Ticker

6/recent/ticker-posts

MAKAMBA AWAONGOZA WANACHAMA NA WAGENI WA TAASISI YA VOLUNTEERS IN DEVELOPMENT


***************

Na. Mwandishi Wetu-MAELEZO Waziri wa Nishati Mhe. January Makamba amewaongoza wanachama na wageni mbalimbali wa taasisi ya Volunteers in Development katika hafla ya matembezi kwa ajili ya kukusanya fedha za kuwanunulia yatima vifaa vya shule kwa mwaka mpya wa masomo 2022.

January Makamba ameongoza matembezi hayo yaliyofanyika Green Sports Park Masaki, Dar es Salaam tarehe 5 Disemba, 2021. “Nawapongeza viongozi wa taasisi ya Volunteers in Development kwa juhudi zenu za kuwasaidia watoto yatima na pia nawapongeza kwa kunipa heshima ya kuwa mgeni rasmi kwenye shughuli hii,” alisema Makamba.

“Hali za watoto yatima na madhila wanayopitia zinafahamika. Wengi hawana uhakika wa kupata mahitaji muhimu ya maisha kama ya malazi, chakula, mavazi, kupelekwa shule kupata elimu na kadharika” alisema Makamba.

“Niwapongeze waliokuja na watoto wao kwa ajili ya zoezi hili la kuchangia yatima, naamini nao watawarithisha watoto wao,” alisema Makamba.

Vilevile aliwashukuru viongozi wa taasisi hiyo kwa kujitoa kwao kuwasaidia watoto yatima, alisema kuwa, zipo taasisi nyingi zinazofanya shughuli hii lakini hazina uwezo wa kutosha wa kifedha wa kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu.

Aidha, alishauri jamii nzima kushirikiana na taasisi kama hizi ili kusaidia yatima na wale ambao wana hali duni za kiuchumi. Katika risala iliyosomwa na Tune Salim ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa taasisi hiyo, taasisi hiyo ilianzishwa mwaka 2011 na ilianzia katika mtandao wa Facebook ambapo wanachama wake wengi ni wanawake. Wengi wa wanawake hawa ni kutoka Tanzania na Kenya. Tune Salim alipokuwa akitoa maelezo juu ya Taasisi hiyo, alisema kuwa , Taasisi hiyo ina yatima zaidi ya 865 waliopo Dar es Salaam, Unguja, Pemba, Bagamoyo, Tanga, Mwanza, Arusha na Mkuranga.

Aliendelea kusema kuwa, Taasisi hiyo imejikita katika kuwasaidia yatima katika nyanja mbalimbali kama vile; kuwapatia chakula na nguo msimu wa sikukuu, kusaidia yatima katika nyanja za kielimu hasa vifaa vya shule, kuratibu na kugharamia semina za ushauri wa kielimu kwa watoto yatima, kusaidia wagonjwa mbalimbali ambao hawana uwezo wa kumudu gharama za matibabu na pia kusaidia jamii kwenye ujenzi wa visima na zahanati.

Post a Comment

0 Comments