoka Jamhuri ya Burundi
Ujumbe kutoka Jamhuri ya Kenya
Ujumbe kutoka Jamhuri ya Uganda.
0 Comments