Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akipata maelezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uhifadhi Mazingira Mufindi mkoani Iringa Waston Mkane alipokwenda kukagua Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi kwenye eneo la chanzo cha maji cha Mpogolo kijiji cha Idetelo kata ya Mbalamaziwa wilayani Mufindi mkoani Iringa jana. Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akipata maelezo kwenye eneo la chanzo cha maji cha Mpogolo kijiji cha Idetelo kata ya Mbalamaziwa wilayani Mufindi mkoani Iringa alipokwenda kukagua Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi katika eneo hilo jana. Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wakazi wa kijiji cha Idetelo kata ya Mbalamaziwa wilayani Mufindi mkoani Iringa alipokwenda kukagua Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi katika eneo la kijiji hicho jana. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Saadi Mtambule Sehemu ya wakazi wa kijiji cha Idetelo kata ya Mbalamaziwa wilayani Mufindi mkoani Iringa wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alipokwenda kukagua Mapango wa Matumizi Bora ya Ardhi katika eneo hilo jana. (PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA WIZARA YA ARDHI)
***********************
Na Munir Shemweta, WANMM MUFINDI
Serikali imewataka wananchi wanaoishi maeneo yanayofanyiwa Mipango wa Matumizi Bora ya Ardhi kukubaliana na mabadiliko katika maeneo yao ili kuepuka athari zinazoweza kutokea ikiwemo ile ya uharibifu wa mazingira kwenye vyanzo vya maji.
Hayo yalibainishwa jana na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Idetelo kilichopo kata ya Mbalamaziwa wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.
Dkt Mabula aliwaomba wananchi kuzingatia utaratibu waliojiwekea kupitia Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi kwa kuwa mpango huo unainisha maeneo mbalimbali kama vile kilimo, ufugaji na huduma nyingine za jamii na tofauti yoyote ya utekelezaji wake italeta athari kubwa ikiwemo za kimazingira.
Aliwaelezea wakazi wa Idetelo wanaofanya shughuli za kilimo katika ukingo wa chanzo cha maji cha Mpogolo kuwa, wanao wajibu wa kuhakikisha Mpango huo unazingaitwa kwa kuwa chanzo hicho ni muhimu kutokana na kupeleka maji mto Ruaha unaopeleka maji pia kwenye mradi mkubwa wa umene wa bwawa la Mwl Nyerere alilolieleza litakapokamilika litakuwa msaada mkubwa wa umeme nchini.
‘’Niwaombe mzingatie huu mpango wa matumizi bora ya ardhi ulioletwa kwa kuwa utaepusha athari ya uharibifu wa mazingira na wazee wangu ninyi ni mashahidi Idetelo iliyokuwa miaka ya nyuma ni tofauti kabisa na ya sasa’’ alisema Dkt Mabula.
Wananchi wa kijiji cha Idetelo kupitia mkutano na Naibu Waziri wa Ardhi, pamoja na kukubalina na maamuzi ya serikali ya kuacha kufanya shughuli za kilimo kwenye ukingo wa chanzo cha maji cha Mpogolo wameiomba serikali kuwatafutia njia mbadala itakayowawezesha kujipatia kipato cha kuendesha maisha yao kwa kuwa mategemeo yao yalikuwa chanzo hicho.
Dkt Mabula alishauri upangaji mipango ya matumizi bora ya ardhi uzingatie mahitaji ili kuepuka migogoro na kubainisha kuwa eneo la hekta 40 zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za ufugaji katika kijiji cha Idetelo ni dogo na hali hiyo inaweza kuzua migogoro kati ya wakulima na wafugaji.
‘’Hapa wafugaji ni wengi lakini maeneo machache hivyo tunatakiwa kuwashauri wafugaji namna bora ya ufugaji ikiwemo ‘zero grazing’ na wakulima tuwashauri kilimo kisichoharibu ecolojia’’ alisema Naibu Waziri Mabula.
Aidha, alizitaka halamashauri zote nchini zenye mipango ya matumizi bora ya ardhi kuhakikisha mipango hiyo inasimamiwa pamoja na halmashauri hizo kutenga fedha za utekelezaji wake sambamba na kutoa elimu kwa wananchi ili mpango huo ufahamike na kutekelezwa kwa ufasaha.
Akigeukia taasisi zisizokuwa za kiserikali zinazojishughulisha na kazi za mipango matumizi ya ardhi katika maeneo mbalimbali Dkt Mabula alizitaka taasisi hizo kuhakikisha zinazingatia sheria ikiwa ni pamoja na kuwa na mawasilianao na Tume ya Taifa ya Matumizi Bora ya ardhi ili mipango hiyo iingizwe kwenye mipango ya serikali.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mufindi Saadi Mtambule alisema, mpango wa matumizi bora ya ardhi katika wilaya hiyo sasa unaenda kupunguza migogoro ya ardhi katika eneo hilo na kusisitiza kuwa wilaya hiyo haitakuwa sehemu ya kukwamisha mradi huo.
‘’Wilaya yangu haitakuwa sehemu ya kukwamisha mpango huu wa matumizi bora ya ardhi na changamoto kubwa hapa ni mabadiliko ya tabia nchi yaliyosababisha maji kupungua sana kutokana na uharibifu wa mazingira na hali hii haijawahi kutokea, vinyumgu tunavihitaji lakini kesho vitapotea’’ alisema Mtambule.
Tume ya Taifa ya Matumizi Bora ya Ardhi inatekeleza mradi wake wa Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo yale miradi ya kimkakati na takriban wananchi 5,738 wameshafikiwa mpango huo.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameutaka mkoa wa Iringa kuongeza kasi ya ukusanayaji mapato yatokanayo na kodi ya pango la ardhi sambamba na umilikishaji ili kuiwezesha serikali kupata mapato katika sekta hiyo.
Hatua hiyo inafuatia ripoti ya mkoa huo kuonesha baadhi ya halmashauri katika mkoa huo kuwa nyuma katika suala la ukusanayaji mapato yatokanayo na kodi ya pango la ardhi na utoaji hati za ardhi kuwa chini.
‘’Ilipoelezwa msitumie nguvu katika kudai kodi kumewafanya watendaji wengi ‘kurelax’ na kuwaacha wadaiwa sugu bila kuwadai, wakurugenzi muwabane watendaji wenu wafanye kazi kwa bidii maana haiwezekani ndani ya miezi sita halmashauri ya Mufindi inatoa hati tisa tu’’ alisema Dkt Mabula/
Hata hivyo, ameipongeza halmashauri ya Mufindi kwa kutoa hati nyingi za kimilla kwa wamiliki ambapo halmashauri hiyo imetoa jumla ya hati 2,173 kati ya hati 2,400 ilizojipangia katika utekelezaji wake na kuelezea hali hiyo kuwa inalenga kuwawezesha kiuchumi pamoja na kuondoa migogoro ya ardhi.
0 Comments