Ticker

6/recent/ticker-posts

MFUKO WA MAENDELEO WA ABU DHABI WAAHIDI KUWEKEZA NCHINI TANZA


Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kulia) akiwa na mwenyeji wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi, Falme za Nchi za Kiarabu Mohammed Saif Al Suwaidi, walipokutana na kufanya mazungumzo namna ya kupata mikopo nafuu na misaada kutoka katika Mfuko huo kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya kimkakati nchini Tanzania. Katikati ni Waziri wa Nchi-Ofisi ya Rais-Fedha na Mipango-Zanzibar, Mhe. Jamal Kassim Ali, Mjini Abu Dhabi.


Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kushoto) akifurahia jambo wakati wa mazungumzo na mwenyeji wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi, Falme za Nchi za Kiarabu, Bw. Mohammed Saif Al Suwaidi, walipokutana na kufanya mazungumzo namna ya kuendeleza ushirikiano kati ya Tanzania na Taasisi hiyo ya Fedha, Mjini Abu Dhabi.


Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kushoto) akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na mwenyeji wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi, Falme za Nchi za Kiarabu, Bw. Mohammed Saif Al Suwaidi, walipokutana na kufanya mazungumzo namna ya kuendeleza ushirikiano kati ya Tanzania na Taasisi hiyo ya Fedha, Mjini Abu Dhabi, Falme ya Nchi za Kiarabu.

Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kushoto) wakibadilishana mawasiliano na mwenyeji wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi, Falme za Nchi za Kiarabu, Bw. Mohammed Saif Al Suwaidi, baada ya kukutana na kufanya mazungumzo namna ya kuendeleza ushirikiano kati ya Tanzania na Taasisi hiyo ya Fedha, Mjini Abu Dhabi, Falme ya Nchi za Kiarabu.


Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (wa nne kushoto) ukiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe kutoka Mfumo wa Maendeleo wa Abu Dhabi, Falme ya Nchi za Kiarabu ukiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Bw. Mohammed Saif Al Suwaidi (katikati), Mjini Abu Dhabi, Falme ya Nchi za Kiarabu.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini- Wizara ya Fedha na Mipango-Abu Dhabi)

*************************

Na Benny Mwaipaja, Abu Dhabi

MFUKO wa Maendeleo wa Abu Dhabi wa Falme ya Nchi za Kiarabu, umeahidi kushirikiana na Tanzania kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati itakayo harakisha maendeleo ya watu ikiwemo sekta za kilimo na mifugo pamoja na utalii.

Ahadi hiyo imetolewa mjini Abu Dhabi, Falme za Nchi za Kiarabu na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo Bw. Mohammed Saif Al Suwaidi, alipokutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.

Al Suwaidi alisema kuwa Mfuko huo umekuwa na ushirikiano mkubwa na Tanzania na kwamba pamoja na kuahidi kutoa fedha kwa njia ya mikopo nafuu na misaada lakini watakuja kuwekeza moja kwa moja kwenye miradi ya kilimo na utalii.

Aidha Mkurugenzi Mkuu huyo wa Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi, Bw. Mohammed Saif Al Suwaidi alimwahidi Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba na Waziri wa Nchi-Ofisi ya Rais-Fedha na Mipango Mhe. Jamal Kassim Ali kwamba atawaunganisha na sekta binafsi ya Abu Dhabi ili wawekeze nchini Tanzania.

“Tuna mambo mengi sana ya kufanya pamoja katika upande wa maendeleo na uhusiano kwa njia ya kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu kama tunavyofanya hivi sasa kwa kufadhili baadhi ya miradi nchini Tanzania lakini jambo la pili ni kuwekeza mitaji moja kwa moja katika maeneo ambayo tunaamini yana tija” alisema Mohammed Al Suwaidi

Kwa Upande wake Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba aliuomba Mfuko huo kusadia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi kadhaa ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa, Bwawa na Umeme la Mwalimu Nyerere, Ujenzi wa nyumba katika sekta za elimu, afya, kilimo na mifugo.

Alisema kuwa kukamilika kwa mtandao wa Reli ya Kisasa inayojengwa hivi sasa ambao ujenzi wake unaendelea kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza, kutachangia maendeleo ya nchi kwa kufungua fursa mbalimbali za kiuchumi zinazopatikana kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu hususan kwenye nchi 6 zinazopakana na Tanzania ambazo hazijazungukwa na bahari.

Naye Waziri wa Nchi- Ofisi ya Rais-Fedha na Mipango-Zanzibar Mhe. Jamal Kassim Ali, alisema kuwa nchi yake inahitaji kusadiwa kujenga makazi 10,000 yenye gharama nafuu kwa ajili ya kuwauzia watumishi wa umma na wananchi wengine, kuendeleza sekta ya mafuta na gesi, afya, kuimaarisha utalii pamoja na ujenzi wa Bandari ya Manga Pwani.

“Bandari hii itakuwa na matumizi mtambuka ambapo kutakuwa na eneo la kuhifadhi kontena, sehemu ya kuhifadhi mafuta na gesi, bandari kavu na eneo maalumu la uwekezaji kiuchumi” Alisema Mhe. Ali

Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi umetoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini Tanzania ukiwemo ujenzi wa Hospitali ya Wete-Pemba, barabara ya Kidawe hadi Uvinza, ujenzi wa Kiwanda cha Sukari cha Kagera na mradi wa maji Zanzibar vijijini ambayo imekamilika na hivi sasa wanafadhili ujenzi wa barabara ya Uvinza-Ilunde hadi Malagarasi wenye thamani ya dola za Marekani milioni 15.

Post a Comment

0 Comments