Ticker

6/recent/ticker-posts

MIAKA 60 YA UHURU, WANATAALUMA YA USTAWI FANYENI TAFITI MUISHAURI SERIKALI-SOFIA SIMBA


Waziri mstaafu wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia na watoto Sofia Simba akifungua kongamano kuelekea miaka 60 ya uhuru, liliondaliwa na Taasisi ya Ustawi wa Jamii na kufanyika tarehe 8 December 2021Kutoka kushoto, Prof. Mihanjo, Prof. Hosea Rwegoshora, Balozi mstaafu Christopher Liundi, Waziri wa maendeleo ya jamii mstaafu Sofia Simba, Dkt. Joyce Nyoni Mkuu wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii, Dkt. Eventus Mugyabuso kaimu makamu mkuu wa Taasisi Taaluma na Dkt. Zena Mabeyo kaimu makamu mkuu wa Taasisi Utawala fedha na Mipango

Baadhi ya Washiriki wa kongamano la kuelekea miaka 60 ya uhuru.

Picha zote na Ofisi ya Uhusiano ISW

*******************

Na Mwandishi wetu

Waziri mstaafu wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto Sofia Simba amewaasa wanataaluma ya ustawi wa jamii kufanya tafiti na kuishauri serikali ili kuipa mbinu za jinsi ya kutatua matatizo mbali mbali yanayoibuka katika jamii yetu ya kitanzania kwani kila siku yanaibuka matatizo mapya kutokana na maendeleo ya kidunia.

Akizungumza wakati akifungua kongamano hilo ambalo lili jadili mada isemayo ‘’Miaka 60 ya uhuru na ustawi wa jamii kwa maendeleo ya taifa,tulipotoka, tulipo na tunapokwenda’’, waziri mstaafu Simba amesema japo serikali ya hayati Baba wa Taifa Mwl. Nyerere ilifanya jitihada kubwa kuboresha huduma za ustawi wa jamii baada ya uhuru wa Tanganyika, ambapo awali huduma za ustawi wa jamii zilitolewa na wageni wa serikali ya mkoloni pekee bado tunahitaji kuboresha Zaidi.

Katika kutambua umuhimu wa huduma za ustawi wa jamii Serikali ya Mwl. Nyerere iliunda idara ya ustawi wa jamii ili iweze kuratibu, kusimamia na kutoa huduma hizo, aliongeza.

‘’Huduma za Ustawi wa jamii ziliendelea kongezeka kutoka zile za majaribio ya ujenzi wa tabia na kujumuisha huduma za ustawi wa jamii, watoto na malezi, makuzi na maendeleo ya mtoto, wazee na watu wenye ulemavu ambazo zinatolewa kwa misingi ya ushirikishwaji wa jamii na sekta binafsi’’.

Alieleza Nchi yetu ilipiga hatua kubwa sana katika sekta ya ustawi wa jamii mwaka 1973 ilipoanzisha chuo cha ustawi wa jamii ili kuzalisha wataalamu wa ustawi wa jamii hapa nchini.

Fani ustawi wa jamii inatakiwa kuendelea kuboreka na ushirikishwaji wa wadau ndio chachu ya kuboreka huko, hivyo ninyi wanaustawi wa jamii ndio wadau wakubwa kushiriki katika kuboresha hali ya fani ya Ustawi wa jamii nchini.

‘’Kazi bado ipo, bado hatujafikia kile kiwango ambacho tunapaswa kuwa tumefikia hivyo kazi iendelee’’ alisema Waziri mstaafu Simba.

Aidha aliwaeleza wanafunzi wanaosoma fani ya ustawi wa jamii kuwa kazi iliyofanywa na wenzenu waliotangulia katika fani hii toka uhuru, lazima muiendeleze na mtaiendeleza kwa kufanya tafiti ili kupata taarifa sahihi na kuishauri serikali namna bora ya kuboresha ustawi wa jamii yetu.

Waziri mstaafu ,Simba aliongeza kuwa serikali ya awamu ya sita ya Mh. Rais Samia Suluhu Hassan imeendeleza jitihada hizi za kuboresha huduma za ustawi wa jamii kwa ujumla. Ikiwa katika dira ya taifa ya 2025 serikali ya awamu ya sita inahakikisha kuwa maendeleo ya viwanda inaenda sambamba na huduma za ustawi wa jamii.

Aidha serikali inatambua kuwa maendeleo ya uchumi wa viwanda bila huduma za ustawi wa jamii na mapinduzi ya kijamii ni kazi bure hivyo basi imejikita kujenga jamii yenye ustawi bora ikipambana na matumizi mabaya ya madawa ya kulevya, maambukizi ya VVU, majanga na hali za dharura, migogoro ya kifamilia na kijamii, huduma kwa watoto wa mtaani, kushughulikia mimba na ndoa za utotoni, huduma kwa walemavu, wazee na vijana na kushughulikia manyanyaso dhidi ya makundi mbali mbali katika jamii.

Kwa upande mwingine akitoa mada kuhusu miaka 60 ya uhuru na ustawi wa jamii katika kongamano hilo Profesa Hosea Rwegoshora, alieleza kuwa wanaustawi wa jamii ni muda sasa wanahitaji kujiamini, kuwa mstari wa mbele ili kuifanya fani ya ustawi wa jamii kuonekana na kushikika na wanajamii wote.

Alisema Taasisi ya Ustawi wa Jamii ni kitovu cha fani ya Ustawi wa Jamii nchini kwani imezalisha wataalam wengi na ndio chimbuko la fani ya Ustawi wa jamii katika vyuo vingine vingi kwani walikuja kujifunza jinsi ya kundaa mitaala na kufundisha kozi hii nchini hapa Taasisi ya Ustawi wa Jamii.

‘’Kozi hii ya ustawi wa jamii kufundishwa na vyuo vingine ni moja ya mafaniko ya Taasisi hii katika kukuza fani hii hapa nchini’’. Alisema Profesa Rwegoshora..

Aidha Profesa Rwegoshora alibainisha kuwa kuna changmoto katika fani ya ustawi wa jamii na moja wapo ni kutoshirikishwa kwa wanataaluma ya ustawi wa jamii na watunga sera katika masuala mbali mbali kutishia ustawi wa wenye uhitaji ambao unawakilishwa ama kutatuliwa changamoto za maisha na wanaustawi wa jamii ambao hawashirikishwi vyema.

Aliongeza, kuwa ni muda sasa taaluma ya ustawi wa jamii kuanza kujigawanya katika ubobezi wa nyanja za wazee, watoto, vijana, walemavu na makundi mengine na fani ya Ustawi wa jamii kuacha kuwa fani Jumuishi ambayo haina ubobezi katika makundi na nyanja mbali mbali za masuala ya jamii.

Kongamano la kuelekea Miaka 60, pia lilijadili mada mbali mbali zikiwa pamoja na miaka 60 ya uhuru na namna ya kukomesha ukatili wa kijinsia, miaka 60 ya uhuru na maendeleo ya kielimu na mtoto wa kike ambapo Dkt. Leah Omary kutoka Taasisi ya Ustawi wa Jamii alieleza mafanikio makubwa katika miaka 60 ya uhuru kuwa ni elimu bure kwa mtoto wa kike na watoto wa kike waliopata mimba kupata fursa ya kurudi shule na kuendelea na masomo.

Mada nyininge ni Miaka 60 ya uhuru na huduma ya afya kwa makundi maalum, miaka 60 ya uhuru na maendeleo ya nchi. Miaka 60 ya uhuru tulipotoka na tunaelekea.

Post a Comment

0 Comments